3. Kimatiafa

Al–Nahyan wa UAE ashika nafasi ya tatu kwa ushawishi

Jenerali Sheikh Mohammed bin Zayed Al-Nahyan, Mrithi wa Kiti cha Ufalme cha Abu Dhabi, ambaye pia ni Naibu Kamanda wa majeshi ya Falme za Kiarabu (UAE) ametajwa katika nafasi ya tatu miongoni mwa Waislamu 500 wenye ushawishi zaidi duniani.

Nahyan ameshika nafasi hiyo kutokana na ushawishi wake duniani, ikiwemo katika nchi za Magharibi, pia kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko UAE na pia misaada ya kibianadamu anayoitoa maeneo mbalimbali.

Al- Nahyan, ambaye ndiye anatarajiwa kuwa mrithi wa kiti cha urais wa taifa la Falme za Kiarabu ni mtoto wa tatu wa marehemu Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan, rais wa kwanza wa UAE aliyepata umaarufu duniani kote na ambaye aliitawala nchi hiyo tangu ilipopata uhuru mwaka 1971 hadi alipofariki 2004. Rais wa sasa wa nchi hiyo Khalifa bin Zayed Al Nahyan, ambaye ni kaka wa Jenerali Sheikh Mohammed.

Katika orodha hiyo inayotolewa kila mwaka nchini Jordan, anayeongoza katika orodha hiyo ni Jaji Sheikh Muhammad Taqi Usmani wa Pakistan anayetajwa kuwa ni mwanazuoni wa Sharia ya Kiislamu na Mambo ya Fedha.

Hata hivyo, kwa nchi za Kiarabu, Al- Nahyan anaongoza akiwabwaga viongozi wengine maarufu kama Mfalme Salman bin Abdul-Aziz Al-Saud wa Saudi Arabia ambaye yuko nafasi ya nne, Mfalme wa Jordan, Abdullah II Ibn Al-Hussein aliyeshika nafasi ya tano na Mfalme Mohammed VI aliyeshika nafasi ya saba.

Nafasi ya sita katika orodha hiyo imeenda kwa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki huku Mwafrika aliye nafasi ya juu zaidi katika orodha hiyo ni Rais Muhammadu Buhari ambaye anashika nafasi ya 17, akimbwaga Mwana Mfalme wa Saudi Arabia Muhammad bin Salman bin Abdul-Aziz Al-Saud aliye katika nafsi ya 25.

Orodha ya Waislamu 500 ni chapisho ambalo limekuwa likitolewa kila mwaka, kuanzia mwaka 2009 liorodhesha Waislamu wenye ushawishi zaidi duniani. Jarida hili linaandaliwa Kituo kiitwacho ‘Royal Islamic Strategic Studies Centre’ chenye makao yake Amman, Jordan.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close