Junaynat Ally Dama
Historia imeandikwa. Kwa mara nyingine, Qur’an imejaza uwanja wa michezo nchini Tanzania katika mashindano ya Qur’an ya dunia, mara hii ikihusisha wanawake pekee.
Amina Yakhlef, mshiriki kutoka Algeria, ameibuka mshindi katika fainali za mashindano hayo yaliyofanyika katika uwanjwa wa Benjamin Mkapa unaobeba watu 60,000 ulioko wilaya ya Temeke katika mkoa maarufu kibiashara wa Dar es Salaam.
Washindi wengine katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini ni Nura Mohamed Ahmed kutoka Marekani, huku nafasi ya tatu ikienda kwa binti wa ki-Jordan, Sondos Saeed Saydawi.
Nafasi za nne na tano zilijazwa na washiriki wa Kitanzania, Aisha Abdallah Salum kutoka Zanzibar katika nafasi ya nne akifuatiwa na Sumaiya Shuaib Othman kutoka Tanzania Bara aliyeshika nafasi ya tano. Washindi hao wamepatiwa zawadi mbalimbali zikiwamo fedha pamoja na ufadhili wa safari za Umrah, kwa baadhi.
Ingawa mabinti hao watano ndio walitangazwa washindi, washiriki wote 11 walionesha umahiri wa hali ya juu katika hifdhi na kuchunga hukumu za usomaji, jambo lililopelekea kupitana kwa nukta chache, hivyo wote walikuwa washindi. Ukiacha nchi tano zilizotoa washindi nchi nyingine zilizoshiriki ni Saudi Arabia, Ujerumani, Urusi, Yemen, Sudan, Kuwait na Misri.
Ukiacha washindi watano na washiriki wengine saba, kufanikiwa kwa tukio hilo ni ushindi pia kwa wanawake wote wa Kiislamu, Tanzania nzima na duniani kote, kwa sababu jambo lao la kidini lilifanyika kwa ufasini, kwa uwezo wa Allah Mtukufu.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha nchi 11 yaliandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa ushirikiano na taasisi ya kimataifa ya Muslim World League (MWL) yakilenga kuwaenzi na kutambua mchango wa wanawake katika jamii.
Alikuwa ni raia namba moja wa Tanzania, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan aliyeongoza maelfu ya Watazamaji kuwaunga mkono mabinti hao shujaa 11 na baadae akawakabidhi zawadi na kuwapongeza.
Licha ya mashindano hayo, kulitolewa pia zawadi za kutambua mchango wa magwiji wa usomaji wa Qur’an ili kuenzi mchango wao walioutoa katika kuendeleza usomaji wa kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu. Watoto wa magwiji marehemu walikuwepo kupokea nishani hizo.
Aidha, Rais Samia naye alipewa tuzo ya heshima kutambuliwa kwa kazi yake kubwa anayoifanya ya kuhudumia jamii na kuinua ustawi wa taifa.
Vilevile, hadhara hiyo ilitumika kuzindua msahafu wa mtandaoni uliongizwa sauti za wasomaji zaidi ya 60 kutoka pande mbalimbali za duniani.
Salamu za Rais Samia
Rais Samia, akizungumza katika hadhara hiyo ya Qur’an iliyohudhuriwa na viongozi wote wa taasisi kubwa za Kiislamu, ikiwemo baadhi wa kimataifa na pia mabalozi, alisema taasisi za kidini zina wajibu wa kuandaa vijana katika misingi ya dini ili kuwa na maadili mema katika Taifa.
Kutokana na hilo, amezitaka taasisi hizo nchini, kubuni mbinu mpya zitakazowezesha kutoa elimu bora ya dini kwa vijana, wavulana na wasichana na kina mama ili jamii iendelee ibaki katika misingi ya maadili mema, amani, haki, upendo, mshikamano.
“Kumlea mtoto wa kike katika misingi ya kiimani unakuwa unaandaa mwanamke au mama atakayeishi katika misingi hiyo. Mtakubaliana na mimi kuwa watu wazima wenye kutenda haki ni zao imara la makuzi yao,” alisema.
Hata hivyo, alisema mkakati wa kulea mtoto wa kike uende sambamba na malezi mema kwa watoto kiume, kama ilivyoelekezwa katika dini.
Alisisitiza Waumini wa Kiislamu wasiishie kuisoma tu Qur’an bali waelewe maelekezo katika kitabu hicho kitukufu, akisema Qur’an ina majibu ya changamoto na kwamba njia zake zikifuatwa basi watu hawatapotea.
Akizungumzia mashindano hayo kufanyika Tanzania, Rais Samia alisema: “Mashindano haya kufanyika hapa kulitokana pia na Tanzania kuendelea kukubalika kimataifa kutokana na kuwa na amani na utulivu, Watanzania tuendelea kuilinda.”