2. Afya

Afya ya akili: Tatizo kubwa

Oktoba 10 kila mwaka ni Siku ya Afya ya Akili Duniani. Mwaka huu, siku hiyo imekuja kipekee kwa sababu ya changamoto mpya zilizotokana na maradhi hatari ya Covid -19. Covid – 19 imetajwa kuchangia ongezeko la wagonjwa wa akili kwa sababu ni maradhi yaliyoleta athari kubwa kiuchumi, kijamii kwa watu wengi.

Watu wengi wamepoteza ajira na vipato kwa sababu ya maradhi haya ambayo yalisimamisha shughuli nyingi za kiuchumi na kibiashara, na kuongeza masikini wa kutupwa.

Mathalan Covid -19 iliua kabisa sekta ya utalii ambayo imeajiri watu wengi. Kwa baadhi ya mataifa, sekta ya utalii ndiyo tegemeo, ndiyo kila kitu, na ilipodondoka ikawaacha watu wengi bila ajira. Sekta nyingine zilizoathirika ni usafiri, biashara za kupeleka bidhaa nje ya nchi na kuingiza, biashara ndogondogo na kadhalika.

Kudondoka kwa ajira kulipelekea watu kukumbwa na msongo mkubwa wa mawazo, na hivyo kuongeza idadi ya wenye matatizo ya akili. Kutokana na umaalumu huu wa siku ya afya ya akili yam waka huu, inategemewa kuwa uhitaji wa huduma ya matibabu ya afya ya akili itahitajika zaidi katika miezi na miaka michacho ijayo.

Kwa sababu hiyo, kauli mbiu ya mwaka huu la Siku ya Afya ya Akili Duniani ni haja ya kuongeza uwekezaji zaidi katika huduma za afya za akili.

Covid -19, kidonda chumvi

Changamoto zilizotokana na corona zilizoongezeka katika sekta ya afya ya akili ni kama zimeongeza chumvi, pilipili na limau kwenye kidonda kibichi. Hii ni kwa sababu, hata kabla ya changamoto za corona, kumekuwa na huduma hafifu ya matibabu katika nchi maskini, hususan za barani Afrika.

Uhafifu huo wa huduma umepelekea familia kushindwa kuwapa wagonjwa uangalizi wa kutosha na wakitaalamu wagonjwa na matokeo yake ndugu wamekuwa wakiwafungia wagonjwa ndani na kuwafanya waishi kama wapo kifungoni.

Kutokana na kutopatikana kirahisi kwa huduma za kisasa za matibabu ya wagonjwa wa akili na kutokana na imani za kishirikina, si ajabu kuona katika nchi nyingi maskini wagonjwa wa akili wakikimbizwa kwa waganga wa kienyeji ambako hamna huduma za kisayansi bali nyingi hutegemea ramli.

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema mamia ya watu wenye matatizo za afya za akili kote ulimwenguni wanakabiliwa na vifungo.

Wagonjwa wa makundi yote, wanaume kwa wanawake, bila kusahau watoto na wazee, wamekuwa wakifungiwa kwenye vyumba vidogo kwa wiki, miezi ama hata miaka. Kulingana na ripoti hiyo, haya yanafanyika kwenye mataifa angalau 60 huko Asia, Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati na hata Amerika.

Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya watu 350 wenye matatizo ya akili miongoni mwao watoto, familia za watu 430, watumishi wa vituo vya wagonjwa hao, wataalamu wa magonjwa ya afya ya akili, matabibu wanaoponya kwa imani, maafisa wa serikali na wapigania haki za watu wa aina hiyo.

Ripoti hiyo ya kurasa 56 iliyopewa jina “Kuishi na minyororo: Vifungo vya watu wanaoishi na matatizo ya kiakili ulimwenguni”, inaangazia namna gani watu hao wanavyokabiliwa na vifungo vya mara kwa mara majumbani ama kuzingirwa na uchafu kinyume na ambavyo wangetamani kuishi kutokana na kuongezeka kwa unyanyapaa na kukosa huduma za maradhi hayo.

Wengi hushurutishwa kula, kulala, kujisaidia haja ndogo na hata kubwa kwenye chumba hicho hicho kidogo wanachoishi wakiwa na minyororo ikiwa imezungushwa kwenye vifundo vya miguu yao.

Na hata kwenye vituo vya huduma za afya vya serikali ama binafsi pamoja na vile vya kidini ama vya kienyeji, mara nyingi wagonjwa hawa hulazimishwa kukaa bila kula, kunywa dawa za kienyeji na zaidi kunyanyaswa kingono.

Ripoti hii inajumuisha tafiti zilizofanywa kwenye maeneo kadha wa kadha pamoja na shuhuda kutoka Afghanistan, Burkina Faso, Cambodia, China, Ghana, Indonesia, Kenya, Liberia, Mexico, Msumbiji, Nigeria, Sierra Leone, Palestina, jimbo lililojitangazia uhuru la Somaliland, Sudan Kusini, na Yemen.

Wakati ni kweli kuwa familia ina wajibu mkuu na wa msingi katika kumuangalia ndugu yao mgonjwa wa akili, hakuna kikubwa wanachoweza kufanya bila uwezeshaji wa serikali, kupitia kuwekeza katika huduma ya matibabu ya maradhi hayo.

Ulimwenguni kote, inakadiriwa watu milioni 762 ama 1 kati ya 10 ikiwa ni pamoja na Watoto 1 kati ya 5 wana matatizo ya afya za akili. Lakini hata hivyo, serikali zinatumia chini ya asilimia 2 ya bajeti zao za afya kuwatibu wagonjwa hao.

Pamoja na kukosekana huduma, changamnoto nyingine ni ukosefu wa ufahamu. Inatajwa kuwa, familia nyingi zinahisi kuwa hazina chaguo lengine zaidi ya kuwafungia ndani ndugu zao. Wanafamilia mara nyingi huhofia kwamba wanaweza kukimbia ama kujiumiza wenyewe.

Familia ambazo hasa huwafungia wagonjwa ni zile zinazoamini maradhi hayo husababishwa na ushirikina ama kutenda dhambi. Pia, matra nyingi, kabla ya kuwafungia wanafamilia huhangaika kwanza kuwapeleka ndugu zao hao kwa waganga wa kienyeji ama kuombewa na ikishindikana kabisa mara chache ndiyo hukimbilia hospitali.

Kutokana na umuhimu wa mada hii, wiki ijayo tutaanza kujadili mambo anuai kuhusu afya ya akili ikiwemo ni nini, husababishwa na nini, viashiria vyake, huduma za matibabu, Imani potofu kuhusu maradhi haya na mengineyo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close