1. TIF News

Ziara ya M’kiti TIF Nyanda za Juu Kusini yafungua fursa

Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi yenye makao yake makuu mjini Morogoro amefanya ziara ya siku tatu kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi hiyo katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe na pia kufungua fursa mpya za kuanzisha miradi mipya ya dini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Makongamano wa TIF, Tajmohamed Abbas, katika ziara hiyo iliyoanza Jumatatu ya Agosti 31, akiwa njiani Mwenyekiti alijionea baadhi ya miradi ya ujenzi wa misikiti inayotekelezwa na taasisi yake.

Aidha, Tajmohamed alisema, taasisi ya TIF pia ilikabidhiwa viwanja kadhaa vya Waqf kwa ajili ya kuviendeleza kwa kujenga misikiti na pia huduma nyingine za kijamii, kama vile shule, madrasa na visima vya maji.

Aidha, Tajmohammed alifafanua kuwa TIF imekabidhiwa kiwanja kimoja cha Waqf mkoani Iringa, viwanja vitatu mkoani Njombe na kiwanja kimoja mkoani Mbeya ambacho kilitolewa na Jamii ya Wabulushi wa Tanzania.

Ukiacha viwanja hivyo walivyokabidhiwa, TIF iliombwa isaidie kuendeleza viwanja vingine kadhaa vya Waqf ambavyo viko chini ya taasisi ya BAKWATA. Moja ya viwanja hivyo kipo mjini Makambaku (mkoa wa Njombe) na vitatu vipo mkoa wa Songwe.

Katika mpango wa muda mrefu, taasisi ya TF ina mpango wa kujena zaidi ya misikiti 40 katika mkoa wa songwe pekee. Katika ziara hiyo, Nahdi pia alikutana na viongozi mbalimbali wa Kiislamu wakiwemo baadhi ya masheikh wa mikoa na wilaya wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kubadilisha nao mawazo juu ya namna ya kushirikiana kuendeleza dini katika kanda hiyo.

Miongoni mwa masheikh aliokutana nao ni pamoja na Sheikh wa Mkoa Songwe Alhaj Hussein Batuza na Sheikh wa Wilaya ya Njombe, Shaban Dinga ambao katika mazungumzo nao walikubaliana maeneo kadhaa ya ushirikiano. Wakiwa Mbeya, Nahdi na ujumbe wake pia walikutana na kubadilishana mawazo na viongozi wa taasisi ya Dhinurain.

Akitia tathmini juu ya ziara hiyo, Tajmohamed alisema imekuwa ya mafanikio makubwa, hususan katika kuendeleza ushirikiano na mahusiano mema na taasisi nyingine za Kiislamu sambamba na kuondoa ikhtilaf zilizopo.

“Mwenyekiti alikuwa anatekeleza kauli mbiu yake ya ‘Tukubaliane kutokubaliana,’ lakini tushirikiane katika miradi yenye maslahi ya pamoja ya kuendeleza Uislamu hususan katika mikoa hii ambayo kuna uhitaji mkubwa wa misikiti,” Tajmohamed alisema.

Tajmohamed aliongeza kuwa, ziara hiyo pia iliwafungua macho juu ya uhitaji mkubwa wa miskiti katika maeneo mengi. Alisema kuna maeneo mengi kuna Waislamu lakini hawana misikiti. “Kwa kweli ziara hii imefungua fursa na milangi ya kuanzisha miradi mipya ya dini kuanzia Njombe hadi Songwe.”

Kauli ya Mwenyekiti

Akizungumza katika vituo mbalimbali alivyosimama katika safari yake, Mwenyekiti Nahdi pamoja na ujumbe wake walishukuru kwa mapokezi mazuri waliyapata katika kanda hiyo, huku pia akipongeza jitihada za Waislamu wa mikoa hiyo katika kuupeleka mbele Uislamu.

Nahdi pia alitoa wito kwa taasisi nyingine za dini ya Kiislamu kutembelea maeneo kama hayo kwani kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili Waislamu hasa waishio vijijini.

Nao wenyeji wa kanda hiyo waliipongeza viongozi wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kwa kuwatembelea na kuwapa moyo katika harakati zao za kujenga Uislamu. Miongoni mwa walioshukuru TIF na kutambua mchango wake wa kusaidia Waislamu na jamii kwa ujumla ni Sheikh wa Mkoa wa Songwe, Sheikh Hussein Batuza.

Sheikh Batuza alisema amefurahishwa kuona The Islamic Foundation imepokea maombi yao ya kusaidiwa kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi wa misikiti. Pia, Sheikh Batuza aliahidi kuwa Waislamu wa mkoa huo wapo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa TIF.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close