1. TIF News

Watendaji wa The Islamic Foundation Wapata Ajali Manyara…

Watendaji watatu wa taasisi ya The Islamic Foundation wapata ajali wakiwa katika majukumu yao ya kikazi katika kijiji cha Komolo wilaya ya Simajiro mkoani Manyara siku ya Jumapili tarehe 6/10/2019 wakiwa njiani kuelekea Arusha mjini.

Watendaji hao wametajwa kuwa ni Mkurugenzi wa Makongamano ndugu Tajmohamed Abbas, Naibu Mkurugenzi wa The Islamic Foundation mkoa wa Arusha Sheikh Ramadhani Mfinanga pamoja na Mfanyakazi wa vyombo vya habari vya Imaan Yusuf Mahmud Hujale.

Sababu ya Safari

Kama ilivyo ada ya taasisi ya The Islamic Foundation moja ya majukumu yake ni kuihudumia jamii kwa misaada ya kidini na kibinaadamu. Mnamo mwaka 2018 uongozi wa taasisi ya The Islamic Foundation ulipokea wageni kutoka taasisi ya iERA ya uingereza ambayo ilikuja nchini Tanzania kwa lengo la kufanya daawah maeneo mbalimbali nchini Tanzania, miongoni mwa maeneo waliyotembelea ni kijiji cha Sukuro kilichopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na kwa idhini ya Allah walisilimisha wanakijiji wa jamii ya kimasai takribani 80.

Hivyo basi, wanakijiji hao waliomba kupatiwa baadhi ya huduma za kibinadamu zilizokosekana kijijini hapo. Miongoni mwa huduma za msingi zilizokosekana kijijini hapo ni upatikanaji wa maji safi ambapo wanakijiji hao wanategemea maji ya mto ambayo wanatumia pamoja binadamu na wanyama, huduma za chumba cha kujifungulia wakina mama katika zahanati iliyopo kijijini hapo ambapo watu husafiri zaidi ya kilomita 100 kutafuta huduma hizo pamoja na huduma ya sehemu ya kufanyia ibada yaani msikiti.

Hivyo taasisi ya The Islamic Foundation ilitekeleza baadhi ya miradi ya huduma za kijamii katika eneo hilo ikishirikiana na wafadhili kutoka falme za kiarabu (UAE AID), ikiwemo kuchimba visima virefu vya maji safi, kujenga msikiti na kujenga chumba cha kujifungulia akina mama katika zahanati ya kijiji hicho.

Kwa kuanza na utekelezaji, The Islamic Foundation ilianza kwa kuchimba visima virefu viwili katika kijiji hicho, hivyo basi watendaji hao iliwabidi kwenda kukagua na kusimamia miradi hiyo na kuona utekelezaji wake.

Tukio la Ajali

Majira ya magaribi baada ya kukagua uchimbaji wa kisima cha kwanza katika kijiji cha Sukuro na kuridhishwa na maendeleo yake viongozi hao walianza safari ya kurejea Arusha mjini ili kuendelea na majukumu mengine ya taasisi.

Wakiwa katika gari inayomilikiwa na taasisi ya The Islamic Foundation yenye namba za usajili T293 AGW Land Cruiser Prado maeneo ya kijiji cha Komolo, kwenye sehemu yenye kona kali gari ilipoteza uwezo wa kurudisha usukani katika hali yake ya awali hivyo ikapelekea kupinduka zaidi ya mara 4 mpaka ilipokwenda kutua ikiwa imegeuka magurudumu yakiwa juu.

Baada ya Ajali

Baada ya tukio la ajali hiyo, wasamaria wema walifika eneo la tukio kuwanasua katika mkasa huo, na kuwachukua wahanga wawili wa ajali hiyo kuwawahisha hospitali ya Selian Arusha mjini huku mkurugenzi wa Makongamano akisubiri timu ya usaidizi ikiongozwa na Mkurugenzi wa The Islamic Foundation mkoa wa Arusha Sheikh Bader kuja kuendelea na taratibu nyingine za polisi.

Majeruhi wawili wa ajali hiyo waliruhusiwa usiku huohuo wa siku ya ajali kwa kuwa walikuwa wakiendelea vizuri huku wakiwa wamepata majeraha madogo madogo, michubuko pamoja na mistuko ya baadhi ya sehemu za mwili.

Mhanga mwingine wa ajali hii Sheikh Ramadhani Mfinanga ambaye ni naibu Mkurugenzi wa taasisi ya The Islamic Foundation mkoa wa Arusha bado angali hospitali akiendelea na matibabu.

Akizungumza na mwandishi wa makala hii hospitali hapo Sheikh Ramadhani alisema “Muumini anapopatwa na matatizo humshukuru Allah (Subhanahu Wata’ala) kwa Qadari zake kwani yeye ni mbora wa kukadiria, ni vyema kupata madhara ukiwa unatenda wema kuliko madhara yakupate ukiwa unatenda uovu”

Nae Mkurugenzi wa Makongamano wa taasisi ya The Islamic Foundation ndugu Tajmohamed Abbas aliwaasa ndugu jamaa na marafiki pamoja na wafanyakazi wote wa The Islamic Foundation kuwa wapole wakiwa na Subra kwani ni katika nyakati za maafa ndio shetani hutumia mwanya huo kucheza na akili zetu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation Sheikh Aref Nahdi atuma salamu za pole kwa Sheikh Ramadhani Mfinanga pamoja na familia yake na sasa yupo safarini kuelekea jijini Arusha kumjulia hali Naibu mkurugenzi huyo, na pia akaongeza kwa kutoa shukrani kwa kutoa shukrani kwa Mkurugenzi wa Arusha Sheikh Bader Nahdi na Mkurugenzi wa Redio Imaan Arusha Ali Akrabi kwa kuchukua hatua za haraka kusaidia majeruhi wa ajali hiyo.

Kilicho muhimu kwetu kwa sasa ni kuwa na subra na kumuomba Allah (Subhanahu Wata’ala) awaponye haraka majeruhi wote na kisha tufuate mafundisho ya dini yetu tukufu ya Kiislam ambayo inatufunza tukipatwa na Majanga, Misiba au Maafa tuamini na kusema Qaddara Llah Wamaa Shaa’a Fa’ala (Amekadiria Allah na anachokitaka ndicho hukifanya).

Tunachukua fursa hii kumomba Allah awape afwu majeruhi na afanye ajali hii kuwa ni sababu ya kukubaliwa mema yao na kufutiwa madhambi yao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close