2. Taifa

Mufti: Msidai haki kwa kuvunja haki

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar bin Zubeir bin Ally Mbwana amewataka Watanzania kutohalalisha fujo kwa kisingizio cha kudau haki.

Sheikh Zubeir alitoa wito huo jana, Ijumaa Septemba 25 wakati akizindua kitabu cha ‘Nasaha kumi kuelekea Uchaguzi wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani’ kilichoandikwa na Sheikh Mohammed Iddi (Abuu Iddi).

“Ukitetea haki kwa kuvunja haki ya mtu ni makosa makubwa sana…Ukivunja sheria ili kudai haki mchakato wa kudai haki utakuwa umeukosea,” alisema Sheikh Zubeir.

Mufti Zubeir alifananisha kudai haki kwa fujo na matendo ya Iblis yaliyosimuliwa katika Kitabu Kitukufu cha Qur’an. Alisema Iblis alikaidi amri ya Mwenyezi Mungu kwa kisingizio cha kudai haki ya kwamba yeye ni bora kuliko baba yetu Nabii Adam.

“Tukumbuke kile kisa maarufu cha Iblis ambacho ni maarufu watu wote wanakielewa alipoamrishwa amsujudie Adam ambaye huyu ndie baba wa watu wote, alikataa yeye. Na madai yake ya kukataa ni jambo dogo tu kwamba yeye kaumbwa kwa moto na Adam kaumbwa kwa udongo. Akaona yeye kaumbwa kwa kitukufu zaidi na Adam kaumbwa na kitu duni, anavyoona yeye (Iblis).” Alieleza Sheikh Zubeir.

Alisema kitendo hicho cha kufanya fujo ya kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Muumba wa kila kitu, kilipekelekea Iblis alaaniwe na kufukuzwa. “Angekuwa huyu Iblis anajua wajibu, angeutekeleza,” alisema Sheikh Zubeir.

Vilevile katika nasaha zake, Mufti aliwataka wagombea katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 28 waamini kuwa kushinda kunatokana na ridhaa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kwamba kama hakuandika upate, hata ufanyeje hupati.

Mufti Zubeir alisema kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayefanya mtu apate. Alisema, mtu hata awe na juhudi kiasi gani kama Mwenyezi Mungu Sub’haanahu wataala kaandika asipate, hatapata. Na hata akiwa dhaifu kiasi gani, kama Mwenyezi Mungu akitaka mtu huyo apate, basi bila shaka atapata, licha ya unyonge alionao.

Katika hatua nyingine, Sheikh Zubeir amewataka Watanzania kumheshimu Rais John Pombe Magufuli kwa sababu licha ya kuwa ni mgombea, bado yeye ni rais wa nchi. Mufti Zubeir alisema, kumheshimu rais ni wajibu wa Watanzania wote na kwamba jambo hilo inafaa litazamwe vizuri.

Katika kufafanua suala hilo, Mufti Zubeir alitoa ushahidi kadhaa wa hadith za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) zinazotaka watu wapewe heshima kadri ya hadhi zao.

Katika moja ya hadith alizonukuu, Sheikh Zubeir alimnukuu Mtume (rehema za Allah na amani zishukie) kuwa amesema: “Wawekeni watu katika daraja zao” na katika hadith nyingine: “Katika mambo mabaya ni mtu kumvunjia heshima mwenzake.”

Mufti alimsifu mtunzi wa vitabu hivyo na kuwataka Watanzania wanunue kitabu hicho, wasome na wafanyie kazi yaliyomo. Aidha, katika kumuunga mkono Mtunzi ili ujumbe uliomo katika vitabu hivyo usambae Mufti alinunua vitabu mia na kuvigawa kwa watu waliohudhuria ghafla hiyo.

Mufti Zubeir pia alitoa rai kwa Sheikh Abuu Iddi aandike vitabu vingine viwili kuhusu wajibu wa viongozi kwa raia na kingine wajibu wa raia kwa viongozi iwe muongozo kwa wale watakaochaguliwa na ili raia wajue wajibu wao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close