7. Visa Vya Mitume

Uislamu umekuja kumkomboa mwanamke – Sheikh Dkt Qahtwan

Imeelezwa kwamba Uislamu umekuja kumtukuza mwanamke na kurejesha heshima yake iliyopotea. Aidha imeelezwa kuwa, visa mbalimbali katika kitabu kitukufu cha Qur’an kuanzia wakati wa Nabii Adam hadi wakati wa Mtume wa Mwisho Muhammad, vimethibitisha namna mwanamke alivyotukuzwa kiasi kwamba, hakuna jambo lolote zuri liliofanyika bila mchango wa mwanamke.

Akizungumza katika Kongamano la Tatu la Kida’aawa la Afrika ya Mashariki, Miski ya Roho lililofanyika jijini Dar es Salam, msomi kijana wa Kiislamu, Sheikh Dkt. Salim Qahtwan amesema kitabu kitukufu cha Qur’an kimeonesha mfano wa nafasi ya mwanamke ilivyo.

Sheikh Dkt Qahtwan ambaye ana Shahada ya Uzamivu katika fani ya sheria, alisema, hakuna jemedari yeyote ambaye amefanikiwa pasi na uwepo wa msaada wa mwanamke na kuongeza kuwa, nyuma ya watu wote ambao wamefanikiwa katika kaumu mbalimbali walikuwepo wanawake wema.

Akifafanua juu ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alivyokuwa akiwajali na kuwapa nafasi wanawake, Sheikh Dkt Qahtwan alisema Mtume alikuwa anawajali wanawake hata wa ngazi ya chini, akitoa mfano wa mwanamke mfanya usafi msikitini ambaye ilitokea Mtume akawa hamuoni.

Mtume alipouliza, alimbiwa kuwa alifariki usiku wa jana lakini Maswahaba walishindwa kumwambia Mtume kwa sababu alikuwa amelala. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alienda kwenye kaburi ya yule mwanamke na kumuombea dua.

Mtume alisema, kaburi lile lilikuwa limejaa giza lakini Mwenyezi Mungu aliingiza nuru baada ya dua kumuombea dua. Dkt. Qaitwan alisema licha ya nafasi ndogo ya mwanamke yule ya kufanya usafi msikitini, Mtume alimjali.

Hivyo, Uislamu unawathamini watu wa jinsia zote kwa usawa. Sheikh aliongeza kuwa, Qur’an  inamtaja mwanamke kama mtu mwenye upeo wa hali juu anayeweza kusaidia kufikia malengo ya kimaendeleo. Sheikh Qahtwan pia alisema, wakati wa Musa, katika hatua zake zote alizopitia hakuna kilichofanyika bila mchango wa mwanamke.

Akitaja mfano wa busara na akili za kuona mbali za wanawake, Sheikh Qahtwan alitoa mfano wa mabinti wa Nabii Shuaib ambao, mmoja wapo alimshauri baba yao amuajiri Nabii Musa baada ya kung’amua kuwa ni mtu mzuri .

Qur’an inasema: “Akasema mmoja katika wale wanawake, ‘Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.” [Qur’an, 28:26].

Ushauri huu ulikubaliwa na Nabii Shuaib kama inavyosema aya ya iliyofuata: “Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, hiyari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. Inshallah utanikuta miongoni mwa watu wema.” [28:27].

Dkt. Qahtwan alitaja pia sifa ya uvumilivu ya mwanamke Alisema, mwanamke ni kiumbe ambaye anavumilia mengi: njaa, shida, tabu, na ndio maana hata Mwenyezi Mungu mwenyewe ameona jukumu zito la kubeba ujauzito apewe mwanamke.

Alisema, lau jukumu hilo zito angepewa mwanaume asingeliweza na huenda leo hii dunia isingekuwa na watu maana wangekuwa wanatumia vidonge vya kutoa mimba hizo kila leo.

Mfano mmojawapo alioutoa wa uvumilivu wa mwanamke ni kutoka kwa Ummu Suleim aliyefiwa na mwanawe na kuonesha utulivu wa hali ya juu. Ummu Suleim aliwaambia watu wasimwambie taarifa mumewe Abu Talha kuhusu kifo cha mtoto wao. Mumewe aliporudi alimuacha kwanza atulie, ale, apumzike ndipo alipomwambia habari hiyo.

Sheikh Dkt. Qahtwan alisema: “Idadi ya wengi hapa nguo zenu zimepigwa pasi na mwanamke. Maisha ya wajawema yaligubikwa na wanawake wema. Muangalie Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kupitia kwa Bi. Khadija aliweza kumpa mawazo mazuri mtume kabla ya utume na baada ya utume na kufanikiwa katika kazi zake.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close