8. Wema Waliotangulia

Dunia uwanja wa matendo, Akhera malipo

Dunia ni miongoni mwa viumbe vya Allah, ambavyo mwanadamu huishi ndani yake. Maisha ya mwanadamu, tangu kuzaliwa mpaka kufa kwake ni maisha yenye mitihani na majaribu mbalimbali.

Allah ‘Azza Wajallah’ ameyataja maisha ya dunia kama maisha ya muda mfupi pale aliposema: “Na siku kitakaposimama kiyama, wakosefu wataapa kwamba hawakukaa duniani ila saa moja tu. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakipotezwa.” [Qur’an, 30:55]. Maisha ya dunia ni maisha ya mchezo, kujifaharisha na kupumbaza.”Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, pumbao, na pambo, na kujifaharisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na Watoto.” [Qur’an, 57:20].

Pamoja na wasifu huo, hapa duniani ndipo mahala pa kutenda mambo mema yenye kunumnufaisha mwanadamu katika maisha ya akhera.

”Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!” [Qur’an, 99:7–8].

Uhusiano wa mwanadamu na maisha ya akhera

Hakika maisha ya dunia ni ya kudumu na ya milele. Allah anatuambia:

“Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima.” [Qur’an, 40:39].

Huko (Akhera) ndiko ambako wanadamu wataulizwa juu ya waliyokuwa wakiyatenda duniani, na baada ya hapo yatafuata malipo. Allah anasema:

“Tutawahoji wote, kwa waliyokuwa wakiyatenda.” [Qur’an, 15:92–93]

Kwa msingi huo, mafungamano yaliyopo kati ya mwanadamu na maisha ya akhera ni kuhojiwa na kulipwa pepo au moto kutokana na yale aliyoyafanya katika maisha ya dunia. Kila mtu ataulizwa kikamilifu juu ya matendo yake aliyoyafanya hapa duniani. Ewe mja wa Allah, tambua kuwa siku moja utasimamishwa katika uwanja wa hukumu na kulipwa kulingana na yale uliyoytaenda hapa duniani.

Jukumu la mwanadamu

Hapana shaka kuwa kuna mafungamano makubwa kati ya majukumu ya maisha ya sehemu zote mbili, yani maisha ya kilimwengu na malipo ya akhera. Hii ni kwa sababu, majukumu ya mwanadamu hapa duniani ndiyo malipo yake katika maisha ya akhera. Majukumu hayo yanaanza kwa mtu mmoja na kumalizikia kwa watu wengine.

Majukumu ya mtu katika nafsi yake

Allah amempa mwanadamu neema nyingi ikiwamo ufahamu, kuona na kusikia. Pia, Allah amempa mwanadamu uwezo wa kiwiliwili na kiroho ili aweze kutumia neema za Allah katika kutekeleza jukumu aliloumbiwa, yaani kumuabudu Allah.

Mwenyezi Mungu anasema: “Anayeongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anayepotea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.” [Qur’an, 17:15].

Kutekeleza yanayowanufaisha watu ni hatua muhimu ya kujiandalia malipo mema huko Akhera. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie] amesema:

“Hakika nafsi yako ina haki juu yako.” [Bukhari].

Majukumu ya kifamilia

Kuna majukumu mengi ya kifamilia na kila mtu atakwenda kuulizwa kulingana na nafasi yake katika familia. Kuna majukumu ya wazazi kwa watoto na watoto kwa wazazi, majukumu ya mume kwa mke na mke kwa mume. Mtume ametuambia:

“Nyinyi nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa kwa alichokichunga.” [Bukhari na Muslim].

Ukiitazama familia kwa undani wake, utagundua kuwa ndugu wanaoizunguka familia wana majukumu makubwa katika familia zao.

Jukumu la kila mtu katika jamii na umma kwa ujumla

Hapa tunazungumzia nafasi ya mtu katika jamii anayoishi, jamii ambayo inawakilisha kundi kubwa la watu na familia zao. Kila mtu katika familia anao mchango katika kutengeneza au kuharibu jamii inayomzunguka.

Kila mtu anatakiwa afanye mambo mema kwa manufaa yake na wengine na si kwa maslahi binafsi. Hapa tunaizungumzia nafasi ya mtawala kwa raia wake au raia wenyewe kwa wenyewe.

Ni wajibu kwa mwenye mali kumsaidia mnyonge na tajiri kumsaidia fukara na masikini. Pia viongozi wana wajibu wa kusimamia rasilimali zilizopo vizuri kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Jukumu la wanadamu kwa viumbe wengine

Kwa kuzingatia kuwa mwanadamu ni kiongozi katika ardhi hii, Allah amempa akili na maarifa mazuri kuhakikisha kuwa anasimama katika nafasi yake kama kiongozi kwa viumbe wengine, wakiwamo wanyama, ndege na mimea.

Mtume (rehema na mania ya Allah imshukie) amesema: “Hakika Allah amewajibisha wema juu ya kila kitu.” Kwa hivyo, mtu anatakiwa awafanyie wema wanadamu wenzake na viumbe wengine kwa kiwango alichowezeshwa na Allah.

Akhera ni uwanja wa malipo

Kama tulivyotangulia kusema, jukumu kubwa la mwanadamu katika maisha ya akhera ni kujibu maswali yanayotokana na utekelezaji wa majukumu yake hapa duniani.

Majibu hayo ndiyo yatakayopambanua mwelekeo wake  ima kwenda peponi au motoni. Katika majukumu ya kilimwengu, watu hushirikiana kwa pamoja, lakini Siku ya Kiyama hawataweza kushirikiana katika harakati za kujinasua na adhabu ya Allah. Kila mtu atasimama mwenyewe na atakuwa anahangaikia nafsi yake mwenyewe. Allah atawaambia wanadamu siku hiyo:

“Nanyi mlitujia wapweke kama tulivyokuumbeni mara ya kwanza. Na mkayaacha nyuma yenu yote tuliyokupeni. Na wala hatuwaoni hao waombezi wenu, ambao mlidai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika mahusiano baina yenu, na yamekupoteeni mliyokuwa mkidai.” [Qur’an, 6:94].

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close