7. Visa Vya Mitume

Wasia mzito wa Mtume kwa wanawake

K ama inavyoeleweka, Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) aliletwa kwa watu wote. Mafunzo yake yaliwahusu wote – wanaume na wanawake pia. Kutokana na ukweli huu, Mtume alifanya juhudi za makusudi za kuwaelimisha, kuwaonya na kuwaongoza wanawake katika vikao vyao ama darsa maalumu alizoziitisha kwa ajili yao tu.

Katika makala yetu hii, tutaipitia moja ya hadith zinazothibitisha hilo na kisha tuifafanue na kuchukua mafunzo yanayopatikana ndani yake. Mtume wa Allah alisema kuwaambia wanawake:

“Enyi wanawake, toeni sadaka (sana) na muzidishe kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu kwani nimekuoneni kuwa ndiyo wengi katika moto.”

Mwanamke mmoja mkakamavu akamuuliza: “Tuna nini sisi mpaka tuwe wengi motoni?” Akasema: “Mnapenda kufanya (au kusema) ya laana na mnapinga mema (hisani) za wanaume zenu, na sijapata kuona wapungufu wa akili na dini wanaoweza kumteka mwanamme mwenye akili kuliko nyinyi.”

 Yule mwanamke akauliza tena: “Ni nini upungufu wa akili na upungufu wa dini tulionao?” Mtume akasema: “Ama upungufu wa akili ni kwamba, ushahidi wa wanawake wawili hulingana na ushahidi wa mwanamume mmoja. Huu ni upungufu wa akili. Na mwanamke hukaa masiku kadhaa, haswali na hula mchana wa Ramadhani (kwa dharura zake). Basi huu ni upungufu wa dini.” [Muslim]

Maelezo

Hadith hii imesimuliwa pia na Maswahaba wengine. Katika riwaya ya Abuu Said (Allah amridhie) amesema:

“Mtume alitoka kwa ajili ya sala ya Eid ya Adhhaa au ya Fitr. Kisha akawapitia wanawake baada ya hotuba yake watu wote, aliwahusisha wao tu, aliwaonya na akawakumbusha mambo mbalimbali na kuwahamasisha juu ya kutoa sadaka kwa wingi ili wajikinge na ghadhabu za Allah.”

Wanawake kuwaathiri wanaume

Katika riwaya hiyo Mtume ameeleza wazi kwamba mwanamke ana uwezo mkubwa wa kuipora (kuiteka) akili ya mwanamme hata kama alisifikana kwa ushujaa, akili na ukali. Hii hutokana na uzuri wa umbo, ulaini wa maumbile na ushawishi wake wenye mvuto mkali. Mtume ameashiria kwamba, ikiwa mwanamume makini anasalimu amri mbele ya mwanamke, basi wengine wa kawaida ni zaidi.

Wanawake kuwa wapungufu wa akili

Mtume alimaanisha upungufu wa akili wa wanawake kama tafsiri ya kauli ya Allah kuhusu kuandikana wakati wa kukopana isemayo:

“ …Na shuhudisheni mashahidi wawili katika wanaume wenu. Lakini ikiwa hakuna wanaume wawili, basi iwe mwanamume mmoja na wanawake wawili miongoni mwa mnaowakubali kuwa mashahidi, (ili0 akija kusahau (mwanamke) mmoja wao, mwengine amkumbushe…” [Qur’an, 2: 282]

Kwa hiyo, kuwepo haja ya kuongezwa shahidi wa kike katika mikataba ya kifedha ni dalili ya uchache walionao wa kudhibiti mambo mazito kama hayo. Na huo ni ndiyo upungufu wa akili.

 Upungufu wa dini

Ikiwa mwanamke anaacha sala na funga kwa siku kadhaa na kukosa kushirikiana na Waislamu wengine katika ibada hizo mbili ndani ya wakati wa asili wa utekelezwaji wake, ilhali hiyo ndizo nguzo kuu za dini kiutekelezaji, basi huo ni upungufu wa dini. Tena kwa upande wa sala, wala halipi!

