1. TIF News

Prof. Kabudi aimwagia sifa UAE

Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa nchini, Mheshimiwa Khalifa Abdulrahman Mohamed Al Marzooqi amesema nchi yake itaendeleza ushirikiano baina yake na Tanzania kindugu, kidiplomasia, kiuchumi na kuhakikisha ushirikiano huo unadumu kwa faida ya nchi zote mbili.

Akizungumza katika maadhimisho ya 48 ya Umoja wa Falme za Kiarabu, yaliyofanyika kwenye Ubalozi wa UAE jijini Dar es Salaam, Balozi huyo alisema ushirikiano baina ya UAE na Tanzania utaimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali ikiwamo uchumi, afya, elimu na maji.

“Napenda kuwafahamisha kuwa UAE itaendelea kuwekeza hapa nchini Tanzania ikiwa ni ishara ya kukuza uchumi. Tutaendelea kuwaeleza wawekezaji fursa zilizopo Tanzania ili waendelee kuja kuwekeza,” alisema Balozi Al Marzooqi.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alimuahidi Balozi Al Marzooqi kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano wake na Umoja wa Falme za Kiarabu katika sekta za biashara, utalii, utamaduni, usafirishaji, kilimo, afya na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Profesa Kabudi aliongeza: “UAE imekuwa ikisaidia katika ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kusaidia juhudi za Tanzania kufikia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama vile ufadhili wa ujenzi wa barabara kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (ADFD).

Ni matumaini yangu kuwa mfuko utaendeleza usaidizi na kutelekeza miradi mingine ya maendeleo.” Profesa Kabudi alisema serikali imeanza maandalizi ya mkutano wa pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Falme za Kiarabu (UAE) utakaofanyika hapa nchini mwaka 2020.

“Tunatarajia kupanua wigo wa ushirikiano wetu katika mkutano ujao wa JPC. Kwa sasa tunafanya mashauriano ya ndani ili kuondoa tozo za ushuru mara mbili; pia tunafanya mapatano ya mkataba wa pamoja juu ya kukuza na kuendeleza ulinzi wa uwekezaji ambapo kwa makubaliano hayo, itapelekea Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwekeza Tanzania, alimalizia kusema Profesa Kabudi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close