2. Taifa

Wanaotaka uongozi misikitini wajipime

Aliyewahi kuwa Imam Mkuu wa msikiti wa Ijumaa wa Mwanza, Sheikh Jabir Katura amewataka Waislamu wanaotamani kushika vyeo misikitini kujitathmini kama wana sifa zinazotakiwa za ukweli na uaminifu.

Sheikh Katura alisema, ukweli na uaminifu ni sifa za kiigizo chetu, Mtume Muhammad mwenyewe (rehema za Allah na amani zimshukie); na kwamba, kwa sababu ya sifa hizo Mtume aliweza kuaminiwa na wengi na hakuwahi kushutumiwa kwa wizi au namna yoyote nyingine ya hiyana.

“Wale wanaotaka kushika madaraka misikitini wafahamu kuwa wanakwenda kuifanya kazi ya Allah, (hivyo) wanapaswa kujipima kama wanasifa ya ukweli na uaminifu,” alisema Sheikh Katura katika mahojiano maalumu na gazeti la Imaan baada ya kuulizwa nini kifanyike ili kukomesha migogoro misikitini na badala yake taasisi hizi ziwe kitovu cha maendeleo ya Waislamu.

Akifafanua zaidi, Sheikh Katura alisema, kiongozi wa dini anapaswa kuwa mtu wa kuiangalia akhera zaidi kwani anakwenda kubeba matatizo makubwa ambayo anategemewa kuyatatua. Alisema, kamwe uongozi wa dini sio sehemu ya kukimbilia, akitoa mifano mbalimbali ya hofu ya kubeba majukumu ya uongozi waliyokuwa nayo wema waliotangulia.

Moja ya mifano ambayo Sheikkh Katura aliitoa ni ule wa Swahaba mkubwa wa Mtume na Khalifa wa pili, Umar bin Khattwab (Allah amridhie) ambaye aliposhauriwa na watu wake wa karibu kumuandaa mtoto wake Ibn Umar kushika nafasi yake, alikataa wazo hilo kwa hoja kwamba, asingependa kuona mtoto wake anakumbana na shida anayokumbana nayo yeye katika nafasi hiyo .

“Sayyidna Umar alipenda kijana wake abaki alivyo (akijua kuwa) uongozi ni dhima nzito… uongozi ni wajibu na siyo sehemu ya kula,” alisisitiza Sheikh Katura na kushauri jitihada kubwa ifanyike katika kuwaandaa viongozi kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu.

Sheikh Katura pia alikemea migawanyiko ndani ya jamii ya Waislamu. Sheikh alisema: “Haifai hata kidogo Waislamu kubaki wamegawanyika na wanagombana. Kunapaswa kuwa na nidhamu katika misikiti. Kila kiongozi anapaswa kuhakikisha anaweka nidhamu katika msikiti anaoungoza.”

Awali akijibu swali kuhusu changamoto anazoziona kuwa zinakabili uendeshaji wa misikiti, Sheikh Katura alitaja mipango mibaya ya uendeshaji misikiti kiuchumi kuwa ndio tatizo kubwa la misikiti. Changamoto nyingine alizozitaja ni viongozi kukosa ‘Ikhlas’ (nia safi) jambo linalopelekea kuzalikana kwa migogoro isiyo na tija na baadhi yao kuwa na ubinafsi.

Alisema Sheikh Katura: “Ukigusa masuala ya fedha (misikitini) utaonekana ni mbaya. Hiyo ni changamoto kubwa… Bado kuna ombwe la udhibiti wa rasilimali za misikiti hali inayopelekea kushindwa kutimiza baadhi ya majukumu. …Zakatul maal zinakusanywa lakini hakuna usimamizi mzuri wa fedha hizo kuwafikia walengwa wakiwemo mafukara, masikini, na wenye uhitaji.”

Kutokana na changamoto hizo, Sheikh Katura alishauri kuwe na uwazi katika usimamizi wa mapato ya misikiti na pia makusanyo yanayofanywa misikitini ili yafanye kazi ya Allah ikiwemo kujiletea maendeleo na kuwasaidia mayatima na masikini.

Nasononeshwa na migogoro

Sheikh Katura alisema katika mambo yanayomsononesha sana ni migogoro misikitini. Sheikh Katura alisema wakati wa uongozi wake alijitahidi kufanya yaliyo ndani ya uwezo wake, lakini sasa anasononeshwa na mifarakano ambayo inashamiri kila kukicha katika taasisi za Kiislamu.

Sheikh Katura alisema: “Taasisi mbalimbali zinagombana kila kukicha na hakuna wa kuwapatanisha, kibaya zaidi kwa mfano sisi watu wa sunna tunapogombana huwa ndiyo basi tena huwa hatuwezi kupatana.

Kwa nini tugombane? Na kwa nini tusipatane? Mbona wengine wanagombana na wanapatana? Kwa nini sisi!? “(Kuwa mtu wa) Sunna sio mavazi… vilemba. Kuwa mtu wa Sunna ni kufuata mwenendo wa Mtume, ikijumuisha tabia, huruma na upendo, yaani ni akhlaq (tabia) na vitendo vyake. Mtume anasema, ‘Nimetumwa kuja kukamilisha tabia njema.’ Maana yake tabia zilikuwepo, lakini Yeye amekuja duniani kuikamilisha tabia njema.

Dini si ukali. Dini si mavazi. Dini siyo ugaidi… yaani sio mtu akivaa kilemba na mwingine ukamuona hajafanya hivyo basi ndio unataka kumkanyaga, dini haitaki hivyo.”

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close