1. Habari3. Kimatiafa

Museveni atangaza vita dhidi ya Kamari

Picha na HakiPensheni

Katika jitihada za kuondoa michezo ya kamari nchini Uganda, Rais wa nchi hiyo Yoweri Museveni ameamuru kutotolewa tena kwa leseni za michezo hiyo kwa makampuni mapya na wala kutohuishwa kwa leseni za makampuni yanayoendesha biashara hiyo kwa sasa, linaandika gazeti la The East African.

Gazeti hilo limemnukuu Waziri wa Fedha nchini humo, David Bahati, ambaye amesema Rais Museveni amechukua hatua hiyo kwa sababu vijana hawafanya kazi na badala yake wamekimbilia michezo ya kamari.

“Tumepokea agizo kutoka kwa Rais Museveni kusitisha leseni za michezo yote ya kamari. Kwa sasa Rais ameigiza bodi inayoshughulikia michezo hiyo kutosajili kampuni mpya na zile ambazo kwa sasa zinaendesha michezo hiyo kutopewa tena leseni,” alisema Bahati wakati akiongea katika moja ya kanisa nchini humo.


Michezo ya kamari kwa sasa imeshamiri hapa Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania ambako watu wengi wameelekeza nguvu zao huko huku sauti zikipaazwa kukabiliana na hali hiyo.

Hapa nchini Mbunge wa jimbo la Ulanga mkoani Morogoro, Goodluck Mlinga (CCM) aliwahi kukemea kamari bungeni wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango mwaka jana. Katika mchango wake, Mlinga aliita kamari kuwa ni ‘janga la taifa.’ Mlinga alitaja madhara ya michezo hiyo kuwa ni pamoja na kudhoofisha nguvu kazi ya taifa kwa kuwa watu wengi hivi sasa hawajishughulisha na uzalishaji mali badala yake wamekimbilia kwenye kamari.

“Zamani ilikuwa ukienda vijijini unakuta vijana wanacheza kamari kwa Pool table. Sasa hivi, pool table haipo, lakini vijana wote wapo kwenye betting (kucheza kamari). Kwa hiyo, nguvu kazi imepotea. Vijana wote wanaamini watakuwa matajiri (kupitia Kamari),” alisema Mlinga.

Mlinga aliongeza: “Mtu yeyote anayecheza kamari hawezi kuacha. Na hao (wachezeshaji) walivyokuwa wataalamu wanakupa kaelfu tano leo umeshinda, ukishinda elfu tano hiyo huwezi kuacha.” Naye Dkt. Bashiru Ally ambaye kwa sasa
ni Katibu Mkuu wa CCM, aliwahi kusema, taifa linapaswa kuchukua hatua kwani kamari zinaviza nguvu kazi za uzalishaji mali.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close