1. TIF News

Kampeni ya kusaidia wahanga mafuriko Lindi yazinduliwa

Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye makao yake makuu mjini Morogoro imezindua kampeni ya uchangiaji fedha kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko wilayani Kilwa katika mkoa wa Lindi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TIF, Arif Nahdi, katika kampeni hiyo itakayoendeshwa kwa wiki moja, lengo ni kukusanya jumla ya shilingi milioni 100.

Akizungumza katika kipindi maalumu kilichorushwa mubashara kupitia Radio na Tv Imaan, Mwenyekiti Nahdi alisema jamii ina wajibu wa kuhakikisha waathirika wa mafuriko mkoani Lindi wanapatiwa mahitaji muhimu ya kibindamu kama vile dawa, nguo, vyakula na kadhalika.

TIF ambayo ina historia ya kuendesha kampeni hizi za kusaidia waathirika katika maeneo mbalimbali, ndani na nje ya nchi, imeamua kufanya hivyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli zake katika kuihudumia jamii ya Watanzania bila ubaguzi wa kimaeneo wala dini.

“Hili ni jukwaa (platform) tumewaletea hivyo tunawaombeni mlitumie vizuri,” alisema Nahdi. Kwa mujibu wa Nahdi, zoezi la uchangiaji wa fedha hizo lilianza Jumatatu iliyopita, Februali 3 na linatazamiwa kukamilika siku ya Jumapili, Februali 9, 2020.

Katika siku ya kwanza ya uzinduzi huo, jumla ya shilingi za Kitanzania milioni 14.7 zilichangwa na wadau mbalimbali huku misaada ya kibinadamu ikiwamo nguo na chakula ikiendelea kukusanywa.

Aidha, Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi alitoa wito kwa Watanzania, wa imani zote, kuendelea kuchangia fedha kupitia namba za simu za TIF ambazo ni M–Pesa, 0767 627284, Ezy Pesa 0778 627284, Tigo pesa, o738 016473; na pia kwa akaunti ya benki, namba ni KCB Bank, 3300554845.

Mbali na kuchangia fedha, pia Mwenyekiti huyo wa TIF, alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchangia pia wahitaji popote pale Tanzania bila kujali dini, kabila au sehemu misaada hiyo inapopelekwa.

Nahdi alisema: “Mafuriko yanaweza kumkuta yeyote. Hivyo basi, tunapaswa kuishi kwa upendo na undugu. Kwa vile wenzetu wamepata majanga, tuna wajibu wa kuwakimbilia na kuwapa pole. Hebu tufanye haraka tuwachangie ndugu zetu hao. Sisi kama taasisi tunaahidi kufikisha michango yote kwa walengwa.”

Athari ya mafuriko mkoani Lindi

Mafuriko yaliyotokea hivi karibuni mkoani Lindi yamewaacha maelfu ya wakazi wakiwa hawana mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na maji. Moja ya wilaya zilizoathirika zaidi ni wilaya ya Kilwa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, vijiji vilivyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo ni pamoja na Kilanjelanje, Nanjirinji A Ruatwe, Njinjo, Nakiu na Nanjirinji B.

Alisema mbali na nyumba kubomoka, mifugo na mazao wananchi hao nayo yamesombwa na maji, huku mashamba nayo yakiharibiwa. “Mafuriko yamesababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mfululizo,” alisema Ngubiagai.

Kutokana na mafuriko hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilwa amewataka watu wa kada mbalimbali kutoa msaada kwa wananchi hao. “Tunahitaji msaada wa chakula, dawa, nguo na vitu vingine muhimu,” alisema.

Historia ya kampeni za kusaidia waathirika za TIF

Huko nyuma, TIF pia imewahi kusaidia waathirika wa majanga mbalimbali ikiwemo wale wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambapo misaada yenye thamani ya shilingi 243 ilitolewa. TIF pia iliwahi kusaidia waathirika wa mafuriko katika kisiwa cha Panza huko Pemba na Kilosa mkoani Morogoro.

Vilevile, katika ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro mwaka jana, 2019, TIF ilitoa misaada ya kiutu ikiwamo dawa pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya kiasi cha shilingi za kitanzania zaidi ya milioni nane kwa wahanga wa ajali hiyo.

Hata kimataifa, TIF imewahi kuendesha kampeni ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasadia jamii ya Waislamu Warohingya ambao wamekuwa wakiteswa na Serikali inayodhibitiwa na Mabudha nchini mwao Myanmar na hivyo kulazimika kukimbilia uhamishoni Bangladesh.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close