2. Taifa

Wazazi waambiwa, elimu ndio bima bora kwa Watoto

Wazazi na walezi wa Kiislamu nchini wametakiwa kuwekeza katika elimu ya watoto kwa kuwa kufanya hivyo ndiyo bima bora kwa maisha yao ya duniani na kesho akhera. Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), Sheikh Ibrahim Twaha kwenye mahafali ya 19 ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Imaan English medium iliyopo mjini Morogoro.

Sheikh Twaha alisema wakati umefika kwa wazazi kuwekeza kwenye elimu ya watoto ili Tanzania iweze watoto hao wawe raia bora watakaotoa mchango katika maendeleoya nchi na sambamba na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.

“Elimu ndiyo msingi wa kila kitu kama alivyosema Mwenyezi Mungu ndani ya Qur’ an, kuwa Yeye Allah ndiye aliyemfundisha (binadamu elimu zote kwa msaada) wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo ambayo alikuwa hayajui. Kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza kwenye sekta ya elimu,”alifafanua Sheikh Twaha.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi, aliwahimiza wazazi kutimiza wajibu wao katika malezi ya Watoto kwa kuwapeleka katika shule zenye maadili bora ya Kiislamu.

Amanzi alisema, ili kuendana na matakwa ya sera ya nchi, wazazi wanapaswa kutimiza kikamilifu wajibu wa kutoa malezi bora kwa watoto wao na kuongeza:

“Tuhakikishe tunawalea watoto katika misingi ya dini ili watambue namna bora ya kumtii Mwenyezi Mungu na kumuabudu Mwenyezi.”

Katika mahafali hayo ya darasa la saba ambayo pia yalikwenda sambamba na mahafali ya 14 ya wanafunzi wa awali (chekechea), jumla ya wanafunzi 61 wa darasa la saba na 51 wa chekechea walihitimu masomo yao na kukabidhiwa vyeti. Shule ya Imaan English Medium ambayo inamilikiwa na Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye makao yake makuu mkoani Morogoro imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba ambapo kwa mwaka jana wa 2018 iliweza kufaulisha wanafunzi wote.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close