2. Taifa

Mauaji ya Rwanda yalivyomsukuma Sheikh Kishk kuandika kitabu

Asema Tanzania muhimu kuliko chama, mgombea au uchaguzi

Mkurugenzi wa taasisi ya AlHikma Foundation, Nurdin Mohammad Ahmad, maarufu kwa jina la Sheikh Kishk, amesema tukio la kusikitisha la mauaji ya kimbali ya Rwanda mwaka 1994 ni moja ya sababu tatu zilizompelekea kuamua kuandika kitabu chake cha kwanza kinachozungumzia amani kiitwacho ‘Kwa nini amani?’

Sheikkh Kishk alitoa kauli hiyo katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini na kiserikali.

Ilikuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye aliyezindua kitabu hicho jijini Dar es Salaam huku akishuhudiwa na baadhi ya masheikh wakubwa waliohudhuria wakiwemo Sheikh Mohammed Khalifa, Sheikh Twalib Ahmad, Sheikh Hamid Abdallah, Sheikh Suleiman (Mtambani), Sheikh Hashim Madenge, Sheikh Hasssan Katungunya.

Sheikh Kishk alisema alipata wazo la kuandika kitabu hicho baada ya kurejea safari kutoka safari ya mwisho ya kidini aliyofanya nchini Rwanda mwaka 2014. Katika ziara hiyo, msafara wa Sheikh Kishk ulipelekwa katika Jumba la Makumbusho la taifa kushuhudia mabaki ya miili, hususan mafuvu ya watu waliouawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka 1994.

Alisema aliyoyaona, ikiwemo watu wanaotembelea kuwaombea marehemu ndugu zao hali hawawajui fuvu lipi ni la ndugu yao, wengi wakiwa wamegubikwa na huzuni kubwa, iliwasikitisha na kuwasononesha mno yeye na wenzake, hivyo aliporudi nchini akaamua aanze mradi huo wa uandishi wa kitabu.

Sababu ya pili: Uchaguzi mkuu

Sheikh Kishk alitaja sababu ya pili ya kuandika kitabu hicho kuwa ni uchaguzi mkuu ambapo alisema kupitia kitabu hicho naye anatoe nasaha zake katika kuhimza amani.

Sheikh Kishk alisema amegundua kuwa mtikisiko wa amani Afrika huja na uchaguzi.

“Hivi leo wagombea mbalimbali kupitia kampeni mbalimbali (wanatoa) lugha zinazotishia amani (na) maneno makali yanayoweza kukutia hofu. Usipoziba ufa, utajenga ukuta. Ni bora wagombea wakabaki katika kuelezea nini watafanya kwa raia zao na watu kwa ujumla kuliko wakawa wanashambuliana wao kwa wao na kutumia maneno makali.”

Akitoa mfano wa maneno yenye ukakasi ambayo wanasiasa wamekuwa wakiyatumia kuwa ni pamoja na ‘Mwaka huu lazima mambo yaharibike’ ‘Lazima damu imwagike’ na kadhalika.

Kutokana na kauli hizo, Sheikh Kishk aliwaasa wanasiasa waelewe kuwa damu wanayozungumzia si ya mtu mwingine bali ndugu zao wakiwemo, mama, baba, mjomba, shangazi, kaka, dada au Watanzania wenzao kwa ujumla. Sheikh Kishk alisema umwagaji damu ni dhambi kubwa ndio mama hiyo ndio itakuwa kesi ya kwanza kusikilizwa Siku ya Kiyama.

Sababu ya tatu: Vikundi vinavyochafua dini

Akitaja sababu ya tatu ya kuandika kitabu, Sheikh Kishki alisema amekusudia kuutetea Uislamu dhidi ya shutuma na madai kuwa ni dini inayochochea fujo na kuharibu amani.

“Kwa utafiti wangu, nimegundua kuwa wapo watu wanaharibu amani ya ulimwengu na walimwengu kwa kisingizio cha dini. Nikaona niandika kutetea dini yangu kuwa hakuna dini inayotetea amani kama Uislamu. Na kama wapo wanaotumia vibaya aya za Qur’an, mafundisho ya Mtume, basi hao ndiyo hawaajaelewa bali msimamo sahihi ni kuwa Uislamu ni dini inayotetea amani,” alisema Sheikh Kishk.

