2. Afya

Acha tumbaku, itakuua au kukutesa.

Tumbaku ni moja ya vileo vinavyotumiwa na idadi kubwa ya watu. Wengi huamini kuwa pengine tumbaku haina madhara yoyote, na baadhi huamini kuwa madhara yake ni madogo na mtu anaweza kuyapata tu ikiwa atatumia kwa muda mrefu kwa muda mrefu.

 Lakini takwimu za mwaka huu zilizochapishwa katika tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha hali tofauti. Madhara ya tumbaku ni makubwa kuliko unavyofikiri!

Katika kilichonishtua zaidi katika takwimu hizo ni kuwa, tumbaku huua hadi nusu ya watumiaji wake!

Kati ya watu zaidi ya milioni nane wanaokufa kwa maradhi yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku kila mwaka, vifo milioni saba ni matokeo ya matumizi ya moja kwa moja ya tumbaku na vifo takriban milioni 1.2 vinatokana na madhara ya moshi!

Si hivyo tu, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watumiaji bilioni 1.3 duniani kote wapo katika nchi za kipato cha kati na chini ambako huduma za afya ni dhaifu.

Pia, karibu nusu ya watoto huvuta hewa iliyochafuliwa na moshi wa tumbaku wanapokuwa katika maeneo ya jumuiya; na kati yao watoto 65,000 hufa kutokana na maradhi yatokanayo na moshi kutoka kwa watumiaji.

Kama hiyo haitoshi, kwa vitoto vichanga, moshi wa sigara unaongeza hatari ya vifo vya ghafla. Kwa wanawake wajawazito nao, taarifa zinaonesha kuwa moshi wa tumbaku hupelekea shida mbalimbali wakati wa kuzaa. Pia, hupelekea watoto kuzaliwa na uzito mdogo.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, imethibitika kuwa sigara huathiri takriban mifumo yote mikuu ya mwili lakini ni mfumo wa upumuaji ndiyo huathirika zaidi. Pia, sigara husababisha maradhi ya moja kwa moja kwa baadhi ya viungo tofauti vya mwili.

Tumbaku huathiri mfumo wa fahamu, mfumo wa upumuaji, mfumo wa mishipa ya damu, mfumo wa chakula, mfumo wa uzazi, ngozi, nywele na kucha …tukitaja michache.

Kwa upande wa mfumo wa fahamu, tunaambiwa kuwa moja kati ya kemikali kuu zilizomo ndani ya sigara ni nikotini ambayo husafiri moja kwa moja hadi kwenye ubongo na kumfanya mtumuaji kujihisi ameongezeka nguvu kidogo. Hisia hizi hudumu kwa muda mfupi, na baadae kidogo uchovu na uchu wa kuvuta sigara nyingine hurudi kwa kasi na mwishowe kumfanya muhusika kuwa ‘teja’ wa sigara.

Kwa upande wa upumuaji, moshi wa sigara unapoingia mwilini taratibu huathiri mapafu na baada ya miaka kadhaa kiungo hicho muhimu huharibika na kushindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi. Pia, aghlabu mapafu ya wavuta sigara hushambuliwa na bakteria na huweza kupelekea mvutaji kupata maradhi ya saratani ya mapafu na maradhi mengine ya hatari.

Vile vile, sumu ya nikotini katika moshi wa sigara huharibu mfumo mzima wa mzunguko wa damu na kusababisha kusinyaa kwa mishipa na hatimaye hupelekea mtumiaji kupata shinikizo la juu la damu. Kiharusi na shambulio la moyo ni maradhi mengine hatari yanayoweza kuchochewa na sumu zilizopo katika moshi wa sigara.

Je wajua kuwa uvutaji wa sigara huongeza hatari ya kuugua saratani ya kinywa, koo pamoja, kongosho, mapafu na ngozi. Pia, moshi wa sigara huweza kupelekea vidonda vya tumbo na kisukari.

Kama hiyo haitoshi, wanaume wanaovuta sigara wamekuwa wahanga wakuu wa magonjwa ya upungufu wa nguvu za kiume kutokana na kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu katika sehemu za kiungo cha uzazi. Wanawake wavutaji nao wanaweza kupata ugonjwa wa kupungua maji maji katika sehemu za siri na hivyo kupelekea maumivu wakati wa tendo la ndoa.

Moshi wa tumbaku hufubaza ngozi na kumfanya mvutaji kuonekana mzee, huharibu nywele na kusababisha mvi au kipara. Kwa ujumla, tumbaku ni mbaya mno na ndiyo maana wanazuoni wengi wa Kiislamu wamehukumu kuwa uvutaji tumbaku ni haramu kwa sababu ni sawa na kujiua.

Achilia mbali maradhi yanayoweza kuletwa na moshi wa sigara na uharamu katika dini, tumbaku pia inamaliza pesa. Hivyo, kuacha kuvuta tumbaku ni kuokoa pesa, ni kujiweka katika uwezekano wa kuishi muda mrefu katika afya njema. Ukiacha tumbaku utapata usingizi mzuri, utapona vidonda mapema, utaweza kujitawala (sio kutawaliwa na nikotini), utalinda wanaokuzunguka, utalinda afya yako ya akili, na utadhibiti harufu mbaya… Faida ni nyingi mno.

Wengi wamejikuta katika janga la Acha tumbaku, itakuua au kukutesa uvutaji sigara na hawawezi kutoka kwa sababu ya sumu ya nikotini inayokuchochea utake kuvuta na kukufanya uwe teja au mraibu wa sigara. Ushauri wangu ni kuwa, kama hujaanza, kaa mbali na sigara, kaa mbali na tumbaku.

Kama ushazama tayari katika dimbwi hilo fanya mazoezi, jitenga na watu wanaovuta sigara, kuwa bize na shughuli za uzalishaji mali, tafuta starehe nyingine ya halali na isiyo na madhara, na ongea na washauri wakusadie namna ya kujitoa katika uraibu huo.

Kumbuka, ingawa kuacha uvutaji tumbaku ni jambo gumu, waswahili husema penye nia pana njia.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close