1. Habari2. Taifa

Jamii yahimizwa kushikamana na tabia njema

Jamii ya Kiislamu hapa nchini imehimizwa kushikamana na tabia njema kwani kufanya hivyo kutapelekea watu kuishi kwa amani, upendo na wakishiriki ipasavyo katika ujenzi wa taifa.

Sheikh El Sayed Esmat Sharafuddin aliyasema hayo hivi karibuni katika kongamano la kidini lililoandaliwa na Azhar Sharif, Tawi la Tanzania, ambapo yeye ni mmoja wa walimu. Kongamano hilo lilifanyika katika Chuo cha Upeo cha Kiislamu, kilichopo mtaa wa Mpande Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha mada ‘Tabia njema na athari zake katika kuendeleza hali ya mtu na jamii’ Sheikh Sharafuddin alisema kuwa, ulimwengu wa sasa unakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, hivyo bila ya kuwafunza watu tabia njema umma utazidi kutetereka.

Sheikh Sharafuddin alifahamisha kuwa Uislamu umekuja kuwafunza watu tabia njema na siyo kuchochea mifarakano, uadui, chuki na ugaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo cha Kiislamu cha Kimisri (Azhar Sharif) Tawi la Tanzania, Sheikh Mohamed Hassan Attia aliitaka jamii ya Kiislamu hususan vijana kufuata njia (manhaj) ya ukati na kati na kushikamana kikamilifu na tabia njema.

Sheikh Attia alisema: “Tabia njema ina umuhimu mkubwa kwa jamii ya kiislamu na jamii zote kwa jumla kwani tabia njema ni msingi muhimu wa mafanikio na maendeleo.”

Kongamano hilo lililohudhuriwa na watu takriban 300, lilishereheshwa na Dkt. Alaa Salah, Muhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar Sharif, Sheikh Killo Nkullo, Meneja wa Chuo cha Upeo cha Kiislamu na Sheikh Hassan Malinga, Mwalimu wa Chuo cha Upeo cha Kiislamu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close