2. Afya

Damu kutoendana, nadharia au uhalisia?

Mpendwa msomaji pengine umeshapata kusikia watu mbalimbali wakihadithia suala la damu kutoendana baina ya wanandoa. Binafsi nimepata kusikia kisa cha mama mmoja aliyewahi kubeba mimba mara sita, na kuharibika zote isipokua ya kwanza. Nilipouliza watu wanahisi nini sababu?Nikajibiwa kuwa ‘pengine, damu zao haziendani’.

Kwa lugha ya kitaalamu tatizo hili hujulikana kama ‘rhesus incompatibility’ na hutokea tu mama mwenye damu hasi akikutana na mwanaume mwenye damu chanya.

Ndugu msomaji, nadharia ya damu kutoendana ni jambo la kweli kabisa na pia limekuwa tatizo kubwa sana linalosababisha ujauzito kuharibika.

Ungana nami katika makala hii kujionea nini hasa maana ya damu kutoendana, pamoja na hatua za kufuata ili kuepuka tatizo la kuharibika ujauzito ikiwa damu haziendani.

Aina tofauti za makundi ya damu

Ingawa haina tofauti kwa muonekano, lakini damu inaweza kuwa tofauti baina ya mtu na mtu. Tofauti hizi zimepelekea damu kugawanywa katika makundi makuu manne ambayo ni A, B, AB na O.

Mbali na hayo, makundi haya pia yamegawika katika sehemu kuu mbili yaani, hasi na chanya (rhesus positive & rhesus negative). Hasi na chanya za kwenye damu zinatokana na kuwepo ama kutokuwepo kwa kemikali maalum inayoitwa ‘rhesus’ ambayo hupatikana kwenye uso wa seli nyekundu za damu.

Ikiwa mtu yoyote atakua na kemikali hii, basi huyo atakuwa katika kundi chanya. Ikiwa hana, atakuwa kundi hasi. Kwa maana hiyo, tuna makundi ya damu A+, A-, B+, B-, AB+, AB-, O+ pamoja na kundi O-.

Undani wa damu kutoendana

Ndugu yangu msomaji, kwa kawaida mtoto hurithi kundi la damu kutoka kwa wazazi wote wawili, ila hurithi hasi ikiwa wazazi wote wakiwa hasi, hurithi chanya ikiwa wazazi wote ni chanya au mmoja kati ya wazazi atakua chanya na mwengine hasi. Yaani, kwa lugha rahisi, mtoto hasi hana nafasi mbele ya chanya. Suala la damu kutoendana hutokea ikiwa mwanamke mwenye kundi lolote la damu ambalo ni hasi ( A-, B-, AB-, O-) atashika ujauzito wa mwanaume mwenye chanya (A+, B+, AB+, O+) kwani mtoto aliye tumboni atakua na kundi chanya, na mwili wa mama huyu huiona chanya iliyo kwa huyu mtoto ni sumu inayotishia usalama wa mwili wake.

Kwa ujauzito wa kwanza, mtoto huyu atakuwa na kuzaliwa vizuri kwani licha ya kuwepo kwa hisia za kuwa mtoto huyu ni sumu, mwili wa
mama bado unakua haujatambua sumu hii hasa ni ya aina gani na ipi ni njia sahihi ya kupambana nayo. Kwa sababu hiyo, mtoto huyu huokoka.

Hata hivyo, kuokoka kwa mtoto wa kwanza ndiyo husababisha hatari kwa mimba zitakazofuata kwani kiasi kidogo cha damu ya mtoto huyu huingia kwenye damu ya mama na hapo ndipo mwili wa mama unapopata taarifa kamili juu ya ile sumu (damu chanya) na kuanza kutengeneza kemikali maalum ya kukabiliana nayo.

Kemikali hii iliyoandaliwa sasa huwa tayari kuangamiza damu chanya inayoweza kujitokeza wakati mwengine, yaani mimba nyengine. Hivyo, mimba zote zitakazofuata zitaathiriwa na kuuliwa na kemikali hii iliyotengenezwa na mwili wa mama.

Namna ya kukabiliana na tatizo hili

Kabla ya kuamua kushika ujauzito ni vizuri sana mume na mke kufahamu makundi yao ya damu. Ikiwa mwanamke atakuwa na kundi chanya, basi kwake haitakua na athari yoyote ile bila kujali mume ana kundi gani ila hali ni tofauti kwa wanawake wenye kundi hasi.

Ikiwa mume atakua hasi, basi hakutakua na tatizo lolote. Lakini mume akiwa chanya, basi ni lazima mwanamke huyu mwenye hasi kupata tiba maalum ndani ya masaa 72 baada ya kujifungua mtoto wa kwanza. Bila ya tiba hii, mwili wake utatengeneza kemikali za kudumu ambazo zitaangamiza mimba zote zitakazofuata

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close