2. Taifa

Waislamu wakumbushwa kutoa zaka, sadaka kusaidia wanyonge

Jumuiya ya Ahbaabul-Khairiya imewakumbusha wafanyabiashara, wapenda kheri na Waislamu kwa ujumla kokote walipo nchini juu ya wajibu wao wa kutoa zaka, sadaka na kuunga mkono kazi za kuhudumia jamii zinazofanywa na taasisi mbalimbali makini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jumuiya hiyo iliyofanyika Mwananyamala, Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ahmed Shebe alisema watu walio katika mazingira magumu wanahitaji usaidizi wa karibu na wanaopaswa kufanya kazi hiyo ni jamii inayowazunguka.

“Wafanyabiashara wakitoa zaka zao, na sisi watukumbuke. Na niwahakikishie kuwa zitafika mahali husika, kwa wenye uhitaji,” alisema Shebe akikusudia yatima, wajane na wagonjwa wa majumbani; makundi matatu ambayo jumuiya hiyo inashughulika kuwasaidia.

Akielezea mfumo wa ufanyaji kazi wa jumuiya hiyo, Shebe alisema wao wanawafuata makundi hayo ya wanyonge hukohuko walipo.

“Hatuna kituo useme utakuja kuwaona, tunakwenda majumbani kama Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alivyoelekeza,” alisema Shebe.

Kwa mujbu wa Shebe, jumuiya ilianza rasmi kufanya kazi zake toka mwaka 2016, na tangu wakati huo hadi sasa jumuiya hiyo imejijengea uaminifu miongoni mwa watu kutokana na weledi na uaminifu katika kufikisha michango ya watu kwa walengwa.

“Leo tunazindua, lakini haina maana kuwa leo ndiyo tumeanza kazi. Tulianza muda mrefu, tunayo miaka minne sasa. Mpaka sasa tunahudumia wajane 62, yatima 123 na wagonjwa 9 katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam,” alisema Shebe.

Kwa muda ambao tumefanya kazi bado hatujapa wachangiaji wakubwa. Chanzo kikubwa cha fedha ni michango yetu ya kila mwezi. Tungependa tuwe na wadau ili ndugu zetu wanaoishi katika mazingira magumu waweze kusaidika,” alisema.

Shebe aliwahakikishia Waislamu kuwa, taasisi yao ina uwazi wa hali ya juu katika matumizi ya fedha hivyo wafanyabiashara, wananchi na wadau wengine watakaoguswa na kutoa fedha zao wataonyeshwa namna fedha hizo zilivyotumika na wanufaika walipokea sadaka yake.

“Jumuiya yetu inaaminika sana. Tunao watu wetu wa mahesabu hivyo kila shilingi inayoingia inadhibitiwa. Hakuna fedha inayopotea. Tunaomba wapenda kheri ambao wanabajeti ya mwaka watuangalie kwa jicho la pekee na watuamini,” alisema.

Kuhusu namna wanavyowapata wanufaika, Mwenyekiti huyo alisema wana mifumo mizuri ambayo hairuhusu wadanganyifu kupita, ikiwemo kushirikiana na ofisi ya serikali ya mtaa na imam wa msikiti ili kupata taarifa sahihi za muombaji. Alisema pia, kunakuwa na timu kutoka makao makuu inayokagua kabla misaada haijaanza kutolewa.

Jumiya hii changa ilisajiliwa rasmi na kukabidhiwa cheti chake mwaka 2019 pale mjini Dodoma, lakini ilishaanza kazi tangu mwaka 2016 kupitia kibali cha muda. Usajili wa Ahbaabul-Khairiya umairuhusu taasisi hii kufanya kazi katika mikoa mitano ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Tanga na Dodoma lakini kwa sasa wapo katika mikoa miwili, tu mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close