8. Wema Waliotangulia

Ewe Allah, Nijaalie Niwe Kama Yeye

Kutoka kwa Abu Huraira (Allah amridhie) amesimulia kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mama mmoja kutoka kabila la Banu Israil alikuwa akimnyonyesha mwanawe, mara akapita mtu aliyevaa vizuri na mwenye muonekano wa kuvutia akiwa juu ya mnyama.” Yule mama akasema: “Ewe Allah, mjaalie mwanangu awe kama (mtu) huyu.” Mtoto aliposikia hivyo aliacha kunyonya akamgeukia yule mtu aliyekuwa juu ya mnyama na kusema: “Ewe Allah, usinijaalie kuwa kama mtu huyu,” kisha akaliekea ziwa na kuendelea kunyonya.” Msimulizi wa hadith hii (Abu Huraira – Allah amridhie) anasema alimuona Mtume akiingiza kidole chake cha shahada mdomoni kisha akakinyonya.” Abu Huraira anaendelea kusimulia kwamba, baada ya muda mfupi yule mama na mwanawe walipita eneo moja na kukuta watu wanampiga mtumwa wa kike huku wakimwambia: “Umezini, umeiba.” Yule mtumwa akasema: “Hasbiyallahu wani’mal–wakil (Allah ananinotosha, naye ni mbora wa kutegemewa.” Mama aliposikia maneno hayo alishangaa mno akasema: “Ewe Allah, usimjaalie mwanangu kuwa kama (mtu) huyu.” Kwa mara nyingine mtoto akaacha kunyonya, akamuangalia mama yake kisha akasema: “Ewe Mola, nijaalie niwe kama yeye.” Mama akamuuliza mtoto: “Kwanini unasema hivyo?” Mtoto akajibu: “Yule mtu aliyekuwa amempanda mnyama alikuwa mjeuri na mwenye majivuno hivyo nikasema: ‘Ewe Allah, usinijaalie kuwa kama (mtu) huyu.’ Ama yule mtumwa aliyekuwa akipigwa na watu kwa tuhuma za kuzini na kuiba hakuwa mwizi wala mzinifu hivyo nikasema: ‘Ewe Allah nijaalie niwe kama yeye.’” [Bukhari na Muslim].

Mafunzo ya tukio Katika hadith mbalimbali, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amewataja watoto wengine waliowahi kuzungumza wakiwa wachanga, na miongoni mwa hao ni Isa bin Maryam ambaye habari zake zimezungumzwa kwa kirefu ndani ya Qur’an Tukufu.

Mtoto mwingine ni yule aliyetoa ushahidi juu ya tuhuma za uzinifu zilizokuwa zikimkabili mmoja wa waja wema waliopita aitwae Jureyj. Alipotakiwa kutoa ushahidi juu ya tukio hilo mtoto alijibu kuwa Jureyj si mzinifu na kwamba mwanamke anayetuhumiwa kuzini naye alifanya kitendo hicho kiovu na mmoja wa wachunga mifugo.

Katika tukio hili, tumeshuhudia mwanamke wa kabila la banu Israil akimuomba Mwenyezi Mungu amjaalie mwanawe awe kama kijana aliyemuona amevaa vizuri na mwenye muonekano wa kuvutia akiwa juu ya mnyama. Hii ni kwa sababu, binadamu siku zote hutamani vitu vizuri na vyenye kuvutia.

Mama huyo alitamani mwanawe awe nadhifu na mwenye mvuto mithili ya kijana aliyemuona amempanda mnyama bila kujua tabia za kijana huyo.

Baadaye kidogo mama huyo na mwanawe walipita eneo moja na kukuta watu wanampiga kijakazi wa kike. Mama akasema: “Ewe Allah, usimjaalie mwanangu kuwa kama mtu huyu (anayepigwa).”

Kwa kuwa mwanadamu hapendi udhalili na unyonge mama hakutaka mwanawe awe kama yule kijakazi aliyekuwa anapigwa. Jambo zuri ambalo mama alikuwa halijui ni kwamba kijakazi yule alikuwa mtu mwema, mwenye hadhi na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Usitamani kila unachokiona

Kuna wakati mtu hutamani kufanya mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwake. Mwanamke tuliyemtaja hapo juu alitamani mwanawe awe kama yule kijana aliyekuwa amempanda mnyama bila kujua kama ni muovu, mwenye kiburi na majivuno.

Funzo kubwa tunalolipata hapa ni kwamba mtu hapaswi kuiga jambo ambalo hajui undani wake. Ni vizuri tukaridhika na hali tulizonazo na ikiwa mtu anatamani kuwa kama fulani basi atamani kile chenye maslahi kwake, na kama anamchukia mtu au kitu basi achukie kwa ajili ya Allah.

Masheikh na walinganiaji wanatakiwa wafafanue mambo muhimu ya dini kwa kutumia mifano mbalimbali na dalili katika Qur’an Tukufu na Sunna za Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) ili watu wayalewe vizuri na kuyaweka akilini.

Mtume alitumia njia hii kuwafundisha maswah a b a imani thabiti ya kumjua Allah na Mtume wake. Katika darsa zake mbalimbali, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akizungumzia matukio yaliyowahi kutokea katika zama zilizopita ili mafunzo yake yaeleweke kwa wepesi.

Dalili za kuwepo Allah

Kuna matukio mengi ya kushangaza yaliyowahi kutokea hapa ulimwenguni ambayo yanaonesha utukufu na ukubwa wa Allah ‘Azza Wajallah’. Kitendo cha watoto watatu tofauti akiwamo Isa bin Maryam kuongea wakiwa wachanga kinaonesha kuwa Allah Mtukufu ana uwezo wa kufanya atakalo na apendalo.

Mtoto anaweza kumuongoza mzazi wake

Si jambo la kawaida mzazi kukubali maneno anayoambiwa na mtoto wake ambaye hajafikia umri wa kue – lewa mambo. Kuna wakati mtoto huzungumza mambo muhimu lakini mzazi hamsikilizi akifikiri kwamba kile anachokisema si sahihi na hakina faida kwake.

Wasichokijua watu wengi ni kwamba, wakati mwingine Allah huwapa watoto taufiki ya kuweza kuzungumza mambo mazuri ambayo baadhi ya watu wazima hawawezi kuyazungumza. Tunatakiwa tuwe karibu na watoto wetu, tuthamini mawazo yao na pale wanapopatia na kufanya vyema tuwapongeze ili wapate nguvu na ujasiri wa kufanya vizuri zaidi.

Katika tukio hili tumeshuhudia mtoto mchanga akimtanabahisha mama yake kwamba mtu aliyekuwa amempanda mnyama ana tabia mbaya, ni mjeuri na hana thamani mbele za watu ingawa alikuwa mwenye mvuto mbele za watu.

Wanadamu tunatakiwa kuthaminiana na kuheshimiana na tunaposikia maneno, tetesi, uvumi au taarifa yoyote tuifanyie uchunguzi ili kubaini ukweli wake.

Allah anatuambia: “Enyi mlioamini! Akikujieni (mpotovu) na habari yoyote, ichunguzeni (kwanza), msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda.” [Qur’an, 49:6]. Tukifanya hivyo tutaweza kulinda utu na heshima za watu mbele ya jami

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close