1. Habari1. TIF News

TIF yaguswa na msiba Azam; yamkumbuka Said Haji

Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) imesema imeguswa na msiba ulioikumba Kampuni ya Azam Media ambayo ilifiwa na wafanyakazi wake watano katika ajali ya gari iliyotokea Shelui, Singida mwanzoni mwa wiki hii wakati wakielekea wilayani Chato, mkoani Geita kikazi.

Akizungumza na Gazeti hili, Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi alisema, taasisi yake inaipa pole kampuni ya Azam Media kwa kufiwa na wafanyakazi hao ambao walikuwa ni sehemu ya timu ya watendaji walioiletea mafanikio makubwa kampuni hiyo tangu kuanzishwa kwake.

Wafanyakazi waliofariki kwenye ajali hiyo ni Salim Mhando (muongozaji wa matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi ambapo wadau waliojitokeza kuwaaga katika ofisi za Azam Media waliwataja kama mashujaa. Mwenyekiti Nahdi alisema, msiba wa wafanyakazi hao umeigusa taasisi yake kwa sababu nyingi, ikiwemo ukweli kwamba taasisi ya TIF imekuwa na uhusiano mzuri na Azam Media, na pia imekuwa ikishirikiana nayo katika shughuli mbalimbali.

Said Haji aliliwa
Hata hivyo, licha ya kuguswa kwa ujumla, taasisi ya TIF kipekee imehuzunishwa kwa msiba wa mfanyakazi wake wa zamani, Said Haji, ambaye ni miongoni mwa waandishi hao watano waliofariki. Akimuelezea Said Haji, Mwenyekiti Nahdi alimsifia kama ni kijana mwema.

“Haji ni kijana muungwana aliyejifundisha kazi hapa TV Imaan na kupata uzoefu kabla ya kwenda Azam Media. Lakini hata baada ya kuondoka, hakusita kututembelea kindugu na kutupatia ushauri katika mambo mbalimbali.”

“Kitu alichokuwa nacho tofauti na wengine waliopita au kuacha kazi kwetu ni kuwa, Yeye aliendelea kuwa karibu na Tv Imaan na kuja kutupa ushauri kwa lengo la kutuboresha katika fani yake ya upigaji picha na mengineyo,” alisema Mwenyekiti Nahdi kwa njia ya simu.

Kauli ya Mwenyekiti Nahdi iliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha ambaye alisema Haji, licha ya kuondoka, aliendelea kuwashauri kuhusu namna ya kuboresha Imaan Media kwa sababu “alichukulia kufanya hivyo (kutushauri) kama ni wajibu wake wa kidini.”

Mkurugenzi huyo alimmwagia sifa Said Haji akimtaja kama mtendaji mzuri na mchapakazi ambaye alijituma na hakusubiri kutumwa. Sheikh Twaha pia alimtaja Haji kama kijana mstaarabu akitoa mfano namna alivyoondoka bila ugomvi.

Sheikh Ibrahim Twaha alisema: “Haji alipokuwa anataka kuhamia Azam alifuata taratibu za kikazi na aliaga kwa uzuri kwa wakuu wake. Sheikh Ibrahim Twaha pia alimtaja Said Haji kama kijana aliyejitahidi katika dini.

“Tangu kipindi niko naye hapa alikuwa anajibidiisha sana kusali. Kwahiyo
kwa upande wetu tumehuzunika na tunasikitika kwa masikitiko ya kidini. Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tunarejea, Allah tunamuomba amsamehe makosa yake, aipe subira familia yake, na ampe pepo na ajaalie tukutane naye Siku ya Kiyama peponi.”

Hata mtangazaji Ivona Kamuntu, naye alikiri kumjua Said Haji kama kijana mchamungu. Katika matangazo ya moja kwa moja ya kupokea miili ya maiti hao watano, Kamuntu alimuelezea Said Haji kama kijana mtulivu sana, na aliyeonekana kupenda dini.

Kassim Lyimo alivyomjua Haji
Naye mtangazaji wa TV Imaan, Kassim Lyimo, alisema alimjua Said Haji kabla hajaajiriwa Imaan Media. Alisema Said Haji alikuwa ni miongoni mwa timu ya watendaji wa kwanza waliyoajiriwa kuanzisha TV Imaan wakifanyakazi ya kurikodi vipindi mbali mbali. Lyimo alisema, walikuwa na Said Haji mpaka alipoajiriwa na Azam Media, lakini alikiri kuwa Haji aliendelea kuwatembelea na kuwashauri baadhi ya mambo kila alipopata nafasi kazini kwake.

Akizungumzia sifa za Said Haji, Lyimo alimtaja kuwa ni kijana aliyekuwa akifanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Lyimo alisema: “Msiba wake umetugusa sana Watendaji wa Imaan Media pamoja na viongozi wa TIF kwa ujumla.”

Kauli za wadau kwa Azam Media
Katika shughuli ya kuomboleza msiba huo iliyofanyika katika ofisi za Azam Media, wadau mbalimbali walitoa pole kwa familia na Azam Media, likiwemo Jukwaa la Wahariri, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Maliasili na Utalii, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) na wengineo wengi na vyama vya siasa.

Katika salamu zake za rambirambi Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Ayub Rioba alisema vijana waliofariki waliinufaisha TBC katika shughuli ambazo kampuni hizo mbili zilishirikiana kurusha pamoja, wakati Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole akiwataja kama mashujaa waliofariki wakiitumikia nchi kwani walikuwa njiani kwenda kurusha matangazo mbashara ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni alisema Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza ajali hiyo na tayari limemkamata dereva wa lori, huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Harrison Mwakyembe akikemea tabia ya kupiga picha marehemu inapotokea ajali.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close