8. Wema Waliotangulia

MAISHA YA HINDU BINT UTBAH, MKE WA ABUU SUFIANI

K ama ilivyo kawaida, kutoka katika maisha ya wema waliotangulia ambao visa vyao tunavisimulia hapa tunajifunza humo mambo mengi ya kutunufaisha. Katika maisha ya Hindu bint Utba (radhi za Allah zimshukie) Waislamu wana mengi ya kujifunza. Miongoni mwa hayo, kubwa zaidi ni kuwa kisa hiki kimethibitisha ukweli wa maneno ya Mtume (rehema na amani zimshukie) aliposema “Nyoyo za waja zimo katikati ya vidole viwili (mkononi mwa) Alah Ta’ala, huzigeuza apendavo.” Naam, baada ya chuki, kiburi, uadui na vitimbi alivyovifanya Hindu pamoja na mumewe dhidi ya Uislamu na Waislamu, haikudhaniwa kwamba ingelifika siku wakafanya maamuzi mazito ya kubadili dini na kuufuata Uislamu. Tujifunze pia sifa ya uvumilivu katika ulinganiaji na kutomkatia tamaa mtu kwa vile ni mchafu wa matendo, kwani wajibu wa mlinganiaji ni kufikisha ujumbe tu, na Allah ndiye muongozaji. Mtume aliamiliana na watu hawa (wakwe zake) kwa namna walivyokuwa tena kwa kipindi kirefu, huku akiwa na matumaini kwamba mwisho wa siku watauona ukweli na watamfuata. Mtume katika harakati za kuwalingania alikuwa na pupa ya hali ya juu ya kuwaita watu wake kwenye haki, lakini hakuwa na papara. Katika maisha ya Hindu vile vile, tunajifunza jinsi makafiri wanavyopanga njama na kufanya juhudi za mchana na usiku kuujadili Uislamu na Waislamu. Makafiri hutumia, elimu, fedha na muda mwingi katika kupanga mikakati ya kuwadhuru Waislamu na dini yao. Makureishi walikubali kuisabilia (kuitoa) mali yao iliyosalimika kushikwa na Waislamu katika heka heka za kuviziwa msafara wa kibiashara ulipokuwa ukirudi kwao kutoka Sham, kwa ajili ya kujiandaa na vita vingine (vya Uhud). Kwa ujumla, Waislamu duniani hawako salama sana na njama za maadui zao. Hili liko wazi katika kauli ya Allah “… wanatamani yakufikeni ya kukusumbueni, zimeshadhihiri chuki midomoni mwao na yaliyofichwa na vifua vyao (dhidi yenu) ni makubwa zaidi” (Qur’an, 4:118). Tumeona pia jinsi Makureishi walivyoumiza vichwa vyao siku kadhaa katika kupanga mkakati wa kumuua Hamza katika vita vya Uhud. Mwanamke ni kiungo muhimu sana wanachokitumia makafiri katika kufanikisha mipango yao ya kuudhuru Uislamu. Tumeona jinsi Wahshiy (aliyemuua Hamza) denda lilivyokuwa likimtoka (kwa kutamani) alivyokuwa akiahidiwa na Hindu mapambo yaliyokuwa yakimzidishia uzuri na haiba yake kwamba siku moja ataburudisha macho yake anapoyaangalia kwenye shingo ya mkewe. Wakati huo huo Wahshiy alishaahidiwa kuachwa huru na bwana wake Mut-im bin Adii, iwapo atafanikiwa kumuua Hamza. Ukweli ni kwamba, kuna matokeo kadhaa ya uharamia, ujambazi na mengine ya kuhatarisha uhai wa mwanadamu ambayo hufanikishwa kwa msaada mkubwa wa mwanamke, kama ambavyo dunia inashuhudia hivi leo. Tunaweza kusema kwamba, sehemu kubwa ya ushindi wa Makureishi siku ya Uhud ilichangiwa na wanawake -wakiongozwa na Hindu- waliokuwa wakishangilia na kuwaahidi wanaume wao wapiganaji yale wayapendayo. Hadithi zilizokuja katika vitabu mbali mbali, Mtume akizungumza, kuwafundisha na kuwaasa wanawake, ukichanganya na khutba yake kwa wanawake wa Kikureishi (bai-a) baada ya kuiteka Makka, ambapo Hindu alikuwa miongoni mwao, inatuthibitishia kuwa yafaa kuwasomesha akina mama wa Kiislamu mambo ya dini yao kwa mtindo wa darsa au muhadhara kwa ajili yao tu, kinyume na walivyofahamu baadhi ya ndugu zetu ‘matwalibul-ilmi’, kwamba hilo si katika mwenendo wa Mtume na