1. Habari2. Taifa

Mahujaji waliodhaminiwa na TIF, UAE AID waelezea safari yao

Baadhi ya mahujaji waliokwenda kutekeleza ibada ya Hijja mjini Makka nchini Saudia Arabia mwaka huu kupitia udhamini wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) na UAE AID wameishukuru taasisi hizo kwa kuwawezesha kutimiza ndoto yao ya kukamilisha nguzo ya tano ya Uislamu.

Shukrani hizo zimetolewa na mzee Yassin Mtabo pamoja na mzee Haruna Omary ambao wanatokea mkoani Katavi walipotembelea makao makuu ya TIF mjini Morogoro siku chache baada ya kurejea kutoka mjini Makka.

Mmoja wa mahujaji hao, alimsifu Mwenyekiti wa TIF kwa kutekeleza ahadi yake ya kuwapeleka Hijja. Wazee hao pia walimuombea Mwenyekiti huyo kwa Allah ampe nguvu ya kuendeleza zaidi harakati za kuendeleza Uislamu na kuzidi kufadhili watu kwenda Hijja.

Wazee hao wawili walipata fursa ya kutembelea vyombo vya habari vya Imaan, baada ya kurejea kutoka Makka. Katika ziara yao hiyo, wazee hao walijionea namna vyombo hivyo vya habari vinavyoendeshwa. Wakizungumza mwishoni mwa ziara hiyo, wageni hao waliwaomba Waislamu waunge mkono vyombo hivyo vya habari kwani vinatumika katika kazi ya kulingania Uislamu.

Mwaka huu, taasisi ya TIF ilipeleka mahujaji 16 kupitia ufadhili wa taasisi mbalimbali za kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Taasisi hizo ni pamoja na The Zayed bin Sultan Al Nahyan Charitable and Humanitarian Foundation, Dubai Charity Association na Sharjah Charity International.

Mahujaji waliokwenda Hijja mwaka huu wanasimulia kuhusu maendeleo makubwa ya huduma za mahujaji yaliyofanywa na Serikali ya Saudi Arabia, ingawa pia kulikuwa na changamoto kubwa ya mahema katika eneo la Mina ambapo mahujaji walichelewa kupata mahema yao; na hata walipopata walibanana sana, licha ya baadhi yao kulipia madaraja ya juu.

Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa taasisi za kusafirisha mahujaji, Sheikh Haruna Kapama wa Khidmat na Peace Travel, tatizo la mahema lilikuja baada ya baadhi ya taasisi za Kitanzania kuchelewa kulipa fedha za huduma ya mahema.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close