2. Taifa

Waislamu watakiwa kuchangia zaidi vyombo vya habari vya Kiislamu

Waislamu wametakiwa kuendelea kuchangia zaidi vyombo vya habari vya Kiislamu ili viweze kupata nguvu zaidi ya kuendeleza kazi ya da’awa nchini na kimataifa.

Wito huo umetolewa na viongozi mbalimbali wa Kiislamu waliohudhuria na kuwasilisha mada katika kongamano maalumu jijini Arusha, lililoandaliwa na Kituo cha Televisheni cha Mahaasin (Mahaasin Tv) cha jijini Mwanza kwa ajili ya kununua vifaa vya kuboresha matangazo ya kituo hicho.

Katika kongamano hilo, kiasi halisi cha fedha kilichokusanywa hakikufahamika mpaka gazeti linaingia mitamboni kuchapwa, lakini kwa mujibu wa Imam wa Msikiti wa Ijumaa Mwanza na mdau mkubwa wa Mahaasin Tv, Sheikh Hamza Mansur, lengo halijafikiwa.

Sheikh Mansur alisema moja kati ya mambo yaliyofanya lengo lisifikiwe ni mvua iliyonyesha na hivyo kupelekea watu wengi kushindwa kufika uwanjani. Kwa mujibu wa Sheikh Mansur lengo lao ilikuwa ni kukusanya kati ya shilingi milioni 300 hadi 400.

Tamasha la kuchangia fedha hizo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, ambapo pia wito umetolewa kwa Waislamu kutumia vyombo vyao vya habari kuhamasisha amani kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo.

Katika tamasha hilo ambalo lilirushwa mubashara kupitia vyombo vingine vya Kiislamu ikiwemo Tv Imaan, Mahaasin Tv, Africa Tv 2 na ZBC 2, Waziri wa Maliasili na Utaliii, Dkt. Hamisi Kigwangala alichangia shilingi Milioni 1.5 na kuahidi kutoa kiasi kingine cha fedha shilingi Milioni 3.5 siku za usoni.

Hata hivyo, mmoja wa waratibu wa kongamano hilo, Sheikh Hassan Muhammad, maarufu kwa jina la Muhammadain alisema, huenda ikichanganywa ahadi na pesa taslimu, kiasi kilichopatikana kinaweza kukaribia milioni 100, lakini bado hazitoshi.

“Tunaamini kiasi hiki kitasadia kuimarisha urushaji matangazo na kukata kiu ya watazamaji hasa hasa Waislamu,” alisema Sheikh Muhammadain na kuongeza: “Tunaomba Waislamu wazidi kuchangia.”

Sheikh Muhammadain aliongeza kuwa fedha zilizochangwa mpaka sasa zimetokana na Waislamu kuguswa na changamoto zinazovikabili vyombo vya habari vya Kiislamu.

“Vyombo vyetu vinatumia pesa nyingi sana. Kuna satelaiti, kuna mitambo – vyote hivi vinahitaji pesa ili viimarike. Hivyo basi, tunawaomba Waislamu wenzetu wazidi kutuchangia,” alisema Sheikh Muhammadain.

Sheikh Muhammadain aliongeza: “Tuna shida sana ya vifaa, watu wasichoke kutuchangia ingawa kuna watu wanashangaa sisi kuchangisha.”

Aidha, Sheikh Muhammadain aliwashukuru Waislamu na wote walioyachangia kwa kuwaamini kwa kuchangia fedha. Uchangiaji huo ni sehemu ya utekeleza wa kampeni ya uchangiaji fedha kwa ajili
ya kituo hicho cha Mahaasin Tv kinachorusha matangazo yake kutokea jijini Mwanza.

Naye Sheikh Juma Ikusi wa Arusha ambaye ni mmoja wa waratibu wa tukio hilo alisifu itikio la watu waliojitokeza katika shughuli hiyo, licha ya mvua iliyonyesha.

Alisema shughuli ya kuichangia Mahaasin Tv ni muhimu kwa sababu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha vyombo vya habari vya Kiislamu hapa nchini. “Mahaasin Tv ni kituo muhimu kinachotazamwa na kusikilizwa sana katika eneo la Kanda ya Ziwa,” alisema Sheikh Ikusi na kuongeza kuwa kuimarika kwa kituo hicho ni kuimarisha jitihada za kuimarisha shughuli za da’awah Tanzania. Sheikh Ikusi alihimiza Waislamu waendelee kuchangia kituo hicho na vituo vingine vya Kiislamu, na kutaraji malipo kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Siku ya Malipo.

Tamasha hilo lililohudhuriwa na Waislamu takriban 6,000, lilishereheshwa na Masheikh mbalimbali akiwamo Sheikh Saidi Basanaa na Sheikh Hassan Ahmed kutoka Kenya, Sheikh Abdurahman Mhina (Baba Kiruwasha) kutoka Dar es Salaam, Sheikh Ibrahim Twaha kutoka Morogoro na Sheikh Abdulbasit Othman kutoka Mwanza.

Nao, baadhi ya Waislamu waliohudhuria tamasha hilo wameushukuru uongozi wa Mahaasin Tv kwa kuratibu tamasha hilo huku wakiwataka wenzao kuendelea kuchangia vyombo vya habari vya Kiislamu ili viweze kujiendesha.

“Nasi tumefanya jitihada zetu ili kusaidia ndugu zetu hao kama Allah anavyotutaka Waislamu kusaidia hata kwa chochote alichonacho mtu.” Alisema Mmoja wa wahudhuriaji hao Khatibu Said.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close