3. Kimatiafa

Virusi vya Corona, janga la dunia!

Mlipuko wa virusi hatari vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu umeendelea kuikamata China. Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo tayari limevitangaza virusi hivyo vilivyopewa jina la muda la ‘2019nCov’ kuwa dharura ya afya duniani. Mpaka muda huu, virusi hivyo vimeshasambaa majimbo yote ya nchini China.

Vikiaminika kuanzia katika jiji la Wuhan kwenye Jimbo la Hubei, Virusi vya Corona vimeambukiza zaidi ya watu 2000 na kusababisha vifo 56, mpaka Januari 26 mwaka huu. Lakini mpaka wiki iliyopita wakati makala hii ikiandikwa tayari watu zaidi ya 300 wameshapoteza maisha nchini China na wengine zaidi ya 10,000 wakiwa wameambukizwa.

Inadhaniwa kwamba, virusi hivyo vimetoka kwa samaki wa Wuhan na wanyamapori kama popo ambao supu yake inaliwa sana katika jijini humo, ingawa chanzo hasa na sababu za kuwepo virusi hivyo bado havijathibitishwa.

Meya wa Wuhan, Zhou Xianwang amewaambia waandishi wa habari kwamba anatararajia maambukizi mengine mapya zaidi ya 1000 katika jiji hilo ndani ya siku chache zijazo. Meya huyo amesema, jiji la Wuhan limeongeza jitihada zake kubwa za kujenga hospitali maalumu za kukabiliana na wimbi la idadi kubwa ya wagonjwa.

Mlipuko huo wa Virusi vya Corona umewashtua maafisa wa Serikali ya China ambao wameweka zuio la nchi nzima la kuuza wanyamapori. Vikwazo vikali vya kusafiri vimewekwa ndani ya China na nje, ikiwa ni jaribio la kudhibiti kusambaa zaidi kwa virusi hivyo hatari.

Hata hivyo jitihada za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo zimeonekana kushindwa.

Wataalamu wameshathibitisha kwamba, virusi hivi vipya vinaambukiza vikiwa katika hatua ya kabla ya kupevuka (incubation period), ambapo binadamu anaweza kuvibeba na asionyeshe dalili zozote. Muda wa kupevuka wa kirusi cha ‘2019-nCov’ unakadiriwa kufika mpaka siku 14.

Bila ya kuonyesha dalili zozote, mtu aliyebeba virusi hivyo anaweza asifahamu kuwa ameambukizwa mpaka kipindi cha wiki mbili, lakini bado akaweza kusambaza virusi hivyo kwa mtu mwingine.

Ukweli huo unafanya shughuli ya kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo kuwa ngumu mno. Waziri wa Tume ya Taifa ya China Ma Xiaowei alinukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Uwezo wa virusi hizi kusambaa unaonekana kuzidi kuwa mkubwa.”

Kwa mujibu wa wataalamu, kirusi hiki ni aina mpya ndani ya familia ya virusi vya Corona, ambavyo kwa kawaida athari zake huwa zinaishia zaidi kwa wanyama kuliko binadamu. Lakini aina hii ya virusi imekuwa na athari kubwa zaidi kwa binadamu na binadamu wanaweza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe kwa kasi ya ajabu.

Familia ya aina hii ya virusi inajumuisha virusi hatari vinavyosababisha matatizo kwenye mfumo wa kupumua vinavyojulikana kama ‘Acute Respiratory Syndrome’ (SARS) na ‘Middle Eastern Respiratory Syndrom’ (MERS), ambavyo vyote vimesababisha vifo, hasa mwaka 2003 wakati mlipuko mkubwa wa SARS ulivyosababisha vifo vya watu 774.

Ni muhimu pia kutambua kwamba watu waliokuwa na virusi vya SARS waliweza kuambukiza baada ya dalili kuonekana na hawakuweza kuvisambaza virusi hivi kabla havijapevuka (incubation period).

Virusi hivi vipya vinasababisha maambukizi kwenye mfumo wa kupumua na dalili zake ni kikohozi kikavu na homa, ambapo baadaye inaingia kwenye hatua ya kushindwa kupumua na maumivu ya kifua. Katika hali mbaya zaidi, virusi hivi vinaweza kusababisha ‘pneumonia’, figo kufeli na hatimaye kifo. Hakuna chanjo wala tiba inayojulikana mpaka sasa.

Nchi kadhaa duniani zimechukua hatua mbalimbali za tahadhari katika kukabiliana na virusi hivi hatari ambapo vifaa maalumu vya kuwatambua watu walioambukizwa vimewekwa kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa. Baadhi ya mataifa pia yamewaondoa raia wao waliopo nchini China.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bwana Kassim Majaliwa, pia aliwataka wanafunzi wa Tanzania wanaosoma China, na ambao hivi wako nyumbani kwa likizo, kutorejea nchini humo mpaka pale Serikali itakapowatangazia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, tayari virusi hivyo hatari vya Corona vimeshaanza kuingia kwenye nchi nyingine ambapo watu watatu wamethibitishwa kuambukizwa nchini Ufaransa, Marekani na mmoja Canada. Katika ngazi ya kikanda, virusi hivyo vya ‘2019-nCov ‘ vimeshaingia Korea Kusini, Japan, Taiwan, Vietnam, Singapore, Malaysia, Thailand na Nepal.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close