2. Taifa

Mkuu wa shule za DYCCC aonya matumizi ya mitandao kwa watoto

Wazazi na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili watoto hao wajifunze tabia njema kwa kuiga. Kadhalika, wazazi hao wametakiwa wawachunge watoto dhidi ya matumizi ya mitandao.

Wito huo umetolewa na viongozi wawili tofauti katika mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Yemen iliyopo Chang’ombe, Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Utamaduni na Misaada cha watu wenye asili ya Yemen waishio Dar es Salaam (DYCCC), Mohammed Abdallah bin Ishaq.

DYCCC ndiyo wamiliki wa shule ya Yemen.

Ibn Ishaq alisema njia nzuri ya mtoto kujifunza ni kuwa karibu na mzazi ili aige tabia, badala ya kuiga watu wengine wenye mila na desturi tofauti.

Ibn Ishaq aliongeza kuwa, mzazi anapaswa kuwa karibu na mtoto na ajenge urafiki naye ili (mtoto) awe huru kuuliza maswali ya kujifunza na kuiga tabia njema za mzazi.

Ibn Ishaq alisema, ukimkataza mtoto kufanya kitu fulani kwa kuwa ni haramu au kina madhara, ni vema ukamfafanulia pia madhara ya kitu hicho ili apate elimu hiyo. Alisema, kwa kufanya hivyo, mzazi atajenga hofu kwa mtoto na kumfanya asirejee kufanya hivyo tena. Aidha, Ibn Ishaqa metahadharisha kuwa, mapenzi na mtoto yasiwe yale ya kumruhusu kufanya kila kitu na badala yake mzazi ndiyo anatakiwa kutoa muongozo wa kitu gani mwanae afanye na kipi asifanye.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi za Shule za Elimu wa Shule za DYCCC, Hassan Akrabi, alisema changamoto iliyopo sasa katika malezi ni kukua kwa teknolojia ya mitandao hali inayopelekea vijana kuingia kwenye
mitandao hiyo bila ya kujua baya na zuri.

Akrabi aliongeza kuwa, watoto hawawezi kupembua vitu vibaya kwa sababu ya umri wao hivyo wazazi wana wajibu wa kuwasimamia na kuwaongoza kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Akrabi alikiri pia kuwa mitandao ya kijamii ina faida, kama ilivyo na hasara pia na hivyo kutaka wazazi kuwa na tahadhari kabla vijana hawajaharibikiwa kimaadili.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Wazazi ya Shule hiyo, Habibu Suluo amewataka vijana waliohitimu darasa la saba shuleni hapo kuendeleza maadili ya dini ya Kiislamu waliyopata shuleni hapo ili wapate radhi za Mwenyezi Mungu, Subhaanahu Wata’ala duniani na akhera.

Jumla ya vijana 89 wamehitimu elimu ya msingi shuleni hapo kati yao wavulana ni 43 huku wasichana wakiwa ni 46.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close