2. Taifa

Mazito yaibuka ufaulu duni EDK

Wadau wadai maboresho

Ufaulu duni wa somo la dini ya Kiislamu kidato cha sita umezua mjadala mpana kuhusu ufundishwa wa somo hilo katika ngazi ngazi zote za elimu. Wadau wameibua masuala kadhaa muhimu huku pia wakitoa wa kufanyika maboresho katika maeneo kadhaa.

Mijadala hiyo katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ya Waislamu iliibuka baada ya taarifa iliyandaliwa na Mohamed Mikombe wa Tabora juu ya hali ya ufaulu wa somo la dini ya Kiislamu (Islamic Knowledge), ikionesha kuwa somo hilo limezidi kuporomoka kwa miaka mitatu mfululizo, kote Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa kupitia taarifa hiyo, mwanaharakati Juma Nchia alichochea mijadala katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii ambapo wengi walitoa mitazamo yao. Kwa mujibu wa taarifa ya Mikombe, somo hilo ndio pekee Tanzania ambalo kwa miaka mitatu mfululizo kidato cha sita hakuna mwanafunzi aliyepata alama A wala B. Pia, katika miaka hiyo mitatu, hakujawahi kupatikana wanafunzi 15 waliopata C kwa nchi nzima.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mikombe, mwaka 2019 licha ya kukosekana mwanafunzi hata mmoja aliyepata A au B, waliopata alama C walikuwa 13 tu, huku wengine wakiambulia D (117), E (305), S (164) na F (264).

Mwaka 2020 nao, hakukuwa na A wala B huku C zikiwa 9, D (117), E (368), S (223) na F (300).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sio tu ufaulu unashuka bali hata idadi ya wanafunzi wanaochukua somo hilo inazidi kupungua kila mwaka. Kwa mfano, mwaka huu katika mkoa wa Dar es Salaam ni shule 10 tu zilizokuwa na wanafunzi waliofanya mtihani huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo ambayo hata hivyo Gazeti Imaan halijaweza kuzithibitisha.

Mmoja wa wadau alisema takwimu hizo zinasikitisha na kwamba inatakiwa juhudi kubwa ya kuhamasisha wanafunzi juu ya faida ya kuisoma na kuitambua dini yao na kisha kuifanyia kazi.

“Hawawezi kutambua dini yao vema kama hawasomi somo hili. Takwimu hizi za ufaulu na idadi ya wanaochukua somo hilo zinashtua,” aliandika mdau huyo.

Masuala yaliyoibuliwa

Baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na wadau ni pamoja na mitaala, ubora wa walimu, maslahi ya walimu, vitendea kazi na lugha ya kufundishia, utayari wa wanafunzi.

Wengi kati ya wachangiaji walihoji kuhusu ugumu wa mitaala na vitabu vya kiada ukilinganisha na viwango vya wanafunzi, huku baadhi wakidai mitaala ya sasa ya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ingeweza kutosheleza kidato cha kwanza hadi cha sita, na ile ya sita ingefaa kufundishwa chuo kikuu.

Pia, wapo waliodai kuwa mtaala umejaa filosofia ya dini zaidi kuliko kumpa mwanafunzi elimu itakayoweza kumsaidia kutekeleza Uislamu wao.

“Mzizi wa tatizo ni mtaala na utunzi wa mtihani. Nina uhakika mtihani wa EDK akipewa mhitimu wa ‘thanawy’ atafeli. Too philosophical (umekaa kifalsafa sana),” alisema mchangiaji mmoja.

Thanawy hapa imetumika kumaanisha mhitimu wa kiwango cha elimu ya sekondari katika masomo ya Kiislamu.

Mchangiaji mwingine alisema, kwa sababu ya kujazwa filosofia zaidi za dini, ni nadra kwa mtaala huo kumtoa mhitimu anayeweza kuwa Khatib na Imam wa sala ya Ijumaa. Mchangiaji huyo alishauri filosofia ipunguzwe na badala yake yaongezwe maarifa ya utekelezaji wa dini.

Baadhi ya wadau walisema walifanya ulinganishi na vitabu vya somo hilo vya nchi nyingine na kugundua kuwa kuna walakini katika vitabu vyetu.

“Huwa nasoma vitabu vya watoto vya Kiislamu vilivyoandaliwa na Waturuki ukilinganisha na hivi vyetu unaona kabisa kwanini watoto wetu wanafeli,” alidai mdau mmoja.

Baadhi ya watu walisoma zamani katika shule mbalimbali maarufu za Kiislamu jijini Dar es Salaam kama Kunduchi, Ununuo na Alharamain walitoa ushuhuda wa ugumu wa mitaala, ambapo walisema wakati mwingine hata wanafunzi waliotegemewa sana kufaulu waliishia kupata alama ndogo na za kukatisha tamaa.

Wapo pia wachangiaji walioonesha wasiwasi kuwa huenda kuna walakini katika utunzi wa mitihani na zoezi la usahihishaji.

“Ni kweli somo mitaala iko kifalsafa zaidi lakini hata sisi tuliofundishwa na wasomi mahiri na kujibu sawasawa tulifeli. Kweli ile F mpaka leo sijajua ilitoka wapi? Hujuma?,” alihoji mdau mmoja.

Hata hivyo, wengi waliosoma somo hilo, licha ya kukiri ugumu wa mtaala ambao kwa maoni yao unafaa kufundishia chuo kikuu tahasusi za dini, bado wanakiri kuwa somo hilo liliwakomaza na kuwapatia maarifa ya dini na hawajutii.

Jambo jingine lililoibuliwa ni ubora wa walimu, elimu zao, malipo, vitendea kazi. Ilionekana kwanza kuna uhaba wa walimu na hata wale waliopo hawajaandaliwa ipasavyo kufundisha somo hilo. Pia, ilionekana kuwa kipato cha walimu ni duni sana, au aghlabu wengi hujitolea tu.

Utayari wa wanafunzi wenyewe pia uliangaziwa, ambapo wachangiaji wengi walikiri kuwa somo la dini, katika ngazi zote, halipewi kipaumbele kwa sababu watu wanaamini halitampatia mhitimu ajira.

Moja ya sababu zilizotajwa kupunguza ari ya wanafunzi kusoma somo la dini ni kutochangia kwa somo hilo katika maksi za kwenda chuo kikuu, kama ilivyokuwa zamani.

Baadhi ya wachangiaji walitaja wanafunzi kutosoma madrasa kabla ya kwenda sekondari kuwa ni kikwazo kingine kinachopelekea kufeli kwa sababu wanakuwa kama wanaanza upya kabisa.

Suala jingine lililojadiliwa ni matumizi ya lugha ya Kiingereza kufundishia somo hilo kidato cha sita, huku baadhi wakihisi kuwa huenda pia ni kikwazo cha kufikisha maarifa ya somo hilo.

“Kwanini tunawafundisha kwa Lugha ya Kingereza? Lengo vijana waujue Uislamu au wajifunze kingereza? Nafikiri tuanzie hapo. Watu wanakosa kuujua Uislamu kwa kufanya ‘promotion’ ya kingereza. Wakawahubirie kina nani?,” alihoji mdau mmoja.

Mapendekezo

Miongoni mwa maendekezo makubwa yaliyotolewa na watu wengi ni mapitio ya mitaala ili uendana na kiwango husika. Pia, wadau walitaka mtaala uguse maarifa muhimu ambayo mwanafunzi anayahitaji katika kutekeleza Uislamu wake kuliko filosofia.

Ilipendekezwa pia kuwa katika kufanyia mapitio mitaala hiyo, kuwepo na ushirikishwaji mpana wa wadau wote muhimu.

Pia ilishauriwa kufanyika kwa tathmini ya ufaulu kwa miaka kadhaa na pia mapitio ya aina ya mitihani wanayopewa wanafunzi ili kuona kama inafaa.

Pendekezo jingine lililotolewa na wengi ni walimu wa somo la elimu ya dini ya Kiilamu waaandaliwe vema ili wawe sifa stahiki za kufundisha somo hilo. Wadau kadhaa walishauri kuandaliwe kambi maalumu kwa ajili ya kuwapa semina ya kuwajengea uwezo wa kufundisha kwa mtindo ambao ni rahisi kwa hili somo kueleweka.

Pia, ilishauriwa kuwe na kampeni ya kuhamasisha walimu, wanafunzi kulipa kipaumbele somo hilo, kama ilivyo kwa masomo mengine. Moja kati ya mkakati wa kufanikisha hili, ilishauriwa, iwe ni kufanya lazima wanafunzi kusoma somo hilo na kurejesha wanafunzi mwaka iwapo watashindwa kufaulu kwa kiwango fulani.

Labda miongoni mwa mapendekezo pendwa zaidi kwa wengi juu ya kutatua mkwamo huu ni kuitishwa kwa mjadala mpana kuhusu somo la dini ya Kiislamu ngazi zote – msingi, sekondari na sekondari ya juu – ukiongozwa na Islamic Edication Panel, wanaotajwa kuratibu somo hilo.

Kabla ya mjadala huo, baadhi ya watu wapendekeza, ufanyike uchambuzi wa kina juu ya masomo hayo kujaribu kung’amua kwa kiasi gani malengo yanafikiwa, changamoto zilivyopo, vyanzo vyake na mengineyo.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close