2. Taifa

Prof Assad ataka asasi za Kiislamu zikumbatie weledi

Mkaguzi Mkuu mstaafu wa hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Assad amewashauri viongozi wa taasisi za Kiislamu kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea jambo linalodumaza maendeleo ya taasisi zao.

Akiongea katika semina maalumu ya viongozi wa taasisi na wamiliki wa shule ilIyoandaliwa na Umma Education Think Tank Forum katika ukumbi wa DYCCC jijini Dar es Salaam alisema biashara za taasisi nyingi za Kiislamu zinakwama kwa sababu hawatumii wataalamu ipasavyo.

Pia, Prof Assad alitaja sababu nyingine zinazofanya taasisi zishindwe kufanikiwa ni kukosa mifumo mizuri ya udhibiti rasilimali; na hivyo alishauri njia kadhaa sahihi za kufuata ili kuleta tija na muendelezo katika biashara. Moja ya njia ambazo Prof Assad alishauri ni pamoja na kuweka mkazo katika dhana za udhibiti (tools) ikiwemo cheki ambayo inasaidia kuweka kumbukumbu za matumizi ya fedha katika taasisi. Alisema matumizi ya cheki ynafanya mwendeshaji wa biashara asikutane na fedha taslimu mara kwa mara na hivyo kupunguza migogoro ndani ya taasisi kwa sababu fedha zote zinapitia benki. Alifafanua kuwa hiyo ni njia ya kulinda rasimali za taasisi (safe guarding of asset).

Njia nyingine ya pili ya kufuata aliyoshauri ni uandaaji wa tararifa za fedha (financial statement), mathalan kwa vipindi vya miezi mitatu, sita au mwaka kutegemeana na sera ya taasisi.

“Kwa ninavyofahamu, taasisi nyingi za Kiislamu hazifanyi hivi. Kama hamuwezi, tafuteni wataalamu ili wawasaidie kuandaa taarifa za fedha,” alisema Prof Assad na kuongeza: “Taasisi inatakiwa iwe hivyo. Kila kitu weka rekodi. Kiwe kidogo au kikubwa, weka kumbukumbu. Na kazi hiyo inapaswa kuwa endelevu,” alisema Prof Assad.

Prof Assad pia alishauri kuwe na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuwe na ufanisi wa kazi, ambapo kazi ya mtu mmoja isifanywe na wawili.

Prof Assad pia alishauri kila kitu kinachofanywa katika taasisi kiendane na maudhui. Pia, aliwataka wasitoke nje ya lengo.

“Kama umelenga biashara ya shule, basi iwe hiyo na usiyumbe na na kuhamia katika nyingine.”

Mambo mengine ambayo Prof Assad aliyasisitiza ni kuwe na mfumo mzuri wa kubadilisha viongozi na kusiwe na ung’ang’anizi wa madaraka kwani taasisi hizo zipo ajili ya kuhudumia jamii. Kadhalika, Prof. Assad aliwataka viongozi wa taasisi kujifunza vitu vipya na kuwa wabunifu ili kuboresha biashara zao.

Hata hivyo, katika mambo ambayo Profesa aliyasisitiza sana ni kumuomba Mwenyezi Mungu.

“Mkimshirikisha Allah mambo mengi yatafanikiwa. Naamini mkiyafanya haya mtaanza kuona mabadiliko katika shule zenu.”

Wawezeshaji…

Kwa upande wake muwezeshaji wa semina hiyo, Unguu Ramadhani Sulay alisema ili taasisi za Kiislamu zifanikiwe, ni lazima waweke mipango mizuri na mkakati wa utekelezaji wake, jambo ambalo linahitaji wataalamu.

Sulay alisema haoni sababu ya kuwa na utitiri wa shule za kiislamu zisizo na sifa nzuri wakati wangeungana wangemiliki shule kubwa, yenye rasilimali zote na itakayovutia wazazi wengi kuleta watoto wao kusoma hapo.

“Hivi sasa naona tuna shule nyingi, tunanyang’anyana wanafunzi. Tunaanza kujipiga fitina wenyewe. Kwa nini kupitia mwamvuli wetu wa TIPSO tusije na shule mfano?” alihoji Suley na kusisitiza kuwa inawezekana kabisa kuwa na shule kubwa ya Kiislamu ambayo inatakuwa kimbilio la wengi.

Suley ambaye ni mtaalamu bingwa wa uhasibu pia alisistiza umuhimu wa kutumia wataalamu kutengeneza mipango mikakati (strategic plans). mifumo (systems) kama ya kiutawala (management information system), ya kiuhasibu (accounting management system) na kadhalika.

Mtoa mada mwingine Bi Farida Alkhaify aliwataka wamiliki wa shule kulipa kipaumbele suala la ukaguzi wa hesabu zao kwa sababu hiyo inasaidia kudhibiti rasimali za taasisi.

“Nina hakika taasisi nyingi hazina tabia ya kukagua taasisi zao. Usipofanya ukaguzi, hautaweza kujua maendeleo ya taasisi. Ukaguzi unagusa mambo mengi ikwemo rasilimali watu, fedha, kodi na mambo mengine mengi,” alisema Bi Alkhaify.

Alisema ukaguzi unakumbusha dira ya taasisi na kwamba wakaguzi hung’amua sehemu zenye kasoro na kushauri namna ya kurekebisha.

Naye Mratibu Mtendaji wa semina hiyo, Bw. Juma Nchya alisema ameridhishwa na mahudhurio ya semina hiyo. Nchia alisema:

“Sikutegemea Waislamu wangeitikia kwa wingi kiasi kile ukizingania ni harakati ambazo zimebuniwa kupitia kundi la WhatsApp.”

Baada ya semina hii iliyohudhuriwa na washiriki zaidi ya 180, Nchia alisema sasa wanajipanga kufanya semina nyingine mikoani.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close