1. Habari1. TIF News

UAE, TIF zaleta faraja kwa watoto 50

Jumuiya ya Sharjah Charity International kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imefanikiwa kuwafanyia upasuaji wa moyo jumla ya watoto 50 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuokoa kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni 750.

Matibabu hayo yaliyoratibiwa hapa nchini na Taasisi ya The Islamic Foundation kwa kushirikiana na Ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE), yalitolewa bure kwa walengwa kwa msaada wa madaktari bingwa 12 pamoja na wasaidizi wao kutoka Hospitali ya Al–Qassimi iliyopo katika jiji la Sharjah katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Madaktari wageni waliohusika na matibabu hayo ni pamoja na Dkt. Ahmed Al Kamali kutoka UAE, Dkt. Suresh Kailasam Sivamurthy kutoka India, Dkt. Jameel Khan Thareen, Dkt. Ahmed Adel Hassan, Dkt. Mohamed Kasem, Dkt. Alhasan Abdullah Shaaban, Dkt. Saddam Mohammed Al Subuh, DktHamzeh Ghazi Algneady, Dkt. Adnan Ma Abu Ghazaleh, Dkt. Joseph Poulose, Dkt. Ali Mohamed Alrashdi na Dkt. Theodorus Vandekerhof.

Madaktari hao ambao pia walishirikiana na madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete waliweza kuwatibu moyo wagonjwa 35 kati ya 50 bila kufungua kifua kupitia teknolojia ya ‘Cardiac catheterization’ ambapo mgonjwa hutobolewa mishipa maalumu iliyopo mapajani na kuzibwa matundu ya moyo kupitia kifaa maalumu. Matibabu hayo ambayo yalitolewa bure na madaktari hao kutoka UAE yanafanya idadi ya watoto walionufaika na huduma ya upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya ya Kikwete kufikia zaidi ya 2,000 tangu huduma hiyo ilipoanza kutolewa nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2015.

Waziri Ummy ashukuru

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alizuru katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kushuhudia maendeleo ya zoezi hilo la matibabu ambapo alisifia na kuishukuru serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jumuiya ya Sharjah Charity International (SCI), The Islamic Foundation (TIF) na wataalamu wote waliofanikisha kazi hiyo. Waziri Ummy alisema juhudi zinazofanywa na JKCI za kutoa matibabu ya moyo zinachangia katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya utalii wa matibabu.

“Kupitia kambi mbalimbali za matibabu ya moyo, kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka 2018, tumeweza kuwafanyia upasuaji watoto zaidi ya 2000 kutoka ndani na nje ya Tanzania huku wengine wakisubiri matibabu,” alisema Waziri Ummy na kuongeza: “Zamani tulikuwa tunalazimika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kutibiwa lakini kutokana na uwezo wa madaktari wetu kuimarika, tumepunguza safari za wagonjwa nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 95.”

Waziri Ummy alisema moja kati ya faida kubwa ya kambi ya matibabu kama hayo ni wataalamu wa Tanzania kujifunza kutoka kwa wenzao. Aidha, alisifu juhudi zinazofanywa na madaktari kutoka Jumuiya ya Sharjah Charity International na JKCI akisema wanafanya kazi kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.

RC Makonda


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitoa wito kwa Watanznia kujitolea fedha kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya moyo kwa watoto. “Niendelee kutoa wito kwa kila mwenye nafasi achangie walau milioni mbili ili kuokoa maisha ya waoto wetu,” alisema Makonda. Akitotolea mfano wa juhudi anazozifanya, Makonda alisema yeye na Balozi wa UAE wamepanga kuwalipia bima ya afya watoto 500 wakiwamo wale wanaopatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.

“Mimi na Balozi tuna mpango wa kulipia bima za afya kwa watoto 500 wakiwamo yatima na wale wanaopatiwa matibabu moyo hapa JKCI. Mbali na hivyo pia tumewalipia ada wanafunzi 100 wa masomo ya sayansi ikiwa ni mkakati wa kuandaa madaktari wa baadaye,’” alisema Makonda.

Kauli ya Balozi wa UAE

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutamatisha zoezi la matibabu ya moyo kwa watoto 50, Balozi wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa nchini,Mheshimiwa Khalifa Almazrooq aliishukuru serikali kwa kuruhusu kuingizwa nchini vifaa tiba vya matibabu hayo bila ushuru.

Balozi Almazrooq alibainisha kuwa uhusiano wa Tanzania na UAE ni wa kindugu, na ndio maana wameweza kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto 50 wa kitanzania.

“Kufanikisha matibabu kama haya si kazi ya mtu mmoja au wawili, ni kazi ya watu wengi, huyu anawajibika na hili na mwingine anasaidia lile,” alidokeza Balozi huyo.

Aidha, Balozi huyo wa UAE alitoa shukrani zake za dhati kwa wote waliofanikisha shughuli hiyo ya matibabu akiwamo Aref Nahdi, Mwenyekiti wa TIF na Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi wa JKCI huku akiahidi kutoa misaada zaidi kwa serikali ya Tanzania.

Kauli ya wageni kutoka Sharjah

Naye kiongozi wa jopo la madaktari bingwa waliokuwa wanatoa huduma hiyo, Dkt. Ahmed Al Kamali amesema wanashukuru Mungu kwa kuwawezezesha kufika Tanzania kwa mara nyingine. Aidha, Al Kamali aliishukuru serikali ya Tanzania, ubalozi wa UAE pamoja na uongozi wa JKCI kwa kuwaruhusu kutoa huduma ya matibabu ya moyo kwa watoto.

“Tumekuwa tukiendesha kambi hizi za matibabu ya moyo katika nchi nyingi duniani ikiwamo Somalia, Yemen na Tanzania na tumepata mafanikio makubwa. Tunatumia fursa hii kuwatakia afya njema watoto wote wanaosibiwa na maradhi…, tutaendelea kushirikiana na taasisi ya The Islamic Foundation kwani wao ni washirika wakubwa katika kufanikisha shughuli hizi muhimu,” alisema Al Kamali.

Kauli ya Mwenyekiti, TIF

Akizungumza kwa niaba ya viongozi na wafanyakakazi wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aref Nahdi amesema wanamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa kiungo cha kuokoa maisha ya watoto.

Nahdi aliongeza: “Mwanadamu yeyote mwenye uwezo wa kujitolea asaidie gharama za matibabu kwani kutibu watoto ni sehemu ya mafanikio kwa sababu taifa lingeingia gharama kubwa kuwatibu wagonjwa hao lakini gharama hizo zimeokolewa kutokana na msaada wa wataalam uliotolewa bure.”

Hii ni mara ya tatu kwa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kuleta madaktari bingwa hapa nchini kwa ajili ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto. Tangu mwaka 2015 hadi mwaka huu wa 2019, TIF kwa kushirikiana na taasisi ya Sharjah Charity zimefanikiwa kuwafanyia upasuaji jumla ya watoto 65, kwa mujibu wa Profesa Janabi.

Katika hafla hiyo, taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) iliwatunuku tuzo za shukrani Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Balozi wa UAE, Khalifa Almazrooq kiongozi wa msafara Dkt. Ali Mohamed Alrashdi na kiongozi wa jopo la madaktari Dkt. Ahmed Al Kamali, Mkurugenzi wa JKCI, Mohammed Janabi na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close