2. Deen8. Wema Waliotangulia

Nendeni mkatekeleze ahadi yenu

Badri ni jina la mji ulio kiasi cha kilomita mia moja na hamsini kutoka mji wa Mtume wa Allah (Madina). Mahali hapo hapakuwa na kitu chochote isipokuwa bonde tu na kisima kilichokuwa miliki ya mtu mmoja aitwae Badri, na kwa ajili hiyo mahala hapo pakaitwa ‘Badri’. Umaarufu wa jina hili (Badri) ulitokana na eneo hilo kupiganwa vita baina ya Waislamu na makafiri na ndipo watu wakaviita vita vya Badri.

Vita vya Badri vinajulikana kama vita vya kwanza katika Uislamu chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie). Pamoja na uchache wao, Waislamu walipambana vikali na kufanikiwa kuwashinda maadui zao kutoka jamii za Wayahudi, Manaswara, Wanafiki pamoja na Washirikina chini ya uongozi wa Abuu Jahli.

Ushindi wa Waislamu katika vita hii ulivuma na kuacha kishindo kikuu katika pande zote za bara Arabu. Vita vya Badri pia vilileta athari chanya kwa Waislamu wa mji wa Madina ikiwa ni pamoja na kuimarisha na kuboresha nguvu yao.

Mwenyezi Mungu anasema kuhusiana na vita hii: “Na Allah alikunusuruni katika (vita vya) Badr na hali nyinyi mlikuwa dhaifu. Basi mcheni Allah ili mpate kushukuru (kila wakati kwa neema zinazokujieni).” (Qur’ an, 3: 123).

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alifahamu kuwa Makureysh wametoka kwa ajili ya kupambana naye, hivyo akawakusanya Maswahaba zaidi ya mia tatu na kuondoka nao hadi eneo la vita.

Inasemekana Maswahaba walioondoka na Mtume katika vita vya Badri walikuwa 313 au 314, na riwaya nyingine zinasema walikuwa 317. Kati yao 86 ni Muhajirina (Watu waliohamia Madina) na 231 ni Answaar (Wenyeji wa Madina).

Licha ya uchache wa wapiganaji katika jeshi la Waislamu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwakataza Maswahaba wawili, Hudhayfa Ibnul–Yamani na baba yake (Allah awaridhie) kwenda Badri kwa ajili ya kushiriki katika mapigano kwa kuwa tayari walikwishaweka ahadi na Makureysh.

Ahadi ya Hudhaifa na baba yake kwa Makureish Alipoulizwa ni kwani hakwenda vitani, Hudhayfa Ibnul–Yamani alijibu: “Hakuna kilichonizuia kushiriki vita vya Badri isipokuwa ni kwa sababu mimi na baba yangu tulimuendea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) lakini Makureysh walitukamata na kutuambia, “Nyinyi mnakusudia kwenda kwa Muhammad.”

Tukasema: “Hatukusudii (lolote) isipokuwa kuelekea Madina, wala hatutapigana pamoja naye, Makureysh wakachukua ahadi ya Allah kwetu na tukakubaliana nao kwamba tutaelekea Madina. Kisha tukamuendea Mtume wa Allah (rehema na amani ya Allah imshukie) ili kumueleza yaliyotokea.” Mtume akatuambia: “Nendeni, tuwatekelezee ahadi yao na tumuombe Allah atusaidie dhidi yao,” (Muslim). Msimamo huu unatoa taswira ya malezi ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa Maswahaba zake (Allah awaridhie) na msisitizo juu ya umuhimu wa kutekeleza ahadi.

Ingawa inajuzu kutumia lugha ya mafumbo wakati wa vita lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) hakutumia mwanya huo kuwarubuni maadui bali aliipa uzito wa juu ahadi aliyoiweka Hudhayfa na baba yake kwa Makureysh.

Hudhayfa na Baba yake walimuendea Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) ili awaruhusu kushiriki jihadi lakini Mtume aliwakataza ili kutekeleza ahadi na makubaliano yao na Makureysh. Licha ya jitihada kubwa walizozifanya kuhakikisha wanamuangamiza Mtume na Maswahaba zake, Wayahudi na Washirikina walitambua uzuri wa tabia ya Mtume Muhammad.

Wakasema: “Ikiwa mafundisho ya Uislamu yanamtaka mja awe mkweli na mwaminifu hata kwa maadui zake, itakuwaje ahadi ambayo ameichukua kwa Waislamu wenzake?” Hiraql, aliyekuwa kiongozi wa Warumi aliposikia habari ya kuwapo mtu anayejinadi kuwa Mjumbe wa Allah, alifika katika mji wa Makka kwa ajili ya shughuli za kibiashara. Huko alikutana na Abu Sufiyani, akamuuliza, “Je, Muhammad hufanya khiyana (kuvunja ahadi)? Akasema: “Hapana,” Hiraql akasema, “Ndivyo hivyo, Mitume huwa hawavunji ahadi,” (Bukhari).

Hiraql alitaka kujua ukweli wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), hivyo akamuahidi jambo na mwishowe ikathibitika kuwa Muhammad hakuwa mtu mwenye khiyana katika ahadi zake. Huu ni mfano mmoja tu kwenye muktadha wa kutekeleza ahadi, tabia ambayo Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) ameionesha katika vita vya Badri.

Licha ya kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa wapiganaji na vifaa kwenye viwanja vya vita, Mtume hakuwafanyia khiyana maadui aliokuwa akipigana nao.

Kutotekeleza ahadi ni sifa ya wanafiki

Kukhalifu au kutotimiza ahadi ni katika jumla ya alama za unafiki wa mtu. Kwa kuchelea hilo, Uislamu umetuamuru kutekeleza ahadi katika hali zote bila kujali rangi, kabila au dini ya mtu. Allah Azza Wajallah’ anatuambia: “Na timizeni ahadi; hakika ahadi itaulizwa (siku ya kiyama),” (Qur’ an, 17: 34).

Na katika Hadithi iliyosimuliwa na Abi Hureira (Allah amuwie radhi), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mtu yeyote akiwa na mambo manne atakuwa mnafiki hasa (kamili), na kama atakuwa na moja katika hayo manne atakuwa na sifa ya unafiki mpaka aliache. Akiaminiwa hufanya hiyana; na akizungumza anaongopa; na apotoa ahadi huvunja na anapogombana anaiacha haki na kuwa jeuri.” (Bukhari na Muslim).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close