2. Taifa

Nyumba ya Milioni 30 yamsubiri mshindi mashindano ya Qur’an

Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Tukufu Tanzania imeanza mchujo wa kusaka wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kimataifa ya kuhifadhi Qur’an yatakayofanyika Mei 17 mwaka huu.

Mchujo huo unaoanzia katika ngazi ya mkoa na kisha kanda pia utatoa washiriki watakaoshindana katika fainali za mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Mei 9 katika uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.

Mratibu wa mashindano hayo, Sheikh Mtoro Bakari ameliambia gazeti Imaan kuwa anatarajia ushindani mkali mwaka huu ukizingatia kuwa mshindi wa kwanza anatarajiwa kupewa zawadi ya nyumba yenye thamani ya TSH Mil 30.

Akitaja ratiba ya mashindano hayo ngazi ya kanda, Sheikh Bakari alisema yataanza Februari 29 katika Kanda ya Kati (Singida) na kufuatiwa na kanda ya Kaskazini (Arusha) Machi 8.

Mnamo Machi 21 mwaka huu, mchujo utaenda Kanda ya Ziwa (Mwanza – Msikiti wa Ijumaa). Kisha utaenda kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya) Aprili 4. Mchujo wa mwisho utafanyika kanda ya Kusini (Lindi) Aprili 18. Kanda ya Pwani ndio itahitimisha mchujo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa NSSF siku ya Mei 2.

Kabla ya mchujo wa kanda, Sheikh Bakari alisema mikoa katika kanda
husika nayo itafanya mashindano yake madogo kupata washiriki watakaoiwakilisha katika kanda.

Sheikh Bakari alisema, kilele, kwa maana ya fainali, za mashindano hayo ya kitaifa zitafanyika Mei 9 mkoani Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri huku mashindano yake makubwa kabisa ya kimataifa yanayosubiriwa kwa hamu yakitegemewa kufanyika Mei 17 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Sheikh Bakari alisema, katika ngazi ya kanda, zaidi ya washiriki 45 wanatarajiwa kujitokeza ambapo washindi watapatiwa motisha ya fedha, ambazo hakuziweka wazi.

Sheikh Bakari alisema: “Tunatarajia mchujo mkali mwaka huu, ndio maana tukaweka zawadi kubwa ya nyumba…Lengo letu kubwa ni kufanya mapinduzi makubwa kwa vijana wetu katika maadili na tabia.

Licha ya nyumba, washindi watano wa juu pia watapata zawadi mbalimbali.

Qur’an ni amani

Sheikh Bakari alisema, kauli mbiu ya mashindano ya mwaka huu ni Qur’an ni amani. Alisema, kila watakapokwenda kuendesha mashindano hayo watatanguliza mhadhara ili kuelezea umuhimu na faida ya amani katika jamii kwa mujibu wa Qur’an na Sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close