2. Afya

Aina za maumivu ya tumbo na maana zake -2

Kwa kujikumbusha, katika makala iliyopita tulipata kujionea ya kuwa kitaalamu tumbo limegawanyika katika maeneo makuu tisa. Tukianzia katikati ya tumbo tunapata eneo la kitovuni (umbilical area), eneo la juu ya kitovu (epigastric are), maeneo ya kushoto na kulia ya eneo la juu ya kitovu (hypochondriac regions), maeneo ya kushoto na kulia mwa kitovu (lumbar areas), eneo la chini ya kitovu (suprapubic area) pamoja na maeneo ya kushoto na kulia mwa eneo la chini ya kitovu (iliac regions).

Maumivu kulia chini ya kitovu
Kama tunavyojua ya kuwa, eneo hili hujulikana kama ‘right iliac region’ na ndipo utumbo utumbo mdogo hukutana na utumbo mkubwa. Pia katika eneo hili ndipo panapopatikana kiungo kingine kidogo kinachoitwa kidole tumbo ‘appendix’.

Maambukizi au uvimbe katika kidole tumbo huweza kusababisha maumivu makali katika eneo la kulia chini ya kitovu na maumivu haya yanaweza kuwa ya kuja na kuondoka kutegemeana na aina ya ugonjwa.

Magonjwa mengine yanayoweza kusababisha maumivu katika eneo hili ni pamoja na ugonjwa wa kuvimba kuta za utumbo (inflammatory bowel disease), ugonjwa wa kukosa choo na pia magonjwa mengi yanayohusiana na mfumo wa uzazi wa mwanamke yanaweza kusababisha maumivu katika eneo hili.

Maumivu kushoto chini ya kitovu
Kwa lugha ya kitaalamu eneo hili hujulikana kama ‘left iliac region’. Katika eneo hili ndipo sehemu za mwisho za utumbo mkubwa hupita hivyo magonjwa mengi ya utumbo mpana huweza kusababisha maumivu katika eneo hili. Pia ugonjwa wa kukosa choo, ngiri na baadhi ya magonjwa ya mfumo wa uzazi wa mwanamke husababisha maumivu katika eneo hili.

Maumivu ya chini ya kitovu
Eneo hili la hypogastric region, ndilo huenda likawa eneo linalokumbwa na maumivu kuliko maeneo yote ya kwenye tumbo. Wingi wa maumivu haya ni kwa sababu mifumo mitatu ya mwili hupatikana katika eneo hili.

Mifumo hii ni pamoja na mfumo wa chakula, mfumo wa mkojo pamoja na mfumo wa uzazi hasa wa wanawake. Kwa wanaume, maumivu chini ya kitovu mara nyingi husababishwa na maambukizi katika kibofu cha mkojo, tezi dume, ngiri pamoja na baadhi ya magonjwa ya utumbo. Kwa wanawake, pia magojwa ya kibofu cha mkojo na utumbo husababisha maumivu katika eneo hili. Mbali na hayo, takriban magonjwa yote yanayohusiana na mfumo wa uzazi huweza kusababisha maumivu katika eneo hili.

Maumivu yasiyo na chanzo
Mbali na kuwepo kwa vyanzo mbalimbali vya maumivu, yapo baadhi ya maumivu ambayo hayatokani na aina yoyote ya ugonjwa wa kiungo fulani au kuumia katika eneo husika.

Maumivu ya namna hii, yasiyo na chanzo maalumu, hutokana na ugonjwa unaohusiana na akili (somatoform disorder).

Ugonjwa huu wa akili humfanya mgonjwa kupata maumivu katika maeneo tofauti ya mwili bila ya kuwepo ugonjwa wowote unaoathiri eneo husika na kwa kawaida maumivu ya namna hii huweza kudumu kwa muda mrefu na kutotibika kwa tiba za kawaida za kuponesha maumivu.

Pia ugonjwa huu wa ‘somatoform disorder’ huweza kusababisha maumivu katika sehemu nyingine za mwili. Pia, dalili nyingine kadhaa huweza kutokea sambamba na maumivu haya. miongoni mwa dalili hizi ni pamoja na mwili kupata ganzi, kupooza, kupata upofu na nyinginezo nyingi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close