kwa hiyo ni bid-a (uzushi). Tumeona jinsi khutba yake Mtume ilivyokuwa ikikatishwa na mwanamke (Hindu) mpaka Mtume akauliza: “Wewe ni Hindu au nani?!” Naye akamjibu: “Ndiyo, nipo hapa na naomba usamehe yaliyopita.” Katika darasa hiyo, Hindu alitaka Mtume amuweke wazi kuhusu mazoea yake ya kuchukuwa sehemu ya mali ya Abuu Sufiani bila ya idhini yake, kwa vile alikuwa hampi matumizi ya kumtosha, naye akamjibu, tena katikati ya darasa. La kujifunza hapa ni kwamba, wanawake wakati wa Mtume walifanyiwa darasa maalumu kwa ajili yao na walipata fursa ya kuuliza m a s w a l i m b a l i mbali yaliyohitaji u f a f a n u z i , n a mwalimu wao (Mtume) aliwajibika kwa hilo. Ubakhili ni t a b i a mbaya isiyokubalika kwa watu wote, lakini pia ni katika tabia wanazozichukia sana wanawake na wasizoweza kuzivumilia kuziona kwa waume zao. Angalia namna Hindu alivyomshitaki Abuu Sufiani kwa Mtume katika siku ya kwanza kukutana naye akiwa Muislamu, tena mbele ya kadamnasi (hadharani). Ukitaka wanawake wakuseme sana, wakudharau na kukunyooshea vidole, jifanye bakhili. Yaani kitu unacho lakini hukitumii kwa mahitaji ya lazima ya nyumbani. Katika Uislamu, israfu imekatazwa lakini na ubakhili pia ni haramu (Qur’an, 25:67) F u n z o j i n g i n e n i kwamba, imani ni jambo kubwa na zito kabisa. Mara nyingi kub a d i l i imani huambatana na vishindo, misukosuko na kusitasita. Inakuwa sawa na kumuachisha mtoto maziwa ya mama yake, wakati ameshayazoea. Hili lipo katika safari ya Bibi Hindu na mumewe kuuelekea Uislamu. Angalia jinsi alivyomshika ndevu mumewe kwa hasira na kumtikisa akimwambia: “Kwanini hamumuui mzushi huyu?” Ilikuwa ni siku ambayo hofu na simanzi vilitanda kwenye viunga vya Makka wakati Mtume na Maswahaba wake wanaingia kuiteka. Tunajifunza hili pia kwenye mjadala wa Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) na Abuu Sufiani. Mtume alimuuliza: “Hivi haujafika wakati wewe kukubali kuwa mimi ni Mtume wa Allah?” Abuu Sufian alijibu kwamba hilo bado ana mashaka nalo, Abbas akamsogeza kwenye imani na kumshauri atamke Shahada. Haikutosha hapo, bali Abbas (radhi za Allah zimshukie) alimuomba Mtume ampe Abaa Sufian kijiwadhifa angalau ajisikie kwa anavomfahamu rafiki yake alivyoupenda ukubwa. Yote hayo yalifanyika ili kusaidia mabadiliko ya kiimani ya Abuu Sufiani kuelekea Uislamu. Ni jambo zito kwa kweli. Na ndiyo maana Uislamu ukaweka fungu maalumu la zaka kwa wanaoingia sasa au wanaotarajiwa kuingia katika Uislamu. Lengo ni kuzilainisha nyoyo zao ziukubali Uislamu. Jambo jingine na muhimu la kujifunza ni kuisafisha imani na takataka za ushirikina. Hindu alilielewa hili vya kutosha. Aliamini kuwa itikadi sahihi ndiyo neema kubwa zaidi aliyowahi kuipata mwanadamu hapa duniani. Alielewa pia kuwa, imani na ushirikina havikai pamoja, vimbalimbali kama ‘bainalmashrikq wal-maghribi’, na ndiyo maana baada ya kusilimu alikwenda kwa sanamu lake aliloligharamia kabla, kulitunza na kuliheshimu na akalichanja bila ya hofu kwa shoka, huku akilisimanga. Muislamu, ikiwa anamuamini Allah Aliyetukuka hapaswi kuwa na waungu wengine kama vile mizimu, makaburi makongwe, mashetani akawa anawaabudu, anajitisha mbele yao na kuwanyenyekea. Maisha ya Hindu bila shaka ni somo linalotoa ujumbe mzito juu ya mabadiliko ya kiimani na wajibu wa mtu kushikamana sawasawa na itikadi sahihi ambayo ndiyo msingi wa matendo ya mja. Wabillah tawfiq.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close