2. Taifa

Forest Hill yatamani kuwa namba moja Tanzania

TAASISI ya The Islamic Foundation (TIF) imesema ina lengo la kuifanya shule yake ya Forest Hill iliyopo Morogoro Mjini kuwa namba moja kitaaluma na nidhamu sio tu Tanzania bali pia Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aref Nahdi katika mahafali ya 50 kuhitimu kidato cha nne ya shule hiyo ambapo Nahdi alialikwa kama mgeni rasmi.

Wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha nne shuleni hapo mwanzoni mwa wiki waliungana na wenzao kote nchini kuanza kufanya mitihani yao ya kitaifa kuanzia siku ya Jumatatu Novemba 4.

Katika hotuba yake, Nahdi aliwataka wazazi wa wanafunzi wanaosoma shuleni hapo kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa walimu pamoja na uongozi wa shule hiyo katika kupandisha taaluma na kusimamia nidhamu shuleni hapo ili malengo ya kuifanya shule hiyo kuwa bora Tanzania yafikiwe.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Abod Masoud, aliunga mkono malengo ya taasisi ya kuifanya shule iwe namba moja lakini pia alimhakikishia mgeni rasmi na wazazi kuwa, walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi hao wa kidato cha nne na hivyo wanataraji matokeo mazuri na ya kuridhisha katika mitihani yao ya taifa.

Naye Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Onaly Dogo aliipongeza TIF chini ya Mwenyekiti Aref Nahd kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya shule hiyo na kusaidia miradi ya kijamii ili kuleta maendeleo ya Uislamu na taifa kwa ujumla.

Wazazi kadhaa waliohojiwa na Gazeti Imaan walionesha kufurahishwa
na maendeleo ya shule hiyo na kusema wana imani kubwa kwa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF), uongozi wa shule na walimu wote.

“Kwa juhudi zinazofanyika tuna imani kubwa kuwa watoto wetu wapo katika mikono salama na Mungu akipenda watakuwa na mustakabali mwema kielimu,” alisema mmoja wa wazazi Bi. Mariam Juma.

Nasaha za Sheikh Kundya

Katika mahafali hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Da’awa wa taasisi ya TIF, Sheikh Ismail Kundya aliwasihi wahitimu hao kuhakikisha wanaendelea kushikamana na Qur’an kwani hiyo ndio dira na muongozo wa maisha yao duniani na kesho akhera.

Katika mahafali hayo zawadi zilitolewa kwa watu mbalimbali, ikiwemo wanafunzi wanaohitimu waliofanya vizuri katika maeneo mbalimbali. Pia, uongozi wa shule hiyo ulimkabidhi zawadi maalumu Mwenyekiti wa TIF, Aref Nahdi. Pia, kulikuwa na burudani ya mashairi pamoja nashid kutoka kwa wanafunzi hao.

Miongoni mwa waliohudhuria mahafali hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TIF, Sheikh Ibrahim Twaha ambaye alifungua shughuli hiyo kwa dua.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close