3. Kimatiafa

Hijja ya kipekee

1000 washiriki, hakuna wazee, ulinzi mkali

Hijja ya mwaka huu, 1441 mwaka wa Kiislamu inayotarajiwa kuanza Jumatano, Julai 29, itakuwa ni ya kipekee ambapo ni watu 1,000 pekee watashiriki, ingawa baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti huenda idadi ikaongezeka hadi 10,000.

Milioni 2.5 ndio wastani wa idadi ya watu ambao kwa kawaida hushiriki ibada hii kila mwaka katika Mji Mtakatifu wa Makka, kwa mujibu wa takwimu za miaka ya karibuni zilizotolewa na mamlaka za Saudi Arabia.

Ushiriki huo mdogo wa watu watu 1000 (au zaidi kidogo), raia wa mataifa tofauti lakini wote wakiwa ni wakazi wa Saudi Arabia imetokana na janga la corona lililoitikisa dunia kuanzia mwishoni mwa mwaka jana. Ni uamuzi uliosikitisha Waislamu wengi waliotarajia kwenda Makka mwaka huu lakini wengi pia wameukubali kwa kuelewa ukubwa na hatari ya ugonjwa wa corona ambao mpaka sasa umeua zaidi ya watu laki sita duniani kote.

Uamuzi wa zuio la mahujaji kutoka nje ya nchi hiyo unatajwa kuwa ni wa kwanza wa aina hiyo katika historia ya miaka ya karibuni ya ufalme huo.

Imetajwa kuwa, katika hao 1000 walioteuliwa wamejumuishwa wataalamu katika sekta ya afya na walinzi ambao walishaugua corona na kupona. Pia, hakuna mtu mwenye umri zaidi ya miaka 65 ataruhusiwa kushiriki ibada hiyo. Vilevile, wale wenye maradhi ya makubwa ya kudumu – kama presha, sukari, moyo pia hawatahusishwa.

Kwa mujibu wa mtandao wa ArabNews umenukuu taarifa ya Wizara ya Hijja na Umra, mahujaji hao waliochaguliwa kutoka katika mataifa 160 tofauti, walianza ‘karantini’ ya siku saba siku ya Jumapili iliyopita Julai 19. Karantini hiyo itaisha kesho Julai 25. Katika kipindi hiki, mahujaji hao pia wamepimwa corona. Uangalizi wa mahujaji hao Makka na watawekwa chini ya uangalizi wa siku baada ya ibada hiyo tukufu, ambayo ni nguzo ha tano katika Uislamu kwa wenye uwezo wa kulipia gharama.

Uamuzi wa Mamlaka za Saudi Arabia kuruhusu watu wachache kuhiji ulitangazwa mwezi uliopita katika kipindi ambacho taifa hilo limekuwa likipambana na athari za kisiasa na kiuchumi za janga la corona. Katika nchi hiyo, zaidi ya watu 250,000 walipata maambukizi, na watu zaidi ya 2,500 kufariki.

Saudi Arabia ni nchi iliyoathirika zaidi katika mataifa ya Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi linalojumuisha nchi za Bahrain, Kuwait, Iraq, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Zuio la Hijja, pamoja na Umra vinatajwa kuwa na athari kubwa kiuchumi kwa sababu wageni wanaoingia nchini humo kutekeleza zote au moja ya ibada hizo mbili huliingizia taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta kiasi cha dola bilioni12 kila mwaka.

Ulinzi mkali

Taarifa zaidi kuhusu Hijja ya mwaka huu zinaonesha kuwa maafisa wa nchi hiyo wamejipanga kuimarisha ulinzi ili kuzuia madereva wakora wanapeleka mahujaji wasio halali.

Kwa mujibu wa Meja Generali Khaled bin Fahhad Al Juaid, Kamanda wa Polisi wa Hijja na Hati za kusafiria, dereva yoyote atakayekamatwa akiingiza mahujaji wasioidhinishwa anaweza kufungwa hadi siku 15 jela, kutozwa faini ya riyali 10,000 kwa kila hujaji aliyembeba. Kama hiyo haitoshi, dereva atakayerudia makosa atafungwa mpaka miezi sita na kutozwa faini ya hadi riyali 50,000 kwa kila hujaji aliyeingizwa bila kibali.

Kwa dereva ambaye si raia, atahudumia adhabu zote hizo na kisha atatimuliwa nchini humo na kuzuiwa asiingie tena. Pia, gari iliyotumika itataifishwa.

Adhabu kali pia zimepangwa kwa mahujaji wasioidhinishwa, ambapo kwa mujibu Afisa mmoja katika Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kwamba yoyote atakayekamatwa bila kibali Mina, Muzdalifah au Arafat – maeneo makuu kunaofanyika Hijja atatozwa faini.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa ili mtu aweze kuingia mjini Makka katika kipindi hiki cha Hijja atahitaji ikibali maalumu, na mahujaji watazungukwa na uzio ili kuwalinda.

Tarehe zinaonesha kuwa, Kisimamo cha Arafa ambacho kinatajwa kama kilele cha ibada ya Hijja kitakuwa siku ya Alhamisi Julai 30, huku sikukuu ya Idd yenyewe ikiwa ni Ijumaa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close