2. Deen

Wala msife ila mmekuwa Waislamu (Qur’an, 2:103)

Katika tamko hilo, amri ya kumcha Mwenyezi Mungu na kufa Muislamu inaelekezwa kwa Waumini, hivyo kuonyesha jinsi Uislamu unavyoweka umuhimu mkubwa, si tu katika maisha mazuri, bali pia kifo kizuri.

Katika mazingira hayo, Waumini wanaonywa dhidi ya kubweteka, hali inayoweza kuwapeleka kwenye mwisho mbaya. Watu wengi wanajaribu kukwepa kuzungumzia kifo, licha ya ukweli kwamba kifo ni moja miongoni mwa vitu vichache katika maisha ya mwanadamu, ambavyo uhakika wake wa kutokea ni asilimia mia moja.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa wote sisi tunatamani kifo kizuri. Kwa hiyo, kifo kizuri ni nini? Taasisi ya tiba inaainisha kifo kizuri na chenye heshima kama ifuatavyo:

“Kifo kizuri ni kile ambacho hakina dhiki inayoepukika na mateso kwa wagonjwa, familia, na watoa huduma kwa mgonjwa.” (Institute
of Medicine, IOM 1997).

Watu wengi wangependelea kifo kisicho na maumivu. Baada ya kuishi maisha yao kikamilifu, wakitimiza ndoto zao, wangetamani kufa wakifanya kile walichopendelea zaidi. Kama Waislamu, matamanio yetu kwa ujumla ni kama hayo, hata hivyo lengo la maisha yetu ndiyo hasa linalotuamulia kifo gani ni kizuri na kipi si kizuri. Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema ndani ya Qur’an: “Na sikuwaumba majini na watu ila
waniabudu.” (Qur’an, 51:56)

Kwa hiyo, roho iliyoumbwa kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu lazima pia ife katika hali hiyo, ili iweze kufanikiwa kupata kifo kizuri. Kwa namna hiyo, tunastaajabu mwisho wa wale waliojikita katika vitendo vya ibada, wakati walipokuwa wakikata roho, kama ilivyotajwa na Imamu Adh-Dhahabi (Allah amrehemu) katika kitabu
chake mashuhuri, ‘Siyar A’lam An-Nubala:’

Abu Bakr bin al-Ismaili alifariki siku ya Alhamisi usiku wakati wa Swala ya Maghrib, akisoma Surah Al-Fatiha, ‘Wewe tu ndiye tunayekuabudu na Wewe tu ndiye tunayekuomba msaada.’

“Abu Hakim Abdullah bin Ibrahim al-Khabri alikuwa akiandika Qur’an, kisha aliweka chini kalamu yake na kusema: “Hakika hiki ni kifo cha furaha!” na akafariki dunia.

Mus’ab alisema: “Amir bin Abdullah bin Az-Zubair alisikia wito wa Adhana na akasema, ‘Nishike mkono’ akaambiwa, ‘Lakini wewe ni mgonjwa,’ ambapo alijibu, ‘Vipi naweza kusikia wito wa Allah halafu nisijibu?’ Kwa hiyo, wakamshika mkono akaingia msikitini ” pamoja na Imamu kwa ajili ya Swala ya Maghrib. Wakarukuu pamoja kisha akafariki dunia.”

Hiyo ni baadhi ya mifano mizuri ya mwisho mwema kutoka kwa wenzetu waliotangulia, ukiachilia kile tunachojua kutoka kwenye mwisho mwema wa baadhi ya Maswahaba. Mfano uliowekwa na watu hawa na jitihada zao ambazo zimeigwa takriban zama zote na wale wanaotafuta radhi za Mwenyezi Mungu, vinasimama kama ukumbusho wa wazi kwetu sote kuhusu lengo hasa la maisha.

Kadri tunavyojitahidi kutenda mema kwa ajili ya watu, kuwaridhisha na kutaka kukubalika, kuwaletea manufaa na kuwaepushia maumivu na madhila; hatupaswi kupoteza ukweli kwamba lengo letu kuu ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.

Kama mifano hiyo hapo juu ilivyoonyesha, watu hawa watukufu wangeweza kuchukua maslahi yaliyokuwa mbele yao, lakini walichagua kujipinda katika kutafuta malipo makubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu. Allah ‘Azza wa Jalla’ atupe msimamo na mwisho mwema na atufanye tuwe miongoni mwa wale wanaoheshimika:

Akaambiwa, ‘Ingia Peponi! Akasema: Laiti watu wangu wangelijua, Jinsi Mola wangu Mlezi alivyonisamehe, na akanifanya miongoni mwa walioheshimiwa,” (Qur’an, 36:26-27)

“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha, wala msife ila mmekuwa Waislamu,” (Qur’an, 2:103).

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close