8. Wema Waliotangulia

Kumbukumbu yangu isiyofutika ya Sheikh Suleiman Amran Kilemile (Allah amrehemu)

Mwaka 1995 nilijiunga na kitivo cha biashara (B.Com) cha Chuo Kikuu cha Dares Salaam, nikiwa nimeitwa katika mkupuo wa pili wa wasailiwa (second selection).

Kwa kawaida, ningetakiwa nijiunge na chuo mwaka 1996, lakini nilikurupushwa mtaani pale mmoja wa wahisani wangu aliposikia jina langu likitajwa redioni miongoni mwa wanaotakiwa kuripoti chuoni mara moja. Haraka, nilidandia lori kutoka kwetu Lindi kuelekea Dares Salaam. Siku ya tano yake niliripoti chuoni.

Sikujuwa kuwa miongoni mwa mambo vitu aliyonikadiria Mwenyezi Mungu kwa kuitwa kwangu chuoni mapema ilikuwa ni kupata kumbukumbu isiyofutika ya Sheikh Suleiman Amran Kilemile.

Sikubahatika kupata chumba cha kuishi katika hosteli za chuo, hivyo niliwekwa kwapani na ndugu yangu Abdallah Kipalanga. Kipalangaalikuwa akiishi chumba kimoja na kijana msomi, mstaarabu na mtaratibu aitwaye John Mduma aliyekuwa akisoma Shahada ya Uchumi akiwa mwaka wa pili kwa wakati huo.

Mduma alikuwa mpenzi wa elimu na mdadisi, tabia iliyompelekea kutokuwa na woga wa kujifunza imani za dini za watu wengine.Hivyo,kila Ijumaa alipenda kusikiliza kipindi cha mawaidha ya Kiislamu kupitia Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD)kilichokuwa kikiongozwa na Sheikh Suleiman Gorogosi (Allah amrehemu). Udadisi wake huo ndiyo ulionizalishia kumbukumbu ya kudumu kuhusu Sheikh Suleiman Kilemile.

Ijumaa moja, tulikuwa tumeketi chumbani,kaka yangu Kipalanga wakati anakaanga dagaa (kauzu) ili tulie ugali, kaka Muhammad Mbiku akisisitiza nguna iwe kubwa ya kutosha, kijana John Mduma kama desturi yake alikuwa amejilaza juu ya kitanda cha dabodeka akiwa na redio pembeni yake anasikiliza.

Mara sauti ya Sheikh Suleiman Gorogosi ikaibuka: “Assalaamu aleikum warahmatullah. Mgeni wetu kwa siku ya leo ni Sheikh Suleiman Amran Kilemile.”

Allahu Akbar! Baada ya salamu na utangulizi, Sheikh alidokeza mada ya siku ile:‘Demokrasia kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.’ Akasema, kwa kuwa ule ulikuwa ni mwaka wa uchaguzi wa kidemokrasia (1995)unaohusisha vyama vingi vya kisiasa,kulikuwa na umuhimu wa kuizungumzia demokrasia kwa mujibu wa Uislamu ili wananchi wapate muongozo kuhusu jambo hilo. Kichwa cha habari pekee kilitusisimua kutaka kujua zaidi, ingawa kwa mwenzetu Mduma hamu yake ilikuwa maradufu kwani mada husika ilikuwa ni ngeni kabisa kwake.

Sheikh aliidadavua demokrasia kwa umakini wa hali ya juu kwa mtazamo wa kisekula kwanza, kisha, akaja kufanya ulinganisho wa misingi na malengo ya demokrasia kwa mujibu wa falsafa yadini ya Kiislamu.

Ulikuwa ni udadavuzi uliojaa si tu umbuji wa kuongea na umahiri katika lugha ya Kiswahili na Kiarabu, bali pia ufundi wa kitaaluma wa hali ya juu ulioambatana na ushahidi wa kimatukio na rejea za kisomi za kueleweka na kuaminika.

Sheikh Kilemile alipomaliza kuwasilisha mada yake, tulibaki tukitafakari kwa muda kisha John Mduma, mwanafunzi mwenzetu, Mkristo, alituuliza swali: “Huyu sheikh ni profesa anayefundisha wapi? Au ni mtu mwenye taaluma gani na ya kiasi gani?”

Kabla sijamjibu, nilimuuliza msingi wa swali lake. Je kuna mahali alikosea anataka kumkosoa? Au alipatia sana kiasi cha kustahili kongole? Mduma alikuwa ni miongoni mwa vijana wenye akili sana katika darasa lake, niliwaza, hivyo tahadhari ilihitajika.

