3. Kimatiafa

Hijja 2020 itakavyokumbukwa

Ibada ya Hijja mwaka huu wa 2020 imefanyika katika hali tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma ambapo watu takribani 10,000 ndio ambao wametekeleza ibada hiyo, tena wale waishio nchini Saudi Arabia.

Kwa kawaida ibada ya Hijja hukusanya mamilioni ya Waislamu kutoka sehemu mbalimbali duniani bila kujali rangi zao, hali zao kiuchumi, nafasi za kimadaraka, lugha na tamaduni zao.

Mathalan, Hijja ya mwaka jana (2019) iliwakusanya Waislamu takribani milioni 2.5 kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni. Lakini ibada ya Hijja mwaka huu imekuwa tofauti sana. Hali hiyo inatokana na mlipuko wa kirusi cha korona (Covid-19) uliyotikisa dunia nzima.

Utaratibu mpya wa Ibada

Tofauti hiyo inatokana na utaratibu wa mwaka huu ambapo serikali ya Saudi Arabia iliruhusu mahujaji wachache takribani 10,000 waishio nchini Saudi Arabia kushiriki ibada hiyo.

Mahujaji wa Kimataifa hawakuweza kuhudhuria kutokana na zuio lililowekwa na mamlaka ya Saudi Arabia kama njia ya kupambana na ugonjwa wa kirusi cha korona.

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa kwa sehemu kubwa na ugonjwa wa korona ambapo watu takribani 270,000 wameathiriwa.

Hivyo watu wengi duniani na hapa nchini wameshindwa kutimiza azma hiyo mwaka huu, licha ya kwamba walikuwa wameshaweka fedha na wengine kujiandikisha.

Aidha katika Hijja ya mwaka huu, mahujaji hawakuruhusiwa kubusu au kugusa Al-Kaba kama ilivyo ada na wamelazimika kukaa umbali wa mita 1.5 kila mmoja.

Vile vile, mahujaji wamelazimika kuvaa mavazi maalumu ya hijja (Ihram) na kutumia mawe maalumu yaliyotakaswa katika kumpiga mawe Iblis (shetani aliyelaaniwa) kwenye viwanja vya Minna.

Uchumi

Pia zuio la ibada ya Hijja limekuwa na athari kubwa kiuchumi kwa watu kadhaa wakiwamo wafanyabiashara wa mifugo kwenda Saudi Arabia.

Kila msimu wa Hijja unapowadia, Saudi Arabia huagiza idadi kubwa ya mifugo kwa ajili ya kuchinja katika ibada hiyo lakini mwaka huu haikufanya hivyo kwa kiasi kikubwa.

Ripoti ya mwaka 2019 ya Sayansi na dawa za mifugo inaonesha kuwa, Saudi Arabia hununua kutoka nje ya nchi hiyo mifugo zaidi ya milioni 3 wakati wa msimu wa hijja.

Mmoja wa wafanyabiashara waliyokumbwa na changamoto hiyo ni Mfanyabiashara wa mifugo, Cabdi Axmed kutoka Somalia. Cabdi anasema:

“Nimezoea kuuza mifugo yangu popote pale ninaposikia kuna soko. Covid-19 imetuathiri sana sisi tuliyozoea kusafirisha mifugo yetu nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Ibada ya Hijja.”

Athari hizo zimeikumba pia Saudi Arabia kiuchumi ambapo takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka mahujaji huchangia dola bilioni 12 katika pato la taifa la nchi hiyo.

“ibada” upande mwingine

Zuio la mahujaji wa kimataifa limewalazimisha Waislamu wengine kutekeleza ibada mbadala ya kutoa fedha zao ili zitumike kusaidia mambo mengine.

Mathalani, Mzee wa miaka 60 aitwaye Shirin Nazirmadova raia wa Tajikistan ameamua kutoa fedha zake alizopanga kwenda hijja mwaka huu kwa hospitali moja nchini humo ili zitumike kupambana na ugonjwa wa covid – 19.

Mzee huyo anasema hana uhakika wa kwenda Hijja mwakani kutokana na mfumo wa nchi yake ambapo mtu anaweza kujiandikisha kwa ajili ya safari ya hijja hivi sasa lakini akakubaliwa baada ya miaka sita.

Hijja ni nguzo ya tano ya Kiislamu inayopaswa kutekelezwa na kila Muislamu mwenye uwezo wa kimali na kiafya. Na kumalizika kwake huambatana na sikukuu ya Idd Al–Adh–ha. Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Waislamu wengi kuzuiliwa kutekeleza ibada ya Hijja. Mnamo katikati ya karne ya 19 (kuanzia mwaka 1837 na 1846) kulitokea mlipuko wa kipindupindu ulioathiri mji wa Makka. Hali hiyo ilisababisha kusitishwa kwa ibada ya Hijja katika kipindi hicho

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close