2. Deen8. Wema Waliotangulia

Hijra ni njia ya Mitume na Manabii

Kuhama kwa ajili ya Allah si tukio la kitalii bali ni njia mojawapo ya kuitetea na kuitangaza dini ya Allah na kuihifadhi dini dhidi ya vitimbi na uadui wa wapinzani wa Allah. Mitume na Manabii wa Allah (amani ya Allah iwashukie) waliihama miji yao kutafuta mazingira rafiki ya kulingania dini.

Kama ambavyo mkulima anatafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kuotesha mazao yake, vilevile Mitume walikuwa wakitafuta nyoyo zenye rutuba ili waoteshe punje za Tauhid.

Hijra ni tukio la kihistoria

Tunapozungumzia historia ya Uislamu tunamaanisha historia pana inayogusa ujumbe waliokuja nao Mitume na Manabii wa Allah (amani iwashukie). Ulinganiaji ni kazi ambayo Mitume na Manabii wa Allah (amani iwashukie wote) waliifanya kikamilifu licha ya kukabiliwa na matatizo makubwa na uadui katika kuitekeleza.

Allah Aliyetukuka alisema kumuambia Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie): “Huambiwi ila yale yale waliyoambiwa Mitume kabla yako.” [Qur’an, 41:43]. Maana yake, wahyi (ufunuo) walioteremshiwa Mitume waliotangulia ndiyo ambao umeteremshiwa wewe, na maudhi unayofanyiwa na watu waovu na washirikina ni muendelezo wa yale waliyokumbana nayo Mitume waliokutangulia.

Mitume kufukuzwa katika miji yao

Vitisho na kufukuzwa katika miji ni miongoni mwa madhila waliyokumbana nayo Mitume wa Allah na wafuasi wao. Allah ‘Azza Wajallah’ alipeleka Mitume katika jamii za watu waliobobea katika maovu ya ushirikina, dhuluma, kufuru na kila aina ya madhambi.

Katika Qur’an tunasoma mazungumzo ya aina moja kutoka kwa Mitume wa Allah ‘Azza Wajallah’, ambao katika zama tofauti walitumwa ulimwenguni kuwalingania watu dini ya Allah.

Qur’an Tukufu imenukuu kauli za washirikina ambao mara zote walikuwa wakiwafanyia vitimbi na uadui Mitume wa Allah. Kwa mfano, katika Surat Ibrahim [Qur’an, 14:13], washirikina walimuambia Nabii Ibrahim: “Tutakutoeni katika nchi yetu au mrudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi, ‘Hakika tutawaangamiza waliodhulumu.’” [Qur’an, 14:13].

Nabii Ibrahim (amani ya Allah imshukie) alifanya kazi kubwa ya kumlingania baba yake ili aache kuabudu masanamu, lakini juhudi zake ziligonga mwamba. Baba yake alimuambia: “Unaichukia miungu yangu ewe Ibrahim? Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokee mbali kwa muda!” [Qur’an, 19:46].

Nabii Ibrahim alitumia hoja na dalili za wazi kuwalingania watu wake ibada ya Muabudiwa Mmoja lakini juhudi zake hizo hazikufua dafu. Wakuu na viongozi wa jamii za washirikina hawakuacha kumfanyia vitimbi na uadui kwa lengo la kutetea itikadi zao batili.

Ibrahim aliwaambia: “Hivi mnaviabudu vitu mnavyovichonga wenyewe? Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumbeni nyinyi na hivyo mnavyovifanya! Wakasema, ‘Mjengeeni jengo na kisha mtupeni motoni humo!’ Walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndiyo wa chini.” [Qur’an, 37:96–98].

Baada ya kunusuriwa na Allah, Ibrahim (amani ya Allah imshukie) aliuhama mji wake na kuelekea Sham (Syria), na akasema: “Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa.” [Qur’an, 37:99].

Nabii Lut na watu wake

Baada ya kushuhudia yaliyotokea kwa Ibrahim, Nabii Lut alisadikisha yale yote aliyokuja nayo Ibrahim kisha wote wawili wakahama: “Lut akamuamini, na akasema, ‘Mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye Hekima.’” [Qur’an, 29:26].

Allah alimchagua Nabii Lut kuwa Mjumbe wake kwa watu wa Sodoma. Hata hivyo, kazi haikuwa rahisi kwani watu walimpa majaribu na kumuweka katika madhila ya aina mbalimbali.

Allah anasema: “Na tulimtuma Lut alipowaambia watu wake, ‘Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote! Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio na mnawaacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji!’ Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipokuwa kuambizana, ‘Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanaojitakasa.’” [Qur’an, 7:80–81].

Nabii Shuaib na washirikina wa Madyana

Kadhalika, Allah Aliyetukuka amlimtuma Nabii Shuaib kwa watu wa Madyana kama anavyobainisha: “Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaib. Akasema, ‘Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna Mungu mwingine isipokuwa Yeye. Imekwishakufikieni hoja wazi kutoka kwa Mola Mlezi wenu. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwishatengenea. Hivyo ndivyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini. Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini haya niliyotumwa, na kundi jingine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu. Naye (Mwenyezi Mungu) ndiye Mbora wa wenye kuhukumu.’ Wakasema wakuu walio na kiburi katika kaumu yake, ‘Ewe Shua’ib! Tutakutoa wewe pamoja na wale walio kuamini katika mji wetu au mrejee katika mila yetu.’ Akasema, ‘Je, ingawa tunaichukia (mila yetu)?’” (Qur’an, 7: 85–88).

Hadithi ya Musa na Firauni

Musa alikumbana na changamoto nyingi kutoka kwa Firauni kwa sababu tu alikuwa akiwalingania watu ibada ya Muabudiwa Mmoja na kuwaonya wasifanye mambo machafu na maovu.

Ni kwa sababu hiyo, Allah akamuamuru kuihama nchi ya Misri ili apate wepesi wa kuwalingania Wana wa Israil na kuwakomboa kutoka mikononi mwa Firauni. Allah alisema kumuambia Musa, “Basi nenda na waja wangu usiku. Kwa yakini mtafuatwa. Na iache bahari vivyo hivyo imeachana, hakika wao hao ni jeshi litakalozamishwa.” [Qur’an, 44:23– 24]. Misimamo na mila ya washirikina katika kila zama ni moja na wala haibadiliki. Washirikina walioishi zama za Nabii Muhammad (rehema za Allah amani zimshukie) hawatofautiani na wale waliowatangulia katika umma zilizopita: “Na walipokupangia mpango waliokufuru wakufunge, au wakuue, au wakutoe. Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa mipango.” [Qur’an, 8:30].

Hii inaonesha kuwa kazi yao kubwa ya washirikina na waovu wote katika kila zama ni kupanga mikakati ya kuwadhuru, kuwanyanyasa na kuwateza nguvu watetezi wa haki kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwamo kuwawekea vikwazo ili wasitekeleze wajibu wa kulingania dini au kuwafukuza katika miji.

Hijra ya Mtume (rehema na amani zimshukie) na Maswahaba wake (Allah awaridihie) ni muendelezo wa yale yaliyowasibu Mitume waliotangulia.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close