Mduma kwa upole na umakini akasema: “Mimi niliisoma topiki ya demokrasia kwenye somo la siasa nikiwa sekondari ya awali na ya juu. Kisha nilisoma pia hapa chuoni kutoka kwa maprofesa bobezi wa somo la siasa chini ya somo la Maendeleo (Development Studies), lakini, nakiri kuwa huyu Sheikh ametumia chini ya saa moja kuielezea vizuri sana demokrasia hii hii niliyosoma mimi kwa miaka kadhaa! Na nimeweza kuielewa zaidi demokrasia  kuliko nilivyosomeshwa huko nyuma!

Huyu ni sheikh ni profesa!?

Mduma pia alimsifu Sheikh Kilemile kwa namna alivyoielezea demokrasia kwa mujibu wa dini ya Uislamu. “Hivi hii dini yenu inazungumzia mpaka demokrasia kwa upana hivyo?” aliuliza kwa mshangao.

Subhaanallah! Mduma aliguswa kweli kweli. Hapo ndipo akina siye tukapata nguvu na kumpa maelezo kidogo kuwa huyu ni sheikh wetu mwenye elimu ya ngazi ya Shahada katika elimu dini. Pia ni muasisi wa taasisi ya elimu itoayo elimu ya sekondari na mafunzo ya dini. Lakini pia, tukapata fursa ya kumfafanulia upana wa dini ya Kiislamu na namna Uislamu unavyogusa nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Kwa kifupi hapo akina siye tukapata, kwa maneno ya Mzee wa Msoga,tulipata fursa ya kujimwambafai tukitumia vijielimu vyetu vya Uislamu vya kuchovyachovya tulivyojaaliwa kuokota mashuleni. Subhanallah

Tukio hili limeacha athari ya kudumu katika maisha yangu na kunipa chachu ya kufuatilia mafunzo ya Sheikh Kilemile kupitia mada zake zilizotapakaa mitandaoni. Sheikh ni katika wanazuoni waliotuachia athari kubwa inayoshikika, inayonusika, inayosikika na inayoonekana!

Kwa wale wote wanaofuatilia mawaidha ya sheikh, watakubaliana na mimi kuwa Sheikh Kilemile siku zote alilenga kutoa mawaidha na mafunzo ya Kiislamu kulingana na halaiki inayolengwa na wakati husika. Wazungu wanasema, ‘delivering lectures that resonate with time and target population.’

Falsafa ya Sheikh Kilemileilikuwa ni kuielimisha jamii juu ya Uislamu, kama mfumo uliokamilika katika kuongoza maisha ya mwanadamu (Islam as a complete way of life).

Nikitafakari kuhusu siku ile, ni wazi kuwa Sheikh alitumia fursavema katika radio ya taifa kuzungumzia demokrasia kwa mtazamo wa Kiislamu kwani uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa ni wa kwanza baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia wa vyama vingi. Hivyo, dhana hiyo ya demokrasia ilikuwa ndiyo stori iliyokamata mitaani ambapo kila mtu alikuwa akijadili na kutafakari athari, matokeo na mustakabali wa mfumo mpya wa kidemokrasia nchini.

Athari aliyoiacha

Vijana wengi hivi leo wamepitia Thaqaafa, shule aliyoiasisi Sheikh Suleiman Amran Kilemile na kuipenda na walinufaika kwa kutokana na usimamizi, maono na miongozo yake ya kimaadili na kielimu.

Kadhalika, kwa waumini wengi tuliobakia Sheikh katuachia hazina kubwa ya elimu iliyotapakaa mitandaoni na itakayoishi kwa miongo,kama si kwa karne nyingi zijazo, chini ya falsafa ya Uislam kama mfumo kamili wa maisha ya binadamu kwa vitendo (in practical sense).  Sheikh ametuachia pengo katika orodha ya masheikh waliokuwa na athari chanya na tija kubwa kwa umma. Yeye hakutosheka na wadhifa na umaarufu, bali alitamani kuleta mapinduzi ya kifikra na kiimani kwa umma wa Kiislamu. Lau umma wetu ungepata akina Kilemile 20 tu; hakika, inshaAllah, tungepiga hatua kubwa kimaendeleo ya kifikra, dini, kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Sheikh atakumbukwa zaidi kwa namna alivyoji-brand, nikitumia maneno ya vijana wa zama hizi. Hakukosea mtu mmoja aliyemuelezea kwa ufupi, kwa lugha ya kigeni:

“Sheikh Amran Kilemile was a mainstream sheikh who appealed to all Muslim community, regardless of their sects.”(Yaani alikubalika na Waislamu wote bila kujali tofauti zao za kimadh’hab au mitazamo).

Jukumu letu kama umma tuliobakia nyuma yake ni kuenzi aliyoasisi na pia kutunza hazina ya kitaaluma aliyotuachia kupitia machapisho na njia nyinginezo za uhifadhi wa turathi za kidini kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

Tunamuomba Allah amjaalie sheikh wetu Suleiman Amran Kilemile kauli thaabit na pepo ya Firdaus. Aamiin Aamiin.

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close