1. Habari1. TIF News3. Kimatiafa

Tamko la Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF) kuhusu mashambulizi ya kigaidi ya New Zealand

Assalaam alaykum
Uongozi wa taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) tumepokea kwa masikitiko taarifa za tukio la mashambulizi ya kigaidi lililofanyika katika misikiti miwili mjini Christ Church, New Zealand Ijumaa Machi 15, 2019, ambapo maisha ya Waumini Waislamu 50 wasiokuwa na hatiya yalikatishwa na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa.

Kufuatia mashambulizi haya, kwanza tunapenda kuungana na wapenda amani wote duniani kutoa pole kwa wafiwa na kuwaomba wawe na moyo wa subira na kukubali maneno ya Allah: “Na wala haikuwa kwa nafsi yoyote iwe ya kufa isipokuwa kwa idhini ya Allah, ni amri iliyokewa muda maalumu.” (Qur’an 3:145).

Pili tunawaombea kwa Allah wale waliojeruhiwa katika shambulio hili la kinyama la kigaidi dhidi ya Waislamu wapone haraka majeraha yao na waungane na familia zao wakiwa na imani madhubuti zaidi ya kumuabudu Allah.

Aidha tunapenda kuwaomba Waislamu wote walitafakari tukio hili kwa jicho la imani kwamba hawatokuwa Waumini pasina kufikwa na mitihani na masaibu mbalimbali kama haya na kila tukio kama hili linapotufika tuseme kama alivyosema Mtume Muhammad: “Kamwe haliwezi kutufika isipokuwa lile alilotuandikia Mola wetu, yeye ndiye Mlinzi wetu na kwa Allah waumini wategemeze mambo yao. (Qur’an 9:51).

Kwa hiyo, tusiwe watu wa kuhamaki kwa hasira na jazba bali turejeshe ubaya tunaofanyiwa kwa wema ili kuuonesha ulimwengu kwamba Uislamu ni dini ya amani na ya watu wenye kuutakia ulimwengu kheri na utulivu.Aidha, siyo kila jambo linalotuchukiza ni baya kwetu bali linaweza kuwa la kheri kubwa. Katika tukio hili wale wasio Waislamu watavutika kutaka kuujua Uislamu na wengine tumeshasikia wameanza kusilimu.

Tunamuomba Allah asitupe mitihani mizito zaidi ya uwezo wetu na pindi mitihani inapotufika basi atumiminie subra na azithibitishe nyayo zetu na nyoyo zetu kwa kuzidi imani na kumtegemea Allah

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close