8. Wema Waliotangulia

Ashura ni siku ya furaha, siyo huzuni

Siku ya Ashura ina nafasi kubwa katika maisha ya Waislamu bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Ni siku ambayo kila mmoja anajaribu kuielezea kupitia vyanzo (dalili) mbalimbali ambavyo anaitakidi kuwa ni sahihi kwa mujibu wa mafundisho yaliyomfikia.

Lakini ukweli unabaki pale pale kuwa wapo wanaoielezea siku hii kwa usahihi na wapo wanaokosea. Ilivyo ni kwamba, ili jambo lionekane dhahiri kuwa ni sahihi katika dini, ni lazima litokane na dalili (vyanzo) sahihi ambavyo ni Kitabu cha Allah (Qur’an) na Sunna za Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie).

Kwa hiyo, yeyote atakayefanya amali (jambo) ambalo halijaelekezwa katika Qur’an na Sunna, atakuwa amekosea hata kama atatumia fedha na elimu yake kuwaaminisha watu kuwa jambo analofanya ni sahihi. Ni makosa katika dini kuamua kufanya jambo kwa utashi binafsi.

Hisia za furaha

Kila ifikapo siku ya Ashura (tarehe 10 Muharram), baadhi ya watu hukumbwa na simanzi na majonzi huku wengine wakiwa na furaha. Kundi la Ahlus Sunnat wal–Jama’ah hudhihirisha furaha yao katika siku hiyo kwa kufanya ibada, kama alivyofanya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Ibada kubwa ambayo kundi la Ahlus Sunnat wal–Jama’ah huifanya siku ya Ashura ni kufunga kwa ajili ya kumshukuru Allah kwa kumuokoa Nabii Musa na watu wake kutoka kwenye makucha ya Fir’auni.

Abdullahi bin Abbas anasimulia kwa kusema: “Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) alifika katika mji wa Madina akawaona Mayahudi wanafunga (swaumu) siku ya Ashura, akawauliza: “Kwa nini mnafunga siku hii?” wakasema: “Hii ni siku tukufu ambayo Allah alimuokoa Musa na kaumu (watu) yake, na akamzamisha Fir’auni na wafuasi wake. Musa alifunga siku hii kumshukuru Allah, nasi tunafunga.” Mtume akasema: “Sisi tunamsitahiki zaidi Musa kuliko nyinyi.” Mtume akafunga siku hiyo na akaamuru watu wafunge.” [Bukhari].

Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa kundi la Ahlus Sunnat wal–Jama’ah limeihusisha siku ya Ashura na kile ambacho Mtume alikiridhia na kukifanyia kazi. Mtume alifunga na kushukuru kama alivyofanya Nabii Musa (amani ya Allah imshukie). Na huu ndiyo muongozo wa Mtume katika siku hii ya Ashura, siku ya ukombozi kwa Musa.

Hisia za kuhuzunisha

Wakati kundi la Ahlus Sunnat wal–Jama’ah likiiadhimisha siku ya Ashura kwa kufunga, kwa upande mwingine lipo kundi la wale wanaoihusisha siku ya Ashura na kifo cha mjukuu wa Mtume Muhammad, Hussein bin Ali.

Wao wameamua kuiadhimisha siku hii kwa kuifanya kuwa ni siku ya maombolezo na kumbukumbu ya kifo cha Imamu Hussein, wakaifanya siku ya kuvaa nguo nyeusi, kuomboleza, kulia na kujiumiza kwa kujipigapiga sehemu mbalimbali za miili yao.

Wameifanya siku hii kuwa ya majuto, lawama, kuyapa kipaumbele mambo yasiyokubalika katika dini na kuwasema vibaya Maswahaba wa Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie).

Kumbukumbu za vifo

Katika maisha yake hapa duniani, Mtume (rehema na amani zimshukie) alifiwa na watu wengi wakiwamo wa familia yake. Si hao tu, pia wapo Maswahaba waliouawa na makafiri kwa dhuluma, lakini hatukuwahi kusikia kuwa Mtume alijiumiza kwa kujipigapiga katika mwili wake kwa sababu amefiwa.

Mashaka yanakuja pale tunapowaona baadhi ya watu wanayafanya haya kwa nembo ya Uislamu. Huku ni kuwapoteza watu wasifuate njia ya haki.

Ashura ilikuwepo

Imethibiti katika sheria kuwa mtu akifunga siku moja (kama hii ya Ashura) anafutiwa madhambi yake ya mwaka mzima uliopita. Mtume amesema:

“Funga ya siku Ashura, nategemea kwa Allah itafuta madhambi ya mwaka uliopita.” [Muslim]. Hii ni fadhila kubwa kutoka kwa Allah.

Pamoja na hivyo, ifahamike wazi kuwa Mwenyezi Mungu husamehe madhambi madogo tu kwa mtu aliyefunga siku ya Ashura. Kwa madhambi makubwa, ni lazima mtu alete toba ili Allah amsemehe.

Mtu anayefunga Sunna ya Ashura hufutiwa madhambi yake madogo na kama hana huenda akafutiwa makubwa, na kama hana ‘Inshaa Allah’ Mwenyzi Mungu atampatia thawabu.

Ikiwa Mtume amezungumzia fadhila na utukufu wa siku hii ya Ashura, vipi tunakubali kuyumbishwa na watu walioigeuza siku hii kuwa ya maomboilezo, huzuni, maandamano na kelele za masikitiko kwa kigezo kwamba wanatukuza na kuonesha upendo kwa familia ya Mtume? Hivi huu ni upendo wa kweli au ni kujaribu kuwahadaa Waislamu wafuate mipango ya watu?

Allah ‘Azza Wajallah’ ametubainishia wazi kuwa Waumini wa kweli ni wale wanaofuata mwenendo wa Mtume wake (rehema za Allah na amani imshukie).

Mwenyezi Mungu anasema: “Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu, basi nifuateni mimi (Muhammad). (Mkifanya hivyo) Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 3:31].

Show More

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button
Close
Close