1. TIF News

Bima ya Takaful yazinduliwa, kuanza Mei

Hatimaye miongozo ya bima inayofuata misingi ya Kiislamu (TAKAFUL) iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wananchi wengi husuusan Waislamu imezinduliwa wiki hii huku Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Bima Nchini (TIRA) ikitangaza kuwa Mei 1 mwaka huu ndio utakuwa mwanzo wa kutumika miongozo hiyo.

Akiongea katika hafla ya kuzindua miongozo hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwl. J.K Nyerere uliopo Posta jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Mamlaka ya Bima nchini , Dkt Baghayo Abdallah Saqware amesema makampuni yanayotaka kufanya biashara hiyo yanaweza kupeleka maombi TIRA kuanzia mwezi Mei 1, 2022 ili waweze kusajiliwa tayari kwa kufanya biashara.

“Muongozo huu utaanza kutumika Mei 1, 2022. Maana yake ni kwamba ikifika tarehe hiyo Makampuni yanayotaka kufanya biashara ya Takaful yanaweza kuleta maombi yaweze kusajiliwa na kuanzisha biashara. Bima ya Takaful inafuata misingi ya kisharia (Shari’ah compliance),” alisema Dkt Saqware

Aidha, Dkt Saqware alisema miongozo hiyo itasaidia kuwezesha wawekezaji wanahitaji huduma za bima zinazofuata misingi ya dini ya Kiislamu kuwekeza katika biashara ya bima na pia kunafungua milango kwa wananchi kuanza kupata huduma za bima kwa mujibu wa huduma hizo za bima ya Takaful

“Ni mategemeo yetu kuwa sasa wananchi ambao wanahitaji huduma kutoka kwa taasisi za namna hiyo wataanza kujiunga ili kupata kinga na kuingia kwenye mfumo rasmi wa kifedha hapa nchini,” aliongeza Dkt Saqware.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kituo cha Usimamizi wa Masuala ya Huduma za Kifedha za Kiislamu na Ushauri Tanzania (CIFCA), Aref Nahdi, alisema kuzinduliwa kwa miongozo hiyo ni hatua kubwa japo bado hawajafika katika hatua wanayoitaka.

“Naomba kutoa angalizo kwa Mamlaka ya Bima na wale watakaotoa huduma hizi. Isije miongozi hii ikabakia katika makabrasha tu lakini utekelezaji wake usiweko. Huduma hizi zina mambo mawili tu, ima kutupeleka motoni au poponi”, alisema Mwenyekiti Nahdi.

Aidha, Mwenyekiti huyo alisema taasisi yake iko tayari kufanya kazi na taasisi za serikali na wadau wowote wanaotaka ushauri wa huduma za kifedha za Kiislamu nchini kwani wanao wataalam wa kutosha kutoa elimu hiyo.

Naye Mratibu wa CIFCA, Sheikh Muhammad Issa alisema biashara ya TAKAFUL ni kwa faida ya Watanzania wote, na ni matumaini yake kuwa mifuko itatuna zaidi kama watu wataifanya biashara hiyo ipasavyo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Zoezi la Uandaaji wa Miongozo ya Bima 2022, Mkurugenzi wa TIRA Muyengi Zakaria, amewapongeza CIFCA kwa ushirikiano walioutoa hadi kukamilika kwa muongozo wa TAKAFUL.

Zakaria alisema kwa kiasi kikubwa CIFCA walitoa maelekezo muhimu yaliyochangia kutengenezwa kwa muongozo huo ambayo unatarajiwa kuleta tija katika taifa.

“Baada ya uzinduzi huu tutaanza kutoa mafunzo mbalimbali kwenye mongozo wa Takaful tukishirikiana na CIFCA. Kimsingi, wawezeshaji wetu watakuwa CIFCA. Mafunzo yataanza na wasimamizi wa sheria (regulator) na baadae tutawaendelea wadau wengine,” alisema Zakaria.

Wadau mbalimbali walioudhuria hafla hiyo wamesema wanaamini wawekezaji wataongezeka hasa kutoka katika nchi za Kiislamu na kwamba hatua hiyo inaenda kutanua wigo wa utoaji bima kwa makundi yote.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati], Kheri Mahimbali alisema Tanzania ilikuwa inakosa wawekezaji hasa kutoka nchi hizo kutokana na kutokuweko kwa huduma za bima ya Takaful nchini.

“Mimi ni mdau mkubwa wa Takaful. Sisi kama wizara kwa muda mrefu tumekuwa tukikosa majawabu tunapoulizwa na wawekezaji kutoka nchi za Mashariki ya Kati iwapo hapa nchini kuna huduma za takaful. Ndiyo maana leo pamoja na majukumu mazito tuliyokuwa nayo, nimeona nifike kushuhudia hatua hii muhimu”, asliema Mahimbali.

Inaelezwa kuwa mchakato wa takafuli ulianza toka mwaka 2014 huku CIFCA wakiwa na mchango mkubwa katika kushawishi, kuelimisha na kueleza faida za biashara ya bima ya Takaful.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close