1. TIF News

TIF, Dar Al Ber zakabidhi msikiti Mikumi

Taasisi ya Dar Al Ber Society ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kushirikiana na The Islamic Foundation (TIF) ya hapa nchini zimekabidhi msikiti kwa Waislamu wa eneo la Mikumi Green wilayani Kilosa katika mkoa wa Morogoro.

Ujenzi wa msikiti huo uliopewa jina la Masjid Haqq, pamoja na sala nyingine, utatumika pia kuswalia swala ya Ijumaa.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya msikiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Sheikh Ibrahim Twaha alisifu ushirikiano wa muda mrefu baina ya TIF na Dar Al Ber Society, iliyodhamini ujenzi wa msikiti huo.

Sheikh Twaha alisema: “TIF kwa kushirikiana na Dar Al Ber inatekeleza miradi ya ujenzi wa misikiti, uchimbaji wa visima, elimu na huduma za afya kulingana na mahitaji ya Waislamu wa eneo husika na bila ubaguzi wa aina yoyote”.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa TIF alisisitiza kuwa, TIF inafanya kazi kwa karibu na wahisani mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ikiwemo taasisi ya Dar Al Ber na kwamba utekelezaji wa miradi hiyo unawafanya wahisani kuwa na moyo wa kuendelea kutoa misaada yao kupitia TIF.

Kwa upande wake, mlinganiaji wa Kiislamu, Sheikh Mikidadi Lipena aliwataka Waumini wa msikiti huo kuepuka kufanya biashara msikitini kwani kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za dini tukufu ya Kiislamu.

“Mnakabidhiwa msikiti huu ukiwa vizuri, hivyo itakuwa fedheha ikiwa msikiti huu utatumika kinyume na malengo ya msikiti…, tunakuombeni Waislamu wa hapa, mjue mmepata neema kubwa sana, basi utumieni vizuri,” alisema Sheikh Lipena.

Nao, Waumini na viongozi wa msikiti huo wa Haqq wamesema wameupokea vema msikiti huo na kuahidi kuutunza na kuepuka migogoro.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close