1. TIF News

TIF waipa Al haramain kitega uchumi

Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi ameahidi kutoa bajaj kwa Markaz Al-haramain AlIslamiya, Kitengo cha Elimu ya Dini na Lugha ya Kiarabu kilichopo Ilala jijini Dar es Salaam.

Nahdi alitoa ahadi hiyo alipoalikwa kama mgeni rasmi katika mahafali ya 39 ya chuo hicho. Lengo la kutoa bajaj hiyo ni ili itumike kama mradi wa kuwawezesha kutatua baadhi ya changamoto za chuo hicho.

Awali, msoma risala Yassir Khalifa, aliomba chuo hicho kisaidiwe bajaj mbili na bodaboda mbili ili zitumike kama sehemu ya mradi huo, ndipo Mwenyekiti Nahdi aliyeguswa na kazi nzuri ya kituo hicho alipoahidi bajaj moja.

Katika nasaha zake kwa wahitimu wa chuo hicho, Nahdi aliwataka wahakikishe wanakuwa nembo ya Uislamu popote pale waendako. Aidha, Nahdi aliwataka wahitimu hao kuwa na maadili ili wawe mfano wa kuigwa katika jamii.

“Nendeni mkaibadili jamii, hakikisheni mnakuwa na maadili mema huko muendako na hakuna kitu kizuri kama kuwa na ukarimu,” alisema Nahdi na kuongeza: “Nyie mmepata bahati kubwa ya kusoma, sio kila mtu anapata bahati hii. Hivyo, hakikisheni mnaitumia vema elimu mliyoipata.”

Naye Amir wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu nchini (Hay-a), Sheikh Selemani Kilemile amewataka Waislamu nchini kuhakikisha wanausoma Uislamu na kuufundisha.

“Uislamu unahimiza suala la elimu. Tufahamu kuwa, umma wenye elimu ndio umma wenye thamani, kwa hiyo ndugu zangu Waislamu tuhakikishe tunasoma,” alisema Sheikh Kilemile.

Chuo cha Al-haramani ambacho kiko chini ya kituo cha Alharamain kilianzishwa mwaka 1976 na Sheikh Abasi Mustafa Maqbul kutoka nchini Saudi Arabia.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close