Ila kwa mambo haya hawalaumiwi kwa sababu hiyo imetokana na asili ya maumbile yao. Mtume alitanabahisha tu kama kujibu suala aliloulizwa. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alitaja adhabu inayowakabili wakina mama juu ya kosa lao la kukufuru neema za waume na kukithirisha maneno na vitendo vya laana, na siyo kwa mapungufu yao ya kimaumbile. Mapungufu ya maumbile yametokana na sababu za kimaumbile zilizo nje ya uwezo wao na hawana namna ya kujiepusha nayo.

Dhana potofu za maadui wa Uislamu

Maadui wa mwanamke wa Kiislamu na Uislamu kwa jumla hujenga shub-ha (dhana tata) juu ya hadith kama hizi. Maadui hao hudai kwamba, eti mafunzo ya Uislamu yamewaonea wanawake kwa kuwapa sheria ngumu za vitisho hapa duniani na kuwatishia kwa adhabu kubwa inayowasubiri huko Akhera.

Ikumbukwe kwamba, Uislamu umemkuta mwanamke katika hali mbaya kifamilia, kiuchumi na kijamii takriban katika mataifa na jamii zote, kisha ukamkomboa. Uislamu ulimkuta mwanamke akiwa ameporwa hata haki ya kuishi kama kiumbe wa heshima, kwa mujibu wa Qur’an na hata historia.

Qur’an inasema: “Na mmoja wao anapopewa habari njema (ya kuzaliwa) mtoto wa kike husawijika uso wake akajaa sikitiko. Akawa anajificha na watu kwa sababu ya khabari ile mbaya aliyopewa, (anajishauri), ‘akaye naye juu ya fedheha au amfukie udongoni (akiwa mzima)?’ Sikilizeni, ‘Ni mbaya mno hukumu yao hiyo’” [Qur’an, 16:58-59]

Ugumu wa hukumu za sheria

Hukumu za sheria si ngumu kwa wanawake. Mwanamke amesamehewa katika mambo mengi. Akiwa katika ada yake haswali wala hafungi. Ameamrishwa kubaki nyumbani kwake ili autunze utu wake na amtii mume wake. Uislamu umemtukuza mwanamke na ndiyo maana hajalazimishwa kutoka na kuhangaikia maisha. Mke na watoto wake wanahudumiwa na mumewe kwa haja zake zote.

Ama kwamba wao ndiyo wengi katika moto kama ilivyobainishwa, Mtume ametaja wazi sababu ya hayo katika khutba yake alipoulizwa na baadhi yao. Mtume alisema, wao huzidisha kuwalaani na hukanusha wema wanaofanyiwa na waume zao, jambo ambalo linashuhudiwa na kila mmoja wetu. Vilevile, vitendo vya laana kama vile: uongo, matusi, umbea, usengenyi kwao pia ni vingi zaidi.

Mwanamke anaweza hata kumuapiza mume wake kwa kumwambia: “Mungu asikurejeshe hapa ila kwa mikono mingi (ukiwa umeshakufa)” au “Mungu akupe balaa dunia nzima ijue.” Pia, mwanamke anaweza kumuapiza hata mtoto wake mwenyewe kwa kumwambia: “Maluuni mkubwa we.”

Haya, na yanayofanana nayo, ndia yanayowatia hatiani ndugu zetu hawa. Allah atuhifadhi na awahifadhi na wao.

Wanawake aliowasemesha Mtume walielewa anachokikusudia aliposema kuwa, wao ndiyo watakaokuwa wengi motoni Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atukinge.

Kutokana na kumuelewa huko Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), katika mapokezi mengine ya hadith tuliyoirejea, walilifanyia kazi haraka agizo lake la kutoa sadaka kwa wingi. Inasemekana walivua mpaka baadhi ya mapambo yao na kuyaweka katika shuka kwa ajili ya sadaka aliyoishika Bilal (Allah amridhie).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close