1. TIF News

Forest Hill: Shule iliyodhamiria kuwa kinara Afrika Mashariki

Forest Hill ni moja ya shule kongwe za mkoani Morogoro ambayo kwa hivi sasa inamilikiwa na kuendeshwa na taasisi ya The Islamic Foundation (TIF). Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi lengo la taasisi yake ni kuifanya shule hiyo iliyopo mwanzoni mwa muinuko wa milima ya Kibwe kuwa miongoni mwa shule bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa kuelewa kuwa juhudi kubwa inahitajika ili kufikiwa malengo hayo, TIF inafanya uwekezaji mkubwa ili kuboresha kiwango cha taaluma shuleni hapo. Uwezekaji huo ulifanyika baada ya TIF kuainisha maeneo matatu ambayo yanahitaji maboresho ikiwemo nidhamu, miundombinu na taaluma kwa maana ya uwezeshwaji wa walimu.

Hakuna wengine wanaotegemewa kuyapa uhalisia maono ya Mwenyekiti Nahdi, yaani kuifanya shule hii kuwa bora zaidi Afrika ya Mashariki, bali ni timu ya walimu wa shule hii wakiongozwa na Mkuu wa shule Aboud Masoud na Makamu wake mwalimu mkongwe, Onaly Hassanal Dogo ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye aliyejiunga na Forest Hill tangu mwaka 1977.

Historia ya shule

Shule ya Forest Hill ilianzishwa mwaka 1966 na taasisi ya Morogoro Education Society. Alikuwa ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume ambaye aliizindua shule hii mwaka huo, kwa mujibu wa Mwalimu Onaly. Ikiwa ni moja ya shule chache za binafsi za wakati ule, Forest Hil ilikuwa inapokea wanafunzi wa aina zote, haibagui kwa misingi ya rangi, dini au hadhi ya mtu. Kwa ujumla ilikuwa ni shule ya watu.

Kundi la kwanza la wanafunzi wa kidato cha nne walihitimu Forest Hill mwaka 1969. Hawa walifanya mtihani wa ya Cambridge. Baadae, kuanzia mwaka 1971 shule iliingia kwenye mfumo wa mitihani ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ambao umeendelea hadi leo.

Kwa mujibu wa Mwalimu Onaly; mwanzo, shule ilianza na mikondo mitatu ya mpaka kidato cha nne, lakini kadri watu walivyofahamu umuhimu wa elimu na kadri shule ilivyofanya vema, wazazi wengi zaidi walitamani kuleta watoto wao kusoma hapa. Hivyo, shule ilitanuka, na bado wengine walikosa nafasi.

Kwa ujumla, miaka ya 1980, ikiwa chini ya Mwalimu Mohammed Ismail Patel, shule ya Forest Hill ilikuwa ni miongoni mwa shule kubwa mbili, nyingine ikiwa ni Kigurunyembe. Baadae ikaja shule ya Jabar Hirra iliyopunguza msongamano Forest Hill na Kigurunyembe, alifafanua Mwalimu wa Malezi, Mrisho Mbwembwe.

Baadae, kutokana na kuongezeka kwa uhitahi, Forest Hill ilianzisha kidato cha tano na sita mnamo mwaka 1987, shule ilianzisha elimu ya kidato cha tano na sita. Tulianza na michepuo miwili kisha tukaongeza miwili mingine na kuwa minne ambayo ni HGE, EGM, ECA na HGL.

Hali ya zamani na sasa

Shule ya Forest Hill ilipoanza miaka ya 1960 hadi 70 ilipata umaarufu mkubwa, kisha ikaja ikapungua umarufu wake kutokana na ushindani mkubwa iliyokuwa ikiupata kutoka shule mpya. Hata hivyo hivi sasa hii inatajwa kurejea katika makali yake ya awali, shukrani kwa juhudi za taasisi ya The Islamic Foundation (TIF).

Nilipotembelea Forest Hill hivi karibuni nilishuhudia ukarabati mkubwaunaoendelea upande wa majengo, na mazingira kwa ujumla ikiwemo viwanja vya michezo na njia zinazozunguka shule (pavements) ambazo zimejengwa vizuri kwa vitofali. Kwa tathmini ya Mwalimu Onaly, Forest Hill inaenda kuwa bora zaidi kuliko ilivyowahi kuwa miaka ya nyuma.

Huwezi kuzungumzia Forest Hill mpya iliyoboreshwa bila kuzungumzia taasisi ya The Islamic Foundation (TIF). Uhusiano wa taasisi hizi mbili unaanzia mbali, hususan mwaka 2010, pale Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi, alipokaribishwa kuwa mjumbe wa bodi ya shule. Ikumbukwa kuwa yeye, Nahdi, mwenyewe ni zao la shule hii kwa maana alisoma hapo. Haikupita muda Nahdi aliteuliwa kuwa meneja wa shule.

