1. Habari2. Taifa

Mahujaji kuweni mfano bora kwa jamii

Wiki zilizopita, kundi la mwisho la Mahujaji wa Tanzania lilirejea nchini kutokea mjini Makka, Saudi Arabia walikokwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hijja kwa mwaka 1441 Hijriya.

Hijja ya mwaka huu imekuwa na mafanikio makubwa hasa kutokana na maboresho katika sekta ya miundombinu, usafiri, afya, ulinzi na usalama, zikiwa ni juhudi za serikali ya Saudi Arabia iliyoweka kuweka mipango madhubuti ya kuboresha ibada ya Hijja na kurekebisha dosari zilizowahi kujitokeza miaka ya nyuma. Wakati mahujaji wakirejea, swali la muhimu, ni je, baada ya kukamilisha ibada ya Hijja, ni kwa kiwango gani wataweza kufikia kilele cha tabia njema na maadili ya dini? Ni Allah Aliyetukuka pekee anajua jawabu la swali hili kiuhakika, zaidi lakini sisi tunawahimiza mahujaji kuwa na ari ya kujijengea misingi imara ya kitabia na kujiweka mbali na matendo mabaya ili wawe mfano wa kuigwa na wengine.

Hakuna shaka juu ya ibada ya Hijja kama nembo muhimu zinazoutambulisha Uislamu, na kwa sababu hiyo si jambo linalotarajiwa kwa Waislamu hasa waliohiji kuishi kinyume na matakwa ya dini.

Kama walivyojitahidi katika kuhifadhi, kulinda na kuimarisha mawasiliano na Allah wakati wa Hijja, pia Mahujaji wanapaswa kuendelea na hali hiyo baada ya Hijja. Tunasema hivyo kwa sababu tabia kwa mwanadamu ni kama vazi, na wakati mwingine huchukuliwa kuwa ndiyo kipimo cha utu.

Umma wa Kiislamu umebahatika kulelewa katika misingi ya viwili hivyo. Qur’an yasema: “Hakika nyinyi mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho…” [Qur’an, 33:21]. Pia, imesimuliwa kutoka kwa Abu Hureira (Allah amridhie) kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Nimetumwa kukamilisha tabia njema.” [Ahmad].

Tunapotafakari kwa kina juu ya kauli hizi tunabaini kuwa, hakuna pambo nadhifu kwa Muislamu isipokuwa tabia njema. Na tabia njema yenye maana pana zaidi, ambayo kila Muislamu anatakiwa kuwa nayo, ni kuepuka kufanya mambo machafu na maovu.

Ukweli ni kwamba, kinachoupa nguvu na kuupandisha daraja Uislamu kutoka kuwa nadharia hadi utekelezaji, ni hoja ya kuwapo kwa tabia njema na kufuata mifano elekevu kutoka kwa waja wema waliotangulia. Mahujaji nao, kwa upande wao, wanaweza kuwa kielelezo na mfano wa kuigwa na jamii kutokana na kudhihirisha kwao dhana ya uchamungu na tabia njema wakati wote wa ibada ya Hijja.

Na hii ndio ilikuwa sera na malengo ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) pamoja na Maswahaba zake (Allah awaridhie) hadi wakaweza kusimamisha dini katika maisha yao binafsi na jamii kwa ujumla. Muhimu kwetu, ni kuandaa mipango maridhawa ya kuutekeleza Uislamu kivitendo. Tukifanya hivyo tutakuwa tumetekeleza sehemu ya majukumu yetu ya kila siku.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close