Historia ya Sheikh Doga kwa ufupi
Yussuf Masoud
Kuweka kumbukumbu sawa kuhusu marehemu sheikh Doga, ijulikane kuwa jina lake kwa ukamilifu ni Muharam Juma Yussuf Mwingishaa Abdurahman Mtupa. Kwa jina maarufu alilozoeleka na wengi ni Doga.
Sheikh Doga alizaliwa mwaka 1948 katika Kijiji cha Usimbe wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani, akiwa ni mtoto wa kwanza katika familia yao ya watoto wa kike na kiume.
Makuzi ya kielimu Tanzania
Kama ilivyokuwa kawaida zamani, watoto wengi huanza kusoma elimu ya dini kupitia kwa wazazi wao au ndugu wa karibu.
Sheikh Doga, yeye alipata bahati ya kuzaliwa katika familia iliyokuwa na wasomi wengi wa dini. Kwa hiyo, alipata elimu yake ya awali ya dini kupitia kwa wajomba zake akiwamo Sheikh Bakari Amiri Shaha Mpendu, ambaye alikuwa ndugu wa mama yake. Baadaye Sheikh Doga alienda kusoma kwa Sheikh Omari bin Abdalla Yussuf Mtambo, aliyekuwa mume wa shangazi yake.
Mwaka 1967, akiwa na umri wa miaka 19 aliwaomba wazazi wake kuenda Dar es Salam kwa ajili ya kujiendeleza ambapo alipofika alijiunga na darsa za dini kwa Sheikh Uwesu Shaha Kaamil mtaa wa Uzuri, Temeke.
Kwa kuwa alipenda kusoma, siku zote hakutosheka na darsa moja, hivyo mwaka 1971 alijiunga na Markaz Islamic Chang’ombe hadi mwaka 1978 alipopata udhamini wa kwenda kusoma Madina.
Ikumbukwe alipokuwa akisoma jijini Dar es Salaam naye alikuwa akifundisha.
Maisha ya kielimu Saudi Arabia
Sheikh Doga alifanikiwa kupita kwenye usaili aliofanyiwa akiwa Madina na kuanza kusoma elimu yake mwaka wa tatu mutawaswitwa katika Chuo cha Maimuna kilichopo Madina. Kisha, alijiunga na elimu ya thanawii katika chuo cha Mubaraka na baada ya hapo akajiunga na Chuo Kikuu cha Sharia ya Kiislamu Madina na kufanikiwa kupata shahada yake katika fani ya Sharia ya Kiislamu.
Harakati za dini
Baada ya kurejea kutoka masomoni, Sheikh Doga alijiunga na Muslim Uniqal Islamia, kwa kufanya kazi ya da’awa Tanzania akiwa mwajiriwa wa taasisi hiyo. Kisha, alishiriki kuanzisha Markaz al Haramain al Islamiya kipindi hicho ikiwa Mnazi Mmoja stendi ya magari ya Tanga chini ya Mkurugenzi, Abasi Mustwafa Almaqbuul
Sheikh doga alisimamia harakati za da’awa nyakati tofauti na mikoa mbalimbali ikiwamo Pwani, Tanga Morogoro Iringa, Dar es Salaam na Zanzibar. Sehemu zote hizo alisimamia kutoa darsa ya tafsiri ya Qur’an kila mwezi wa Ramadhan. Pia alikuwa akitoa darsa mwezi wa Ramadhan na baada katika Msikiti wa Madina uliopo Kariakoo.
Sheikh doga alipata bahati ya kutafsiri vitabu vingi hapa nchini ambavyo wasomi wa dini wanafaidika vikiwemo Arrisalat Dimaat Twabiiyya fi Nnisai kilichoandikwa na Sheikh Uthaimin. Kitabu Al Luuluu wal Marjaan cha Sheikh Fuwad Abdul Baqi na vitabu vingine vingi. Pia, kwa kushirikiana na jopo la wanazuoni alishiriki katika kutafsiri Tafsiri ya Qur’an ya Ibn Kathir. Vilevile, alitafsri kitabu cha Alibayani fi tasfiri maani li Qur’an, kitabu ambacho kilipata mafanikio makubwa ikiwamo kupewa tuzo kutoka kwa Mufti wa Saudi Arabia Al-Malik Faisal
Mbali na kufundisha fani mbalimbali ikiwemo mirathi, lugha, Fiqhi, Nahau, Balaagh, Sheikh Doga alitoa darsa za dini na kurushwa Africa TV 2. Pia, huko nyuma aliwahi kuendesha kipindi cha fatwa (maswali na majibu) kikirushwa na iliyokuwa Redio Tanzania wakati huo chini ya mtangazaji Sheikh Salum Gereza. Kipindi hicho kiliwapa fursa wasikilizaji kuuliza maswali yanayowatatiza na kupata majibu yake kwa ufasaha na kwa mujibu wa sharia na muongozo wa dini ya Kiislamu.
Sheikh Doga bado yu hai katika nafsi za watu, kwa sababu ya elimu yake aliyoisoma na kuifundisha, ameifanya kazi kubwa ya kuandika vitabu na kuacha athari kubwa.