Zilipoanza shule za kata, wanafunzi katika shule ya Forest Hill walipungua sana kwani watoto wengi waliishia kupelekwa huko. Forest Hill ikayumba.

Shule ikakabidhiwa kwa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) ili iiendesha. Mwaka 2016, shule za Sekondari za Imaan na Forest ziliunganishwa na kuwa moja, ambapo wanafunzi wote wa sekondari ya Imaan walihamishiwa Forest Hill chini ya Mkuu wa Shule, Mohammed Patel aliyeiongoza shule hiyo kabla hawajaipokea timu ya iliyokuwa shule ya sekondari ya Imaan.

Tangu TIF iichukue Forest Hill kumekuwa na mabadiliko makubwa. Chini ya uongozi wa Mwenyekiti Aref Nahdi, TIF imewekeza katika maboresho ya miundo mbinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa maabara mpya ya fizikia. Vilevile, uwanja wa michezo uliwekwa taa ili kuwezesha michezo kufanyika hadi usiku.

Hayo siyo maboresho pekee. Miradi mingine ambayo inatekelezwa kwa upande wa maboresho ya miundombinu ni pamoja na ukarabati mkubwa wa majengo ambayo yalikuwa yameshaanza kuchakaa, ujenzi wa ukumbi mkubwa na wa kisasa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua hadi watu 200 na mabweni ya wanafunzi.

Ama kuhusu mipango ya baadae, katika miaka michache ijayo, TIF itajenga jengo la kisasa la ICT litakalokuwa na miundombinu yote ikiwemo kompyuta za kutosha, ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira yanayoendana na karne ya 21. Pia upo mpango wa kujenga nyumba za walimu ndani ya eneo la shule ili kurahisisha usimamizi na nidhamu ya wanafunzi.

Kwa kuwa mabweni ya wanafunzi kwa sasa yapo nje ya eneo la shule, mpango mwingine hapo mbeleni ni kujenga mabweni ya kisasa ndani ya eneo la shule. Suala la usalama pia litazingatiwa ambapo miundombinu ya kisasa ikiwemo teknolojia ya alama za kibaolojia (biometric technology) na kamera za ulinzi (CCTV) vitawekwa.

Eneo jingine ambalo taasisi imewekeza sana maboresho ya taaluma kwa walimu kupitia mafunzo na semina mbalimbali. Pia uamuzi wa makusudi ulifanyika kuanzisha michepuo ya sayansi kwa kidato cha tano na sita ikiwemo PCB, PCM na CBG. Pia, hali ya hali ya juu imerejeshwa shuleni ili kuhakikisha kukua kwa taaluma kunaenda uzingatiwaji wa maadili.

Baada ya shule hizo mbili kuunganishwa, mabadiliko mengine kadhaa yaliyanyika ikiwemo ya sare. Kwa mujibu wa Mwalimu wa Malezi Mrisho Mbwembwe.

“Unajua wakati tunakuja hapa Forest Hill, wenyewe walikuwa wanavaa kaptura na wanawake wanavaa sketi. Lakini sasa wanafunzi wanavaa suruali na wanawake wanavaa magauni ya kutosha kujistiri kwa mujibu wa kanuni za mavazi ya Kiislamu . Mabadiliko haya yalinifurahisha sana,” alisema Mwalimu Mbwembwe.

Mwalimu Mbwembwe alifafanua kuwa, wanafunzi wasio wa Kiislamu walitakwa kuvaa mavazi hayo, ingawa hawalazimishwi kufanya ibada wasio na ujuzi nayo. Alisema hilo ni jambo jema kwani wanafunzi wa Kiislamu wanapata uhuru wa kuendelea kusoma bila kubughudhiwa.

Mwalimu Mbwembwe aliliambia gazeti hili kuwa watu wanaizungumza vizuri sana shule ya Forest Hill, wakiwemo viongozi wa serikali. Alisema, miongoni mwa watu waliokoshwa na maendeleo ya shule ya Forest Hill ni maafisa elimu wa mkoa na hata wilaya ambao kila walipotemnbelea walishangazwa na maboresho mbalimbali yanayofanyika.

Hitimisho

Kama alivyosema Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi, malengo ya taasisi yake ni kuifanya Forest Hill kuwa miongoni mwa shule 10 bora za Afrika Mashariki. Ili kufikia azma hiyo, ushirikiano wa wadau wote – wamiliki, bodi ya shule, walimu, wazazi na wanafunzi ni muhimu sana. Iwapo kila mdau atatekeleza wajibu, inshaAllah, Forest Hill itarejea katika ubora wake wa miaka ya 1970 na 80.

Wito kwa wazazi ni waendelee kuiamini shule ya Forest Hill kwani wamiliki, The Islamic Foundation (TIF), wapo makini na katika kuhakikisha wanafunzi wanapata taaluma nzuri na malezi bora ya Kiislamu ili hapo baadae wawe raia wema ambao taifa litawategemea.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close