1. TIF News

Aref Nahdi atuzwa kwa kuendeleza Qur’an Tanzania

Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tanzania imempa tuzo maalum Mwenyekiti wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Aref Nahdi, kutambua mchango wake na taasisi yake katika kuendeleza jitihada za kuhifadhisha Qur’an tukufu hapa nchini.

Makamu wa Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt Mohammed Gharib Bilal alimkabidhi Nahdi tuzo hiyo katika mashindano ya kimataifa ya Qur’an yaliyofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Tuzo hiyo inatolewa na taasisi hiyo ya kuhifadhisha Qur’an ikiwa ni miaka 30 tangu ianzishwe na kuanza shughuli za kuhifadhisha na kuendesha mashindano, ambapo Nahdi anatajwa katika walioshiriki kuunga mkono juhudi sio tu za taasisi hiyo bali hata jitihada za wadau wengine pia.

Tukio hilo la kukabidhiwa tuzo lilishuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ally Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo.

Viongozi wengine waliokuwepo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi. Tukio hilo pia lilirushwa moja kwa moja na vyombo vya Habari vya Imaan ambavyo vinamilikiwa na taasisi ya The Islamic Foundation inayoongozwa na Nahdi. Tukio hilo pia lilionekana moja kwa moja katika vyombo kadhaa vingine vikiwemo ZBC2, Kishk TV, Channel Ten, Clouds na mitandao ya kijamii.

Mafanikio ya Nahdi

Mwenyekiti Nahdi amefanya mengi kustahili tuzo hiyo yenye hadhi yake iliyotolewa katika jukwaa la kimataifa la Qur’an.

Licha ya mchango wake wa moja kwa moja katika mashindano mbalimbali ya Qur’an, Nahdi amefanikiwa kujenga msingi mzuri wa uendeleaji Qur’an nchini kupitia miradi mbalimbali inayoendeshwa na taasisi yake.

Tukitaja miradi michache, Nahdi kupitia taasisi yake ya The Islamic Foundation, amejenga misikiti zaidi ya 1300 ambayo ndani yake kuna madrasa za kufundisha Qur’an. Misikiti hiyo imeenea nchi nzima sio bara tu bali hata visiwani.

TIF sio tu imejenga misikiti hiyo bali pia inasimamia uendeshwaji waje ikiwemo kulipa watendaji, hususan maimamu. Sasa hivi, TIF inajenga inshaAllah utakaokuwa msikiti mkubwa zaidi mkoani Morogoro ambao pia bila shaka utakuwa kituo muhimu cha kuendeleza Qur’an.

Kupitia taasisi anayoingoza ya The Islamic Foundation, Nahdi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Ushauri wa Masuala ya Fedha ya Kiislamu hapa nchini (CIFCA), amefanikiwa kujenga shule takriban 7 za Kiislamu ambazo ukiacha masomo ya kidunia, pia zinafundisha Qur’an Tukufu.

TIF pia ina vyuo vya dini, Mahad Imaan tisa katika maeneo mbalimbali nchini ambapo viongozi wa baadae wa Kiislamu, hasa katika ngazi za misikiti na walimu wa madrasa wanaandaliwa.

Lakini mchango mkubwa na ulio wazi zaidi wa Nahdi katika kuendeleza Qur’an ni kupitia vyombo vyake vya habari vya Imaan Media ambavyo vinafundisha umma moja kwa moja Qur’an sio tu kuisoma bali pia maana yake.

Imaan Media, kwa miaka mingi, pia imekuwa ikionesha mashindano ya Qur’an moja kwa moja na hivyo kuunga mkono kuenea kwa sio tu elimu bali pia hamasa ya Qur’an.

Mwaka huu, katika tukio linaloonesha mapenzi yake kwa Qur’an, Mwenyekiti Nahdi alitoa ofa kwa mshindi wa jumla (juzuu 30) wa mashindano ya Qur’an ya Umoja wa Shule za Msingi za Kiislamu (TIPSO), kwenda Umra, yeye na mzazi wake.

Huyo ndio Arif Nahdi, kwa ufupi sana. Hakika mapenzi yake kwa Qur’an hayajifichi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close