1. TIF News

TIF yajenga msikiti, yaukabidhi BAKWATA

Kaimu Sheikh wa Bakwata, mkoa wa Morogoro, Twaha Kilango amewataka Waumini wa dini tukufu ya Kiislamu katika kata ya Kichangani, manispaa ya Morogoro kutumia misikiti katika kutekeleza mambo yaliyoelekezwa na dini hiyo.

Sheikh Kilango alitoa nasaha hizo wakati akizungumza na Waislamu wa eneo hilo mara baada ya kukabidhi msikiti uliopewa jina la Abubakr As–Swidiq kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) huku akitoa wito wa kuutunza vema msikiti huo na kuutumia kwa ajili ya ibada.

Ujenzi wa msikiti huo umefadhiliwa na taasisi ya Dar Al Ber Society ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Katika maelezo yake, Sheikh Kilango alisema ni wajibu kwa kila Muislamu kuhakisha anasimamisha sala zote katika msikiti huo sambamba na kuwaombea dua wafadhili wa msikiti huo.

Aidha, Kaimu Sheikh huyo wa mkoa amesifu juhudi zinazofanywa na The Islamic Foundation (TIF) katika kuihudumia jamii huku akiahidi kushirikiana na taasisi hiyo katika kusukuma mbele gurudumu la huduma na maendeleo ya Waislamu na jamii kwa ujumla.

“Taasisi za Kiislamu zinategemeana, hivyo ni vema wadau wa Uislamu wakaiunga mkono The Islamic Foundation katika jitihada za kuupeleka mbele Uislamu kwani juhudi zinazofanywa na taasisi hii zimeleta manufaa makubwa si tu kwa Waislamu bali jamii nzima,” alisema Sheikh Kilango.

Mbali na hayo, Kaimu Sheikh huyo wa mkoa aliwataka Waislamu kuutumia msikiti huo kueneza itikadi sahihi ya Kiislamu na kuepuka mambo yote yanayoweza kusababisha chuki, majungu na uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Aref Nahdi, Mwenyekiti wa The Islamic Foundation alisema taasisi hiyo imekuwa ikijenga misikiti ya kisasa na inayokidhi mahitaji ya Waumini.

“Pamoja na kufanya ibada, tumejenga msikiti huu ili mpate wepesi wakati wa misiba, tumejenga sehemu ya kuoshea maiti, msikiti wa Modeko pia tumejenga sehemu ya kuoshea maiti. Hivyo hakuna sababu tena ya kuosha maiti nyumbani,” aliongeza Nahdi na kuwataka Waislamu kuutumia msikiti huo kwa malengo kusudiwa.

Aidha, Nahdi aliwataka maimamu wa misikiti kuwafundisha Waumini wao namna ya kuosha maiti kwani mafundisho ya Sunna yanamtaka ndugu wa karibu wa marehemu amuoshe nduguye aliyekufa.

Kwa upande wake, Imamu wa msikiti huo wa Abubakar As–Swidiq, Muhsin Uso amewataka Waumini wa msikiti huo kuacha mazoea katika suala la utekekezaji wa ibada na majukumu mengine ya kidini na badala yake wafuate mafundisho ya Qur’ an na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close