Akitoa ushahidi unaoonesha namna Qur’an inavyohimiza amani, Sheikh Kishk alisema ukisoma Kitabu hicho kitukufu utaona kuwa neno la ‘mapigano’ limejitokeza mara 40 tu, lakini neno ‘amani’ limejitokeza zaidi ya mara 360.

Katika miaka ya karibuni kumekuwa na makundi yanayoibuka katika nchi mbaimbali duniani na kufanya mauaji kwa jina la Uislamu. Makundi hayo yanadai yanapigana jihadi huku yakishiriki katika mauaji ya watu wasio na hatia kupitia vitendo vya kigaidi, na hivyo kuharibu taswira ya dini tukufu ya Uislamu.

Kwa nini amani?

Katika hafla hiyo ya uzinduzi, Sheikh Kishk alijibu kwa ufupi swali muhimu linaloulizwa katika kitabu hicho ‘Kwa nini amani?’ ambapo alisema Mola aliyewaumba wanadamu ametutaka tuishi kwa amani, kwa ushahidi wa Qur’an aliouwasilisha. Kadhalika, Sheikh Kishk alinukuu hadithi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye alisema atakayeamka akawa amani ya kutosha, afya na chakula cha kula katika siku yake hiyo, basi huyo kapewa dunia yote.

Akizungumzia umuhimu wa amani kwa Tanzania, Sheikh Kishk alifananisha nchi na jahazi lenye madaraja ambalo Watanzania wamo humo, lakini alionya walio chini wakitoboa watu wote waliomo Tanzania watakuwa wameangamia. Sheikh Kishki alisema:

“Walio chini, kukaa kwao chini siyo unyonge. Walio juu kukaa kwao juu siyo fakhari,. Tusiruhusu jahazi litobolewe.”

Sheikh Kishki alisema, amani iliyojengwa na watu elfu inaweza kuvunjwa na mtu mmoja; na amani iliyojengwa kwa siku elfu moja inaweza kuvunjwa kwa dakika moja.

“Sote tuwe wajenzi wa nyumba ya amani ya Tanzania, na siyo wabomoaji,” alisisitiza Sheikh Kishk.

Alihoji, ikiwa mbomoaji mmoja anaweza kubomoa nyumba ya amani iliyojengwa na watu elfu moja, vipi wabomoaji elfu wanaweza kufanya dhidi ya mjenzi mmoja wa amani. Alisema, amani ikiharibika hakuna watu watapata tabu kama Watanzania. Sheikh Kishk Watanzania hawajatembea, na iwapo watatembea wataona thamani ya nchi nchi yao.

Wito kwa masheikh

Katika hudhurisho lake, Sheikh Kishk alitoa wito kwa viongozi wa dini wawe kati kati (neutral) ili waweze kuwa wasuluhishi wazuri pale mambo yanapoelekea kwenda mrama.

Sheikh Kishk alisema: “Sisi, (viongozi wa dini) tuwe wasuluhishi pale viongozi wa siasa wanapolumbana na wakatumia lugha kali inayoashiria uvunjifu wa amani. Lakini leo viongozi wa dini tulielemea upande mmoja tukapiga debe hakika hili ni tatizo. Mambo yakiharibika hawezi kuletwa mezani akasuluhisha kwa sababu tayari kashajionesha ni kada wa chama fulani. Sisi wa katikati ndiyo tunaoweza kutoa onyo, makemoe kuwa huko tunakokwenda siko.”

Kuhusu Sheikh Kishk Sheikh Nurdin Mohammad Ahmad ana miaka 25 ya uzoefu katika ulinganiaji ambapo ametembelea mikoa yote ya Tanzania isipokuwa Ruvuma. Pia, amewahi kuzuru kwa kazi ya da’awa nchi za Afrika ya Mashariki zikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Msumbiji, Afrika ya Kusini na nchi nyingine kadhaa za Arabuni.

Ukiacha mihadhara na makongamano, Sheikh Kishk amekuwa anafanya kazi ya ulinganiaji kupitia vyombo vya habari vikiwemo ZBC – 2 ambako anaendesha kipindi cha Adhikraa. Mpaka sasa kupitia kipindi hicho Sheikh Kishk ameandaa vipindi zaidi ya 280. Sheikh Kishk pia anaendesha kipindi kingine kupitia chaneli yake ya YouTube ya Kishk Online TV.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close