1. TIF News

Shule zetu zimepiga Hatua, Tuziunge Mkono

Hivi karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kupitia Katibu Mtendaji wake, Dkt. Charles Msonde lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika mwaka jana huku shule nyingi za Kiislamu zikiendelea kufanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka jana.

Miongoni mwa shule za Kiislamu zilizoonesha makali yake katika mtihani huo ni Jamhuri ya Dodoma na Thaqafa ya jijini Mwanza.

Shule nyingine iliyofanya vizuri zaidi katika mtihani huo ni Ilala Islamic ya jijini Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na NECTA imekuwa ya kwanza kiwilaya na ya tatu kimkoa ikiwa imetanguliwa na shule za Kanosa na shule ya Waturuki Feza. Pia, shule hiyo imekuwa ya 17 kitaifa.

Ilala Islamic imekuwa ikipata matokeo mazuri kwa ufaulu wa daraja la kwanza na la pili tu huku ikiepuka daraja la tatu, la nne na sifuri kwa miaka mitano mfululizo kwa kidato cha nne na kwa miaka mitatu mfululizo kwa kidato cha sita.

Katika matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa 26 wamepata daraja la kwanza huku sita wakipata daraja la pili na hivyo kuwa na uhakika wa kupeleka vyuo vikuu wanafunzi wote 32 waliohitimu shuleni hapo.

Katika orodha ya shule zilizofanya vizuri mwaka huu ipo pia Forest Hill inayomilikiwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF). Katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni, Forest Hill imefaulisha wanafunzi wote 25, ambapo tisa walipata daraja la kwanza, huku wengine saba na tisa wakipata daraja la pili na la tatu.

Kwa matokeo hayo, shule hiyo imeshikilia nafasi ya 82 kitaifa kati ya 190 kwenye kundi lake la shule zenye wanafunzi chini ya 30.

Hii ni hatua kubwa ya maendeleo ambayo tumekuwa tukiyatafuta kwa muda mrefu. Pamoja na kwamba shule hizo za Kiislamu zilizofanya vizuri ni chache, lakini zinatoa matumaini na kuonesha njia kwa shule nyingine za Kiislamu kufanya vizuri.

Itakumbukwa kwamba, kwa miaka kadhaa nyuma ilikuwa ni vigumu mno kusikia shule za Kiislamu zimefaulisha wanafunzi wengi kwa daraja la kwanza na la pili. Nyingi ya shule hizo za Kiislamu matokeo yake yalikuwa si ya kuridhisha na zilikuwa hazitoi matumaini na hamasa kwa wanafunzi kwenda kusoma huko. Kwa lugha nyingine shule hizo hazikuwa na mvuto.

Lakini katika miaka ya karibuni, shule zetu za Kiislamu zimepiga hatua. Hivyo, ni wajibu shule nyingine za Kiislamu zifuate njia hiyo ili kufikia malengo yao waliyoyatamani kwa muda mrefu.

Tunaamini mafanikio ya shule za Kiislamu yana mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kwa haraka zaidi. Pia, hakika, haina tija kundi moja la wananchi likawa na mafaniko ya kielimu na jingine likawa nyuma.

Hivyo, ni wajibu wetu kuendeleza juhudi zinazofanywa na shule za Kiislamu zilizofanya vizuri huku pia mikakati na malengo mbalimbali yawekwe ili shule nyingine za Kiislamu zifanye vizuri na kuzalisha wahitimu bora watakaokuwa watumishi bora watakaoiwezesha nchi kusonga mbele kimaendeleo.

Siyo siri kuwa Waislamu ni watu wanaosimamia haki na kadri wanavyokuwa wengi katika nafasi za utumishi serikalini ndivyo rushwa, ufisadi, upendeleo, wizi na maovu mengine yanavyozidi kupungua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close