1. TIF News
Trending

Mfumo wa fedha wa Kiislamu utakomboa maskini

Mwenyekiti Mtendaji wa Kituo cha Usimamizi, Ushauri na Masuala ya Kifedha ya Kiislamu (CIFCA), Aref Nahdi ameiomba serikali kumalizia mchakato wa kurekebisha sheria na kutunga kanuni za kuruhusu huduma za Kifedha za Kiislamu ili kuwakomboa maskini. Nahdi, aliwasilisha ombi hilo serikalini katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa kongamano la kuliombea taifa liwe na amani tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020.

Nahdi alisema, mfumo huo wa Kiislamu ukiruhusiwa utakuwa msaada mkubwa kwa makundi ya wanyonge wan chi hii, hususan wanawake ambapo watapata fursa ya kupata mikopo ya kufanyia biashara zao bila ya riba.

“Tunauhitaji sana huu mfumo wa Fedha wa Kiislamu sisi Watanzania wa hali ya chini kwa sababu ni mfumo ambao hauna riba. Tena kwa akina mama ni mzuri sana. Tukikupeni mikopo kuanzisha biashara hakuna riba,” alisema Nahdi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Nahdi, faida za mfumo wa fedha wa Kiislamu haziishii kwa wat utu bali zinaweza kufaidisha hata serikali.

“Hiki chombo cha CIFCA kinakwenda sambamba na kupata mashirika makubwa ya Kiislamu ambayo yanaweza kutoa msaada, ruzuku au mkopo kwa nchi yetu bila ya riba.”

Aref Nahdi – Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF)

Aidha, Mwenyekiti Nahdi ambaye pia Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) alisema mfumo wa Fedha wa Kiislamu unajumuisha pia bima maalumu ya Kiislamu iitwayo Takaful’. “Mfumo wa Fedha wa Kiislamu unakwenda sambamba na bima ya Kiislamu inayoitwa Takaful Insurance.”

Kasi ya Rais Katika hotuba yake, Aref Nahdi pia alisema mfumo wa fedha wa Kiislamu utasukuma kasi ya Rais John Magufuli ya kuwaletea maendeleo Watanzania. Nahdi alisema: “Rais anavyojitahidi kusukuma gurudumu la maendeleo unaweza kusema anakimbia kilomita 140 kwa saa. Lakini, tukiruhusu mfumo huu wa Kiislamu, nakuhakikishia kasi ya maendeleo itaongezeka.

Tunaweza kutoka katika kasi ya 140 kilomita kwa saa hadi kufikia kilomita 180 kwa saa,” alisema Nahdi.

“Mwenyekiti naomba utufikishie salamu zetu, tunahitajia sana mfumo huu hapa Tanzania. Tunachotakiwa kufanya ni kuukubali na kuutumia. Tutafanya vizuri katika maendeleo ya watu,” alisema Nahdi.

Nahdi ambaye alichaguliwa kuwa Mwenyekiti Mtendaji wa CIFCA, ni miongoni mwa waasisi wa taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009. Pia, ametajwa kuwa amekuwa akifanya juhudi kubwa katika kuandaa mikutano na kuwezesha upatikana wa washauri katika benki zinazofuata sheria za Kiislamu.

Maombi ya muda mrefu ya kutungwa kwa kanuni mahususi za kuendesha na kudhibiti utoaji huduma za kifedha za Kiislamu ni ya muda mrefu; na mara kwa mara, viongozi wa Kiislamu wamekuwa wakiyakumbushia. Mwaka jana (2019), mwanazuoni wa Kiislamu na Mjumbe wa Kituo cha Usimamizi na Ushauri wa Huduma za Fedha za Kiislamu nchini (CIFCA), Sheikh Muhammad Issa alizungumzia suala hili katika mahojiano ya simu na Gazeti Imaan. Sheikh Issa alisema, mabadiliko ya kisheria yatapelekea kutanuka kwa huduma hizo za fedha za Kiislamu hapa nchini na hivyo watu wengi kufaidika kwa kuepuka riba na miamala mingine ya haramu.

Gazeti la The Citizen la tarehe 23 Desemba, 2019 lilichapisha takwimu zinazoonesha kuwa sekta hiyo inakua lakini bado inatajwa kuwa kiwango cha huduma hizo ni kidogo ukilinganisha na ukubwa wa soko la huduma za fedha kwa ujumla hapa nchini. Kwa mujibu rekodi za mwaka jana zilizochpwa katika gazeti la The Citizen, hadi kufikia mwezi Septemba 2019, kiwango cha fedha zote zilizowekwa kwenye huduma za kibenki za Kiislamu kilikuwa ni asilimia 1.73 tu ya fedha zote katika mfumo wa fedha wa nchi. Vilevile, gazeti hilo linalotolewa kila siku kwa Kiingereza lilisema, kiwango cha mikopo iliyotolewa katika huduma za benki za Kiislamu kulinganisha na mikopo yote inayotolewa na mabenki nchini ni asilimia 1.44 tu.

Wanazuoni kama Sheikh Muhammad Issa wanaeleza kuwa sababu mbili kubwa za hali hiyo ni kukosekana kwa kanuni za kusimamia huduma hizo na pia uelewa mdogo wa watanzania kuhusu faida za mfumo huu. Akielezea namna kuchelewa kwa marekebisho ya sheria na kanuni zitakazotawala huduma za kifedha za Kiislamu kunavyoathiri ukuaji wa sekta hiyo, Sheikh Muhammad alisema kwa hali ilivyo sasa, kila mtoa huduma hiyo anafanya kivyake, kwa uelewa wake na matokeo yake wateja wanakosa huduma bora, kama ilivyo kwingineko duniani.

Alisema athari nyingine ya kuchelewa kwa kanuni hizo ni kukosekana kwa utaratibu mmoja wa usimamizi wa huduma za kifedha za Kiislamu hapa nchini. Kwa mujibu wa Sheikh Muhammad, katika nchi nyingine ambazo tayari zilitatangulia kutambua huduma hizi kama Kenya, Afrika ya Kusini na Uganda huundwa bodi ya usimamizi na ushauri wa huduma hizo chini ya benki kuu ili kuhakikisha kuwa huduma inayotolewa inakidhi viwango vya kimataifa. Alisema umuhimu wa uwepo wa chombo maalumu cha usimamizi wa huduma hizo ni kuhakikisha utatuzi wa migogoro unafanyika kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu, ambayo ndio msingi wa huduma hizo.

Aref Nahdi – Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF)

Sheikh Muhammad pia alisema kuchelewa kupatikana kwa sheria hiyo pia kunaathiri upande wa ukaguzi (Auditing) katika benki zinazotoa huduma hizo, ambapo kwa hali ilivyo sasa ukaguzi unafanyika kwa vigezo vya kawaida badala ya kutumika kwa vigezo vya huduma za Kiislamu.

“Kwa sasa, tunakosa kanuni na taratibu ambazo ni muhimu katika kuwezesha wawekezaji kuwa na jukwaa la kutegemewa la utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa misingi ya Kiislamu, jambo ambalo linawanyima wadau wa huduma za kifedha za Kiislamu ulinzi sawa wa kisheria kama ule wa unaotolewa kwa watumiaji wa huduma za kawaida,” alisema Sheikh Muhammad.

Hata hivyo, gazeti la The Citizen limesema mchakato wa marekebisho ya sheriai ya fedha na utungwaji kanuni za huduma hizo upo njiani, na kwamba Benki ya Tanzania (BoT) ilikuwa bado inakusanya maoni kutoka kwa wadau wa ndani na kimataifa ili waweze kutengeneza sheria na kanuni nzuri kwa huduma hizo kustawi.

Juhudi hizo za serikali za kutunga sheria na kanuni za uendeshaji wa huduma za kifedha za Kiislamu kumetajwa kutoa matumaini kwa wadau wa sekta hiyo, ambao wengi wamesema kutapelekea ufanisi zaidi wa huduma hizo na kuondoa migogoro. Hadi hivi sasa, Tanzania ina benki moja ambayo inatoa moja kwa moja huduma za kibenki za Kiislamu zinazokidhi matakwa ya sheria ya Kiislamu kwa ukamilifu. Lakini pia kuna benki tatu tofauti zimefungua dirisha la huduma za kibenki za Kiislamu.

Gazeti la The Citizen lilimnukuu Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Kifedha wa Benki Kuu, Mr. Nassor Omar kuwa benki ya Kiislamu iliyopewa leseni ni Amana Bank, huku benki ambazo zimepewa kibali cha kufungua dirisha la huduma za kifedha za Kiislamu kuwa ni KCB Bank-Tanzania, People’s Bank of Zanzibar na the National Bank of Commerce. Hata hivyo, licha ya uwepo wa huduma hizo, hakuna sheria maalum wala sera inayoelekeza na kudhibiti utoaji wa huduma hizo za kifedha za Kiislamu, isipokuwa upande wa bima ya Kiislamu (Takaful) ambayo kwa mujibu wa gazeti la The Citizen kanuni zake zilipitishwa mwaka jana.

Imeelezwa pia kuwa, BoT, kwa sasa inasimamia utoaji wa huduma za kibenki za Kiislamu kwa kutumia Sheria ya Taasisi za Kifedha na Mabenki ya mwaka 2006, ambayo haielezei kwa kuzitambua kiupekee huduma za kibenki za Kiislamu. Licha ya kuitwa kwa jina la huduma za kifedha na kibenki za Kiislamu, huduma hizo hazina ubaguzi na yoyote anaweza kufaidika nazo. Kwa mujibu wa wanazuoni, tofauti pekee na huduma za kawaida za kifedha ni kwamba, huduma hizi huendeshwa kwa misingi ya uchumi wa Kiislamu, ambayo inakataza